Dili iliyokufa - 46
ILIPOISHIA
“Ninachoamini mimi ni kuwa hiyo damu anafyonza yule mganga labda kwa sababu ya masharti ya uganga wake. Na kwa imani yake yeye anaweza kufanya hivyo kwa usalama tu ingawa mtu mwingine asingeweza”
“Mambo haya ya kishirikina wanayaelewa washirikina wenyewe. Unapotaka kuyaingiza katika akili za kibinaadamu hayaingii. Unaweza kubishana mpaka kesho” aliyesema alikuwa polisi mmoja aliyekuwa kimya muda wote akisikiliza yale mazungumzo.
SASA ENDELEA...
Mpaka magari mawili ya polisi yalipofika hapo, ilipita saa moja hivi. Gari moja lilikuwa lile la kwanza na la pili lilikuwa gari tofauti. Polisi wengine wawili walikuwa katika gari la pili.
Safari hii ilichukuliwa ile miili ya watu waliofukuliwa na kupakiwa kwenye gari la pili. Vitu vingine vilivyochukuliwa vilikuwa pamoja na vile vyungu na vitu vingine ambavyo polisi waliona vinafaa kuchukuliwa.
Mimi na mume wangu tulipakiwa katika gari jingine ambalo lilitangulia kuondoka. Ile miili ya watu ilipelekwa hospitali.
Tulipofika kituo cha polisi tulishuka na kuingizwa ndani ya kituo. Tulimkuta yule mganga na wake zake wakiendelea kuhojiwa.
Nyuso zao zilikuwa zimevimba na macho yalikuwa mekundu. Bila shaka ilikuwa kwa sababu ya vibao walivyokuwa wanapigwa na polisi wakati wanahojiwa.
Wakati tunaingia, mkuu wa kituo, ambaye alikuwa pamoja na polisi watatu, aliniambia:
“Hebu tueleze aliyekupeleka kule mlikokutwa ni nani?”
“Ni huyu hapa.”
Nikamwonesha mke mkubwa wa mganga.
“Na huyu mwenzake alikuwa wapi?” Mkuu wa kituo alimkusudia mke mdogo wa mganga.
“Niliporudi nyumbani kwao ile jioni huyo sikumuona, sijui alikuwa amekwenda wapi. Nilikuja kumuona kule kule mzimuni akiwa na polisi.”
“Mimi mwenyewe nilikuwa naumwa. Nilikuwa nimelala. Nikaona polisi wamekuja na kuniambia niwapeleke alikokwenda mume wangu,” mke mdogo wa mganga huyo akasema.
“Kama wewe hukuwa njama moja na mume wako, ulijuaje kama alikwenda mzimuni kwenu?” Mkuu wa kituo akamuuliza mwanamke huyo.
“Alipoondoka aliniaga.”
“Alikwambia anakwenda huko kufanya nini?”
“Hakuniambia.”
“Lakini wewe ulijua alikwenda kufanya nini?”
“Sikujua...”
Kabla hata hajamaliza kauli yake akala kibao.
“Sema... ukijaribu kuficha kitu utajuta!” Mkuu wa kituo alimwambia.
“Alikuwa... alikuwa... anakwenda kula karamu yake,” mwanamke huyo akasema kwa kigugumizi.
“Kulikuwa na karamu kule?”
“Majini yake ndiyo walimwambia wanataka...”
“Sema! Walimwambia wanataka nini?”
“Wanataka kumfyonza damu...”
“Kumfyonza nani?”
Yule mwanamke akanionesha mimi kwa kidole.
“Kwanini hao majini wake walitaka wamfyonze damu? Aliwakosea nini?”
“Yaani kila baada ya muda fulani wanataka damu ya mtu.”
“Huyu si alimuoa na kumfanya kama mke wake?”
“Wale majini wakimchoka mtu ndiyo humwambia amuoe, halafu siku ikifika wanataka apelekwe kule mzimuni wakamfyonze.”
