Zuchu alivyomsusia Diamond Wiki ya Mwananchi
Muktasari:
- Zuchu, mziwanda wa Malkia wa Taarabu nchini, Khadija Kopa, alitumbuiza kwa nyimbo zaidi ya 10 na kuibua shangwe kubwa majukwaani huku akimsusia kimtindo Diamond Plantumz ambaye ni bosi wake pale WCB Wasafi.
SUPASTAA wa Bongofleva kutoka WCB Wasafi, Zuhura Othman Soud maarufu Zuchu ndiye alikuwa msanii kinara katika kilele cha Wiki ya Mwananchi 2025, tamasha la Klabu ya Yanga lililofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, juzi na kuhudhuriwa na mashabiki takribani 60,000.
Zuchu, mziwanda wa Malkia wa Taarabu nchini, Khadija Kopa, alitumbuiza kwa nyimbo zaidi ya 10 na kuibua shangwe kubwa majukwaani huku akimsusia kimtindo Diamond Plantumz ambaye ni bosi wake pale WCB Wasafi.
Ikumbukwe Zuchu amepata fursa ya kutumbuiza Wiki ya Mwananchi zikiwa ni wiki mbili tangu afanye kitu kama hicho katika fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) 2024 iliyopigwa Moi Kasarani, Kenya.
Tangu atoke kimuziki miaka mitano iliyopita, jina la Zuchu limekua kwa kasi na sasa akiwa mwanamuziki wa pili wa kike Afrika kwa kuwa na wafuasi wengi kwenye mtandao wa kijamii wa YouTube nyuma ya mshindi wa Grammy 2024, Tyla kutokea Afrika Kusini.
Katika Wiki ya Mwananchi, Zuchu alianza kwa kutumbuiza wimbo wake Antenna (2024) uliotayarishwa na Pablo. Huo ni wimbo wenye nguvu kubwa ya kucheza inayochanganya ladha ya Bongofleva na midundo ya Amapiano.
Ndani ya wimbo huo wa kusisimua, Zuchu aliwahimiza mashabiki wake wote kupunga hewani bendera zao kama antena, ikiwa ni baada ya kucheza na kujirusha kwa nguvu hadi kutokwa jasho mwili mzima.
Kwa mdundo wake wa kuvutia na kumshukuru mtayarishaji wake Pablo kwa ubunifu wake wa kutengeneza midundo mikali, kwake Zuchu, Antenna ni wimbo utakaojirudia mara kwa mara ukiweka hali ya furaha na nguvu kwa mashabiki muda wote.
Zuchu alimaliza shoo yake kwa kuimba laivu wimbo wake, Naringa (2023) uliotayarishwa na Trone. Huu ni wimbo wenye maana kubwa kwake akielezea jinsi anavyojivunia mchakato wa mafanikio yake na msaada kutoka kwa Mungu.
Staa huyo alitajwa kuwania MTV EMAs 2023, katika wimbo huo ameonyesha alivyoshiriki shindano la kwanza la Karioki Afrika, Tecno Own The Stage 2015, licha ya kutofanikiwa katika shindano hilo, lakini leo hii ni wanamuziki mkubwa.
Naringa unabaki kuwa wimbo pekee unaohamasisha mapambano ya maisha sio kwa Zuchu pekee bali kwa kila mtu bila kukata tamaa huku changamoto zikichukuliwa kama sababu kuu ya kuendelea kusonga mbele na kufurahia mafanikio yatakayokuja mbeleni.
Nyimbo nyingine alizotumbuiza Zuchu katika tamasha hilo la saba kwa Yanga SC ni hizi hapa pamoja na watayarishaji wake - Amanda (2025 - S2kizzy), Utaniua (2023 - Trone), Honey (2023 - LG) na WaleWale (2024 - Trone).
Mikwaju mingine aliyoichapa ni Makonzi (2024 - LG), Mwizi (2024 - Laizer), Siji (2024 - S2kizzy), Hujanizidi (2024 - Diblo Onetouch) na Baby Mpya (2025 - Don) wake D Voice, staa mwisho kusainiwa WCB Wasafi.
Ukitazama orodha ya nyimbo alizotumbuiza Zuchu, utabaini ni mmoja pekee alioshirikiana na Diamond ndio alioupa nafasi katika tamasha hilo kubwa, nao ni 'WaleWale' kutoka katika albamu yake ya kwanza, Peace and Money (2024).
Ndio sababu tunasema kamsusia Diamond kwa sababu wameshirikiana katika nyimbo tano ambazo zimefanya vizuri lakini Zuchu kaamua kuchugua mmoja tu ambao pia ndio mwisho kutoka kwao.
Ikumbukwe hapo awali, wawili hao walishirikiana katika nyimbo kama Litawachoma (2020), Mtasubiri (2022), Raha (2024) na Cheche (2020), wimbo uliofanya kituo cha televisheni huko Hispania, Lasexta kumtaja Zuchu kama Beyonce wa Afrika!
Wakati Zuchu akimsusia Diamond, alimpa nafasi msanii wenzake kutokea WCB Wasafi, D Voice ambaye walishirikiana kutumbiza nyimbo mbili ambazo ni Baby Mpya (2025) na Hujanizidi (2024), zote zikiwa na mahadhi ya Singeli.
D Voice aliyetoka na kibao chake, Kuachana Shingapi (2021) na ndipo akaja kusaniwa WCB Wasafi, baada ya Diamond, yeye ndiye msanii wa Bongofleva aliyeshirikiana na Zuchu mara nyingi zaidi.
Ndani ya albamu ya D Voice, Swahili Kid (2023) alimshirikisha Zuchu katika nyimbo mbili, Nimezama (2023) na BamBam (2023) ambao umetazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 20. Baada ya hapo zikafuata - Nani (2024), Hujanizidi (2024) na Baby Mpya (2025).