Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dili iliyokufa - 45

HADITHI - 45

ILIPOISHIA

“Maneno  ya kijinga sana.  Hebu kiondoe haraka.

Wakati mganga  anakiburuta kichanja hicho kukiweka pembeni, polisi huyo alikisukuma  kwa nguvu  na kukipindua. Polisi mwingine akasaidia kukisukuma hadi pembeni mwa  mzimu huo.

Mchanga wa mahali kilipoondoka kichanja hicho ulikuwa umetitia.

“Hapa ndipo ulipoizika hiyo miili?” Polisi akamuuliza mganga huyo.

SASA ENDELEA...


“Ndiyo.”

“Sasa utapafukua wewe mwenyewe.”

“Ngoja nikachukue shepe.”

“Kumbe una shepe hapa hapa?”

“Kuna shepe moja kule ndani.”

“Askari, nenda naye.”

Mganga akatoka akiwa anasindikizwa na polisi mmoja aliyekuwa na bunduki.

Baada ya muda kidogo wakarudi. Mganga huyo alikuwa ameshika shepe. Akaanza kuchimba mahali hapo.

Wakati akiendelea kuchimba tuliona vyungu viwili vilivyowekwa chini ya ardhi, vikiwa na mifuniko yake. Chungu kimoja kilikuwa upande mmoja wa kaburi na chungu kingine upande mwingine.

Baadaye tukaona vyungu hivyo vilikuwa vimeshikiliwa na shingo za binadamu zisizo na vichwa. Baada ya shingo hizo kujitokeza, vyungu hivyo vilianguka kwa kuwa mchanga uliovizuia ulikuwa umeondolewa.

Mganga mwenyewe alivichukua vyungu hivyo na kuviweka kando. Akaendelea kuchimba. Baada ya zile shingo, sasa tukaona mabega ya binadamu. Kadiri alivyoendelea kuchimba ndivyo miili ya binadamu ilivyojitokeza.

Tuligundua kuwa mwili mmoja ulikuwa wa mwanamke na mwingine wa mwanaume. Miili hiyo ilikuwa imesimamishwa na ilikuwa imeelekeana ikiwa imeachana umbali wa futi nne hivi.

Mpaka kaburi hilo lilipomalizika kuchimbwa, miili hiyo ikakosa kizuizi na kuanguka chini.

Katikati ya miili hiyo kulikuwa na mwili mwingine uliokuwa umelazwa kifudifudi, ukiwa wa mwanamke.

“Miili ya hivi vichwa ni hii hapa,” yule mganga akatuambia baada ya kumaliza kuchimba.

“Sasa kitendo chako cha kuwachinja hawa watu na kuwaweka hivi maana yake nini?” polisi mmoja akamuuliza.

“Ndiyo mzimu ulivyotaka.”

“Hawa watu ni kina nani?”

“Hawa wanawake walikuwa wake zangu na huyu mwanaume ni mdogo wangu,” mganga huyo alieleza waziwazi kana kwamba hakukuwa na kosa lolote.

Polisi huyo alimtandika mganga huyo kibao kikali.

“Yaani uliwachinja wake zako pamoja na mdogo wako, ukawazika hapa halafu unasema mzimu ndivyo ulivyotaka? Wewe mshenzi kweli!” polisi huyo alifoka kwa hasira.

Mganga huyo alikuwa ameinamisha uso wake akijishika shavu lake lililopigwa kibao. Kwa muda ule alionekana kama hayawani.

“Wewe ni binadamu kweli au mnyama?” polisi mwingine akamuuliza.

Mganga hakujibu. Aliendelea kujishika shavu.

“Una maana hata huyu msichana wa watu pia ungemchinja na kumzika hapa hapa?”

Polisi huyo alikuwa anamaanisha mimi.

Mganga akabaki kimya.