“Huyo bi mkubwa wenu pia anayajua hayo?”
“Ndiyo, anayajua.”
“Una maana wewe pia ungefyonzwa damu?”
Mwanamke huyo akatikisa kichwa.
“Kwa vile mimi nilishaijua siri ile, nisingefyonzwa.”
“Tangu umeishi na huyu mume, ni watu wangapi waliofyonzwa damu?”
“Mimi nimeshuhudia watu watatu.”
“Wanaume au wanawake?”
“Wanawake.”
“Aliwapata wapi?”
“Walikuja kutibiwa halafu akawaoa. Mwisho wa siku akaenda kuwafyonza.”
“Akishawafyonza miili yao anaifanyia nini?”
“Anaizika kwenye mzimu wake.”
“Hapo unaposema kwenye mzimu wake, wamefukuliwa watu wanne wasio na vichwa. Ni kina nani wale?”
“Ndiyo hao wake zake aliowafyonza damu.”
“Mimi pia nilipokwenda nyumbani kwao kwa mara ya kwanza nilimkuta mwanamke mwingine ambaye baadaye sikumuona, lakini sura yake inafanana na moja ya sura za vile vichwa vilivyokutwa kule,” nikamwambia yule mkuu wa kituo.
“Eti yuko wapi huyo mwenzenu?” mkuu huyo wa kituo akamuuliza mwanamke huyo.
“Naye pia alifyonzwa damu na kichwa chake ndicho alichokiona,” mke mdogo wa mganga akamjibu.
Mkuu wa kituo hicho akatikisa kichwa kwa masikitiko.
“Nyinyi mlikuwa mnafurahia hivyo vitendo?”
“Mimi sikuvifurahia, lakini nilikuwa sina la kufanya.”
“Kwanini hukuja kituo cha polisi kutoa ripoti kuwa kuna hiki na hiki?”
“Nilikuwa naogopa kuuawa.”
“Ulikuwa unaogopa kuuawa na nani?”
“Na huyo mume wetu. Aliwahi kuniambia kuwa nikitoa siri ya pale ndani, majini yake wataniua.”
“Kwa hiyo na leo utakuwa tayari mkanyongwe nyote?”
“Mimi sikuwepo wakati akifanya hayo mambo yake.”
“Sisi pia hatukuwepo. Lakini nyote tutawashitaki.”
Mkuu wa kituo akaagiza mwanamke huyo apelekwe mahabusu. Baada ya kupelekwa mahabusu akamtazama mwanamke mwingine ambaye alikuwa mke mkubwa wa mganga huyo.
“Wewe ulituambia kuwa hujampeleka huyu mwenzenu kule mzimuni, wakati mwenyewe nimemuuliza hapa amesema kuwa wewe ndiye uliyempeleka,” mkuu huyo wa kituo akamwambia mwanamke huyo.
“Sikumpeleka, ila tulikwenda pamoja. Sote tuliambiwa na mume wetu twende huko.”
“Mliambiwa mwende huko kufanya nini?”
“Mganga mwenyewe alituambia twende. Sijui alitaka tufanye nini,” mke mkubwa wa mganga alijibu.
“Ulikuwa hujui mnakwenda kufanya nini?”
“Nilikuwa sijui.”
“Sawa. Sasa tueleze mlipofika kule nini kilitokea?”
Mwanamke akaanza kusitasita. Bila shaka kwa vile alikuwa mwanamke, mkuu huyo wa kituo hakutaka kumpiga kibao, lakini niliamini laiti angekuwa mwanaume angekiona cha moto.
“Nakuuliza tena, mlipofika kule nini kilitokea?”
“Tuliona polisi wamekuja na kutukamata.”
“Kabla ya polisi hao kuja nini kilitokea?”
Mwanamke akanyamaza tena.
