Huyu ndiye Raja wa ile filamu ya Hatya

Muktasari:
Utamu wa filamu hiyo wala sio umahiri wa kutembeza mkono wa steringi Govinda. Hapana. Filamu hii ilisisimua wengi kutokana na mtoto mdogo wa kiume aliyebatizwa jina la Raja na Govinda aliyeigiza kama Sagar. Mtoto huyo alicheza kama mlemavu asiyesikia (kiziwi) na hawezi kuongea vilevile (bubu).
KAMA wewe ni shabiki na mpenzi wa filamu za kihindi, ni wazi umeshawahi kuicheki muvi moja matata iitwayo HATYA.
Ndio ni filamu moja kali iliyoteka mashabiki na wapenzi wa filamu za kidosi miaka ya 1990. Filamu hii iliigizwa na kutolewa rasmi mwaka 1988.
Utamu wa filamu hiyo wala sio umahiri wa kutembeza mkono wa steringi Govinda. Hapana. Filamu hii ilisisimua wengi kutokana na mtoto mdogo wa kiume aliyebatizwa jina la Raja na Govinda aliyeigiza kama Sagar. Mtoto huyo alicheza kama mlemavu asiyesikia (kiziwi) na hawezi kuongea vilevile (bubu).

Kwa wanaokumbuka dogo huyo alikuwa akijua kutamka neno moja tu, la 'Yaayaaaa' kama njia ya kumshtua Govinda aliyekuwa mtu wa mitungi, kutokana na stresi alizonazo za kutibuana na mpenziwe. Kila alipokuwa akiona shari, alitumia neno hilo kuita ili kupata msaada kwani hakuwa anaweza kuzungumza kwa tatizo lake la kuwa mlemavu wa kuongea na kusikia.
Sasa kama hujui ni kwamba, dogo huyo aliyekuwa akisakwa na kundi la maadui kutokana na kushuhudia tukio la kuuawa kwa wazazi wake kulikofanywa na kina Ranjit, hususani mama yake ambaye ni shemeji wa Govinda, lakini hawakujuana, hakuwa mtoto wa kiume.

Ndio, Raja alikuwa ni mtoto wa kike aliyeigiza filamu hiyo kama mtoto wa kiume na wengi kushindwa kuling'amua hilo mapema hadi hivi karibuni ilipokuja kufahamika kwamba alikuwa ni binti mrembo tu kama anavyoonekana kwa sasa.
Achana na kava ambalo kuna mtoto wa kiume aliyemshika miguu ya Govinda, aitwae Krushna Abhishek, ambaye hakuwa sehemu ya muvi hiyo, ila alishiriki upigwaji wa picha za kava la filamu hiyo, lakini Raja ndiye aliyekuwa akinogesha filamu kama dogo wa kiume kumbe wapi.
UKWELI ULIVYO
Jina kamili la bibie huyo mwenye umri karibu miaka 44 kwa sasa ni Sujitha Dhanush, aliyezaliwa Julai 12, 1980 katika mji wa Chennai, Tamil Nadu, India.

Sujitha alianza kuigiza filamu tangu akiwa kichanga kabisa, kazi ya kwanza kwake ikiwa ni ABBHAS aliyoingiza akiwa na umri wa siku 41 tu tangu azaliwe.
Mwanadada huyo amecheza filamu nyingi za lugha mbalimbali kama Tamil, Telugu, Malayalam, Kannada na Hindi ambayo ni hiyo ya HATYA.
Nyota huyo anaeendelea kuingiza kwa sasa, akiwa ameolewa na mfanya filamu hasa za matangazo aitwaye, Dhanush na wamejaliwa kupata mtoto wa kiume, Dhanwin wakiishia kwa sasa Huko Chennal.

Sujitha anaaendelea na kazi ya uigizaji na kwa sasa ni maarufu katika vipindi vya televisheni ya Kiasia Kusini.
Baadhi ya filamu alizoigiza ukubwani katika jinsia yake nyingi zikiwa za huko Kusini na sio Bollywood ni pamoja na Roja (1992), Valee (1999), Choonda (2003), Quatation (2004), Samanyudu (2006) na Gorintaku (2008).
SIO YEYE TU
Kama unadhani Sujitha ni mwanamke pekee aliyetumika katika filamu kama mtoto wa kiume, basi utakuwa umekosea.

Yupo bibie mwingine aliyeigiza filamu kama mtoto wa kiume wakati akiwa mdogo, naye si mwingine ila ni Ahsaas Channa, kisura mwingine anayeendelea kutamba katika fani hiyo ya uigizaji akijikita zaidi katika vipindi vya kwenye runinga.
Kisura huyo, aliyezaliwa Agosti 5, 1999 Maharashtra jijini Mumbai, India. Baba yake ni Iqbal Singh Khanna ambaye ni mtayarishaji wa filamu za ki-Punjab na mama yake ni Kulbir Badesron, muingizaji wa televisheni.
Ahsaas alianza kazi ya uigizaji akiwa na umri wa miaka minne tu na alijulikana sana kwa kucheza nafasi za watoto wa kiume katika filamu maarufu kama 'Vaastu Shastra' iliyotolewa mwaka 2004 akitumia jina la Rohan.
Pia aliigiza katika 'Kabhi Alvida Naa Kehna' (2006), 'My Friend Ganesha' (2007), akitumia jina la Ashu na Phoonk, filamu ya kutisha aliyotumia jinsia yake ya kike.
Katika filamu ya Kabhi Alvida Naa Kehna, alicheza kama Arjun, mtoto wa Shah Rukh Khan na Preity Zinta, iliyomshirikisha pia Amitabh Bachchan, Abhishek Bachchan na Rani Mukherjee, huku wengi walidhani yeye ni mvulana.
Kwa sura yake ya upole na nywele fupi, zilimfanya afae kabisa kwa nafasi hizo. Hata hivyo, baadaye aliamua kurejea kwenye utambulisho wake wa kike na sasa ni mrembo maarufu kwenye vipindi vya mtandaoni kama Girls Hostel na Hostel Daze.
Ahsaas ni mfano wa kipaji chenye mabadiliko – kutoka mtoto wa kike anayecheza kama mvulana hadi staa wa kidigitali anayeongoza kizazi kipya cha wasanii wa India.
NOMA SANA
Bila ya shaka ni kwamba kubainika kwamba waigizaji hao wawili yaani Ahsaas na Sujitha kuigiza kama watoto wa kiume ilihali ni wasichana kumeonesha namna gani filamu zina siri nyingi.
Lakini Ahsaas na Sujitha wamekuwa ni mifano nadra ya watoto wa kike walioweza kuigiza nafasi za wavulana kwa ustadi usiotiliwa shaka. Kazi zao za awali zilivunja mipaka ya kijinsia katika uigizaji na kuonyesha kuwa kipaji hakina jinsia.
Leo hii, wote wawili wamekuwa wasanii wakubwa, kila mmoja katika njia yake, lakini kumbukumbu ya kazi zao za utotoni bado ni ya kipekee na ya kuvutia, hususani wa Sujitha kupitia Hatya na namna alivyoigiza kama bubu na kunukuu neno moja tu 'Yaayaah!' akiwachanganya watazamaji waliokuwa wakinogewa na filamu hiyo.