“Ukisikia mganga anataja mizimu, majini, sijui mashetani na makafara, ujue huyo ni muuaji, si mganga. Ukienda kwake ujue umekwisha. Lakini nyinyi dada zetu hamsikii. Pesa zenu zinaliwa na roho zenu zinaliwa!” polisi mwingine akaniambia huku akinitazama kwa macho makali.

Alipoona nilikuwa nikimtazama kwa hofu, akaniambia:

“Unaona yaliyowapata wenzako. Usishangae hawa nao walikuwa wateja wake kama wewe!”

Wakati akiniambia hivyo nilikuwa nikifikiria kwamba maneno yake yalikuwa ya kweli. Kama si wifi yangu kwenda kwa huyo mganga na kufanyiwa dawa iliyozindua akili yangu, muda huo ningekuwa nimeshafyonzwa damu na kuchinjwa, na pengine ningekuwa nimezikwa katika kaburi lile lile ambalo mwenyewe analiita mzimu.

Kweli baadhi ya hawa waganga si watu wa kuaminika. Ikanijia picha akilini ya uso wa yule mganga wakati alipokuwa anataka kunifyonza damu. Sura yake ilikuwa imebadilika na kuwa kama ya shetani. Sikujua kwa nini ilibadilika na kuwa vile.

Lakini ilitosha kunifanya niamini kuwa baadhi ya hawa waganga si binadamu kama alivyosema yule polisi.

“Sasa utawabeba wewe mwenyewe hawa maiti wako na kuwapeleka kwenye gari,” yule polisi aliyenionya akamwambia yule mganga.

Mganga hakupata hata kinyaa. Akaanza kubeba maiti moja moja na kutoka nazo huku akisindikizwa kwa bunduki.

Alipomaliza kutoa zile maiti, polisi mwingine akamuuliza:

“Ndani ya hivi vyungu kuna nini? Hebu funua tuone.”

Mganga huyo alipoambiwa hivyo alichutama haraka, akasema maneno ambayo hayakueleweka, kisha akafunua chungu kimojawapo.

Alipokifunua kwanza kulitokea harufu mbaya kama ya kitu kilichooza, kisha wakatokea wadudu. Wadudu hao waliokuwa na mbawa waliruka mmoja baada ya mwingine kutoka kwenye chungu hicho na kusambaa angani, jambo ambalo lilitusababishia tafrani kubwa.

Mganga huyo alipokuwa anakwenda kufunua chungu cha pili, polisi aliyemwambia afunue vyungu hivyo akamzuia kwa mtutu wa bunduki.

“Acha... acha... acha...!”

Tulikuwa tunawapepeta kwa mikono wale wadudu waliokuwa wakiturukia. Alhamisiurina hawakutuumiza.

Yule polisi akasema:

“Askari mwenye pingu, mtie pingu huyu mtu. Anaweza kutukimbia sasa hivi. Nimeshaona ishara mbaya.”

Mara moja mganga huyo akatiwa pingu mikononi.

“Sasa tutoke humu.”

Tukatoka ndani ya ule mzimu. Vile vyungu tuliviacha kule kule.

Aliyekuwa kiongozi wa ule msafara, ambaye alikuwa na tepe za ukoplo, alipiga radio call kwa polisi wenzake waliokuwa kituoni na kuwaeleza hali waliyokutana nayo, kisha akaomba msaada wa gari jingine kwa ajili ya kuibeba ile miili ya watu.

Alipomaliza kuzungumza alituambia:

“Kwa hapa tulipo si rahisi kwa wenzetu kuja na kufahamu tulipo. Kwa hiyo itabidi baadhi yetu waondoke na hawa watuhumiwa. Wataondoka polisi watatu.”

Polisi hao walipokubaliana hivyo, polisi watatu wakaondoka na wale watuhumiwa, lakini yule kiongozi wao alibaki na polisi wengine wawili.

“Jamani, huyu mganga ni hatari!” polisi huyo akatuambia baada ya wenzake kuondoka.

Akaongeza:

“Mimi sijawahi kuona mganga wa kienyeji anayewachinja wateja wake.”