“Usinilazimishe nikutwange makofi. Nakushtukia sana...!” Mkuu wa kituo alimwambia huku akimtazama kwa macho makali.
Alipomwona mwanamke huyo bado alikuwa akisitasita alinigeukia mimi.
“Mlipofika kule nini kilitokea?” akaniuliza.
Nikaeleza kilichotokea mpaka yule mganga alivyoingia katika kile chumba nilichokuwemo na kutaka kunifyonza damu.
Mkuu wa kituo, baada ya kuyasikiliza maelezo yangu, alimtazama yule mwanamke ambaye sasa alikuwa ameinamisha uso wake.
“Unajaribu kuficha ukweli. Unajifanya hujui mlikwenda kufanya nini, wakati wewe ndiye uliyeita majini wamfyonze damu mwenzenu. Na kama si polisi kuwahi kufika, huyu mwanamke angekuwa ameshakufa!” Mkuu wa kituo alimwambia mwanamke huyo ambaye hakujibu chochote.
“Ulikuwa unashirikiana na mume wako kuua watu kwa imani zenu za kishirikina!”
Mwanamke akabaki kimya.
“Hebu nieleze mmeshaua watu wangapi tukiwatoa wale watatu?”
“Ni wale wale tu, na aliyewaua ni yeye mwenyewe,” mwanamke akajibu kwa sauti ya chini.
“Aliwaua kwa kuwafyonza damu?”
Mwanamke akakubali kwa kutikisa kichwa kwa sababu ya aibu.
“Sema kwa mdomo wako, aliwaua kwa kuwafyonza damu?” Mkuu wa kituo alimkemea.
“Ndiyo, aliwafyonza damu.”
“Mnapofanya hivyo huwa mnapata faida gani?”
“Mimi sijui kwa sababu anayefanya mambo hayo ni yeye mwenyewe.”
“Unataka uniambie kwamba hajawahi kukueleza ni kwanini anafyonza watu damu na kuwaua wakati wewe ndiye mpambe wake?”
“Yeye aliniambia kwamba ndiyo masharti ya uganga wake. Yaani wale majini wake ndiyo wanaotaka damu ya binadamu.”
“Halafu wanampa nini yeye?”
Mwanamke huyo alimtazama mume wake aliyekuwa amekalishwa chini kisha akajibu:
“Hawampi chochote.”
“Nyinyi ni watu katili sana na hamthamini uhai wa watu wengine!”
“Mimi nilikuwa natekeleza amri nikiwa mke wake kwa sababu kama ningekataa angeniua.”
“Ulishindwa kwenda kumripoti kituo cha polisi?”
“Angeniua. Huyu mtu ni katili sana.”
“Mbona mwenzenu alifika hapa kituo cha polisi akaeleza ukweli na polisi tukachukua hatua hadi nyinyi mkaweza kukamatwa?”
Mkuu wa kituo aliposema hivyo mwanamke huyo alinitupia jicho kali kisha akainamisha tena uso wake.
Kama walivyoambiana na mume wake, wote walinitazama. Mume wake naye akainua uso na kunitupia jicho kali.
Nilijua ni kwanini walinitazama vile. Hawakujua ni nani aliyewatoa taarifa polisi hadi wakaja kukamatwa. Bila shaka swali hilo lilikuwa likiwatesa muda wote waliokuwa mikononi mwa polisi. Sasa baada ya mkuu wa kituo kusema kwamba mimi ndiye niliyemripoti mganga huyo polisi ndipo waliinua nyuso zao na kunitazama.
Bila shaka walikuwa wakinilaani. Na kwa upande wa yule mganga alikuwa akijiuliza nilivyopata akili hadi nikaweza kwenda kituo cha polisi wakati yeye alikuwa anaamini kuwa alikuwa ameniroga.
“Mnamtazama?” Mkuu wa kituo akawauliza kisha akawaambia:
“Hata mkimtazama hamuwezi kumfanya chochote.”