Wikiendi hii kamata muvi hii ya kibabe
Muktasari:
- Emily anapokea jalada namba Case 39, linalohusu madai ya wazazi wa Lilith kumdhuru dogo. Mwenyewe anaamini binti huyo yuko hatarini, hasa anapochunguza na kugundua mazingira ya kutisha yaliyopo kwa wazazi wake wakidhani wamerukwa akili kwa kupambana kumrudisha ‘motoni, kwa vile si mtoto wa kawaida.
EBWANAEE wikiendi ndo imeanza hivyo. Kwa wale wapenzi wa muvi, tuwe tunakutana hapa kila Ijumaa kupeana vituz. Hapa tutakuwa tukichambua kwa ufupi muvi ya wiki, kisha kukupa orodha ya mzigo wa kuburudika nao wikiendi nzima.
Pia tutakupa orodha ya kazi zinazotarajiwa kuachiwa ndani ya mwezi, hili mshkaji ujiandae kuzipokea kiroho safi na kuburudisha nafasi. Twende kazi...!
MUVI YA WIKI - CASE 39
EMILY Jenkins ni ofisa wa ustawi wa jamii anayeshughulikia kesi mbalimbali za kijamii, ambapo safari hii anakuja na kesi ya binti mdogo Lilith Sullivan.
Emily anapokea jalada namba Case 39, linalohusu madai ya wazazi wa Lilith kumdhuru dogo. Mwenyewe anaamini binti huyo yuko hatarini, hasa anapochunguza na kugundua mazingira ya kutisha yaliyopo kwa wazazi wake wakidhani wamerukwa akili kwa kupambana kumrudisha ‘motoni, kwa vile si mtoto wa kawaida.
Anawajulisha Polisi, wanaofika kwa wazazi wa Lilith na kuwakamata, Emily kwa huruma aliyonayo anaamua kumchukua Lilith ili akamlee kwake kwa muda. Hapo ndipo mambo yanapoanza kubadilika. Matukio ya ajabu, vifo visivyoelezeka na nguvu zisizo za kibinadamu vinaanza kumzunguka Emily na kila mtu anayemkaribia Lilith.
Unadhihirika ukweli kwamba wazazi hawakuwa wakipoteza akili, bali walikuwa wakijaribu kujilinda dhidi ya kiumbe hatari mwenye nguvu za kumiliki akili za watu na kusababisha vifo vya kutisha bila kugusa hata kidole. Emily anagundua kuwa Lilith si mtoto wa kawaida bali ni kiumbe cha kishetani, hasa baada ya kumuua rafikie, Doug na anapojaribu kupambana naye ili amuangamize ndipo muvi inaponoga.
Mzigo huu wa mwaka 2009 una muda wa dakika 109 ukiongozwa na Christian Alvart chini ya utayarishaji wa Lisa Bruce, Steve Golin na Kevin Misher.
Waigizaji wakuu wa goma hili buana ni; Renee Zellweger (Emily Jenkins), Jodelle Ferland (Lilith Sullivan), Ian McShane (Detective Barron), Bradley Cooper (Doug), Callum Keith Rennie (Jack Sullivan) na Kerry O’Malley (Margaret Sullivan).