Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hatimaye Gen Z wameiona Simba ikicheza Kagame

HISIA Pict


KIPATO huleta majivuno. Huwa anasema hivyo mtangazaji wa Azam TV, Hassan Mvulla. Na ni kweli. Juzi nilikuwa natafakari ni lini nimeiona Simba wakishiriki michuano ya Kagame kama inavyotokea sasa hivi pale Kigali.


Kumbe ilikuwa ni mwaka 2018. Zamani hii michuano ya Kagame ilikuwa ni habari ya mjini. Yaani timu zilikuwa zinajiandaa kucheza michuano ya Kagame. Zilijua zinaenda vitani. Sasa hivi michuano yenyewe ndiyo mazoezi. Inafurahisha.

Zamani ungeendaje Kagame ukaanza na kikosi ambacho Simba walianza nacho katika pambano dhidi ya wale jamaa wa Mogadishu? Siku hizi hali halisi ndio hiyo. Antony Mligo alicheza kama mlinzi wa kati.

Simba wakikosa kuchukua ubingwa hawatalia. Walie kwanini na wakati wapo mazoezini? Na kama wakichukua ubingwa sidhani kama watashangilia sana kwa sababu watani wao hawajashiriki michuano hii.

Mara nyingi hawa wakubwa huwa wanafurahi zaidi wakichukua michuano ambayo na mtani alishiriki. Labda tusubiri kuona zama hizi za mitandao ya kijamii kama watani wanaweza kushangilia sana ubingwa katika michuano ambayo Jirani hakushiriki.

Yanga wao mara ya mwisho kushiriki Kagame ilikuwa mwaka 2021. Kukosa kushiriki mwaka huu sio habari kubwa. Ndio kwanza wameanza mazoezi kwa ajili ya msimu mpya. Nini kimeleta hali hii? Simba wameenda lakini kama sehemu ya mazoezi. Yanga hawajaenda kabisa.

Kisa? Siku hizi wanadharau michuano hii. Akili yao wameielekeza zaidi katika michuano ya Ligi ya mabingwa wa Afrika au wanaposhiriki michuano ya Shirikisho. Hii ndio habari kubwa kwao.

Nyakati zimetokomea wakati ule Simba walipochukua ubingwa wa Afrika Mashariki na kati mwaka 1991. Fainali ambazo mwarabu Hassan Afif alifanya mambo makubwa katika pambano la fainali dhidi ya Villa ya Uganda.

Ilikuwa habari ya kusisimua wakati Yanga walipokwenda Uganda na kutwaa kombe la Afrika mashariki na kati mwaka 1993 katika uwanja wa Nakivubo pale Kampala. Staa wa michuano alikuwa Edibily Lunyamila. Yanga waliwahi kurudia kutwaa tena kombe hilo Uganda mwaka 1998.

Sasa hivi sio habari ya kusisimua. Simba na Yanga wamewekeza pesa nyingi katika vikosi vyao kiasi kwamba hawaoni michuano hii kama ya maana. Wanachofikiria ni nani atakuwa wa kwanza kati yao kufika hatua ya nusu fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika.

Simba na Yanga wamewaacha wenzao wa Afrika mashariki na kati katika ukiwa mkubwa. Kwa sasa wamewekeza zaidi ya hawa kina Gor Mahia, AFC Leopards, Club Sports Villa, APR, Kiyovu na wengineo. Haishangazi kuona wanachoangalia zaidi kwa sasa ni ubingwa wa Afrika.

Watani wamejiweka katika viwango vya akina Al Ahly, Mamelodi, Wydad, Zamalek na wengine wa viwango hivi. Wamewahama kina Gor Mahia.

Wao sasa hivi mchezaji mmoja wanaweza kumnunua hata kwa dola laki mbili na wakamlipa mshahara wa dola 15,000 kwa mwezi.

Hata kule Afrika Magharibi hakuna timu ambazo zinafanya uwekezaji huu. Sawa sisi hatujawafikia akina Al Ahly lakini kule Afrika Magharibi hawatuwezi.

Huku ukanda wa kwetu hawatuwezi. Hata majirani wa upande mwingine akina Malawi na Zambia hawatuwezi. Wanaotuweza ni Afrika Kusini na wale jamaa wa Afrika kaskazini.

Hawa wa Afrika Magharibi sasa hivi tumeenda mbali zaidi kiasi kwamba tumewageuza soko letu la kuchukua wachezaji wazuri katika timu bora za huko. 

Ndio hawa kina Pacome Zouazoua kiasi kwamba Pacome anaweza kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ivory Coast huku kukiwa hakuna hata mchezaji mmoja wa ligi ya ndani ya Ivory Coast aliyeitwa.

Matokeo yake tunayaletea nyodo mashindano haya. Michuano ambayo tunacheza kwa shingo upande ni ile ya kisiasa kule Zanzibar.

Michuano ya Mapinduzi na michuano ya muungano. Sio kwamba klabu zinashiriki kwa moyo mkunjufu, Hapana, wanashiriki kwa sababu kuna vimemo vikali vinatembea.

Vinginevyo hawa watani hata michuano hii ya Zanzibar wasingeshiriki. Nadhani hata watu wa Bodi ya ligi huku upande wa bara wanaziruhusu timu kinyonge kwenda Unguja na Pemba kwa sababu zinaharibu ratiba zao za michuano mbalimbali ya huku. Ligi huwa inasimama.

Nini kifanyike kwa michuano ya Kagame? Labda ungetengenezwa mfumo mpya ambao ungewashawishi wakubwa. Labda mechi za michuano hii zingechezwa nyumbani na ugenini. Zikichomekewa katika wikiendi fulani kama inavyochezwa michuano ya Afrika.

Wakubwa wanaamini wana muda mfupi wa kujiandaa kushiriki michuano hiyo mikubwa mara baada ya kutangaza usajili. Mfumo ungebadilika lakini pia labda Zawadi za mshindi zingekuwa pesa ndefu zaidi kuliko ilivyo sasa.

Vinginevyo kwetu sisi michuano hii imepoteza mvuto. Ni mpaka pale Rais Paul Kagame anapoamua kuandaa ndipo tunapoona timu zikienda kushiriki. Nadhani rafiki zetu wa CECAFA hawana pesa za kutosha za kuandaa michuano hii.

Hata hivyo shukrani kwa Simba kwenda Kigali kufanya mazoezi katika michuano hii. Nadhani kuna vijana wa kizazi kipya walikuwa hawajawahi kuona Simba ikifanya hivyo. Kuanzia mwaka 2018 mpaka leo ni mbali.

Ni muda pia wa wachezaji wapya, hasa wazawa kuanza kuonyesha thamani yao mapema. Hii inaweza kuwa topiki ya siku nyingine lakini hawa wachezaji wapya wazawa wanaosajiliwa na watani wamekuwa wanyonge sana mbele ya wachezaji wa kigeni.

Huwa tunaweka matumaini makubwa kwao lakini wakianza kucheza wanatuangusha. Matokeo yake tunaendelea zaidi kutumainia wachezaji wa kigeni kuliko wazawa. Wazawa waliotoboa katika vikosi vya kwanza ni wachache. Ebu tusubiri kuwaangalia safari hii.