“Inavyoonekana ni kwamba huyu mganga anapompenda mteja wake anamfanyia dawa ya kumzuia akae kwake, lakini lengo lake ni kumtoa kafara kwa ajili ya majini yake,” mume wangu akasema.

“Sasa huo ndio uganga gani? Kama unakumbuka, alituambia mmoja kati ya wale watu aliowafukua ni mdogo wake.”

“Makafara mengine unatakiwa utoe mtu anayekuhusu sana,” polisi mwenzake akasema.

“Sasa huo ni uchawi!” kiongozi wa polisi hao akamwambia.

“Ukiangalia dhana nzima ya uganga wa kienyeji ni kama uchawi tu.”

“Sasa vinatisha. Anawakata vichwa watu na kuwabebesha vyungu ndani ya shimo halafu anasema ni matakwa ya mzimu. Yule mtu ni mzima kweli?” kiongozi wa polisi hao aliendelea kushangaa.

“Mnajua kuna kitu kimoja hamjakizingatia,” nikawaambia wale polisi.

“Kitu gani?” mume wangu ndiye aliyeniuliza.

“Wakati naletwa hapa na kuingizwa katika kile chumba mlikonikuta, yule mke wa yule mganga aliniacha na kutoka. Baadaye nikaisikia sauti yake katika chumba cha pili akiwaita majini yao ili waje wanifyonze damu. Baadaye tena nikamwona yule mganga ameingia katika kile chumba nilichokuwamo akanishika kwa ajili ya kunifyonza, lakini sura yake ilikuwa tofauti.”

Nilimeza mate kisha nikaendelea:

“Meno yake ya mbele yalikuwa yamerefuka na mboni za macho yake zilikuwa nyembamba, zimesimama kama za paka. Lakini polisi walipotokea na kumtoa nje akabadilika. Yale meno sikuyaona tena na zile mboni zikarudi kama za binadamu. Sasa ile ilikuwa ni nini? Tangu muda ule ninajiuliza bila kupata jibu.”

Aliyenijibu alikuwa mume wangu.

“Nafikiri yule bwana anapokuwa katika hali ile ya kumfyonza mtu, wale mashetani wake yanambadili kwa sababu mashetani hayo ndiyo yanayofyonza damu, lakini yanafyonza kupitia mwilini mwa yule mtu.”

“Hii tabia ya kufyonza damu za watu ambao hajui wana matatizo gani, si inaweza kumsababishia madhara ya kiafya?” polisi mmoja akauliza.

“Inavyoonekana wanaofyonza ile damu ni mashetani wake. Yeye hawezi kupata madhara,” mume wangu akamjibu.

“Wanafyonza mashetani wake au anafyonza yeye? Yeye si ndiye aliyetaka kumfyonza mke wako?”

“Shetani anakuwa ndani yake. Pale yeye mwenyewe anakuwa hajielewi. Shetani anakuwa amempanda kichwani na kufyonza ile damu.”

“Hata kama ni hivyo, damu itaingia tumboni kwa shetani au tumboni kwake?”

“Wenyewe wanasema inaingia tumboni kwa shetani.”

“Si kweli. Inaingia tumboni kwa mtu.”

“Unajua mtu mwenye akili timamu hawezi kufyonza damu ya binadamu mwenzake, na hiyo damu haitakaa tumboni mwake. Anaweza kutapika!”

“Ninachoamini mimi ni kuwa hiyo damu anaifyonza yule mganga, labda kwa sababu ya masharti ya uganga wake. Na kwa imani yake yeye anaweza kufanya hivyo kwa usalama, ingawa mtu mwingine asingeweza.”

“Mambo haya ya kishirikina wanayaelewa washirikina wenyewe. Unapotaka kuyaingiza katika akili za binadamu hayaingii. Unaweza kubishana mpaka kesho,” aliyesema alikuwa polisi mmoja aliyekuwa kimya muda wote akisikiliza yale mazungumzo.