Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Werrason kutua Dar es Salaam kwa shoo nzito!

WERASSON Pict

Muktasari:

  • Werrason anatarajiwa kuwasili nchini akiwa na kikosi cha muziki, huku mashabiki wakitarajiwa kupata nafasi ya kushuhudia burudani ya moja kwa moja kutoka kwa mwanamuziki huyo anayefahamika kwa nyimbo na mitindo ya jukwaani inayochanganya rhumba na sebene.

BAADA ya takribani miaka minane tangu shoo yake ya mwaka 2018 jijini Dar es Salaam kukumbwa na changamoto za mvua na kusababisha mipango ya burudani kuvurugika, staa wa muziki wa rhumba na sebene kutoka DR Congo, Noël Ngiama Makanda maarufu Werrason, anatarajiwa kurejea tena nchini kwa ajili ya onyesho Novemba 6, 2026, katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki, Dar es Salaam.

Werrason anatarajiwa kuwasili nchini akiwa na kikosi cha muziki, huku mashabiki wakitarajiwa kupata nafasi ya kushuhudia burudani ya moja kwa moja kutoka kwa mwanamuziki huyo anayefahamika kwa nyimbo na mitindo ya jukwaani inayochanganya rhumba na sebene.


WERA 02

Mwaka 2018

Mwaka 2018, shoo iliyotarajiwa kufanyika Escape One, Mikocheni, Dar es Salaam, ilikumbwa na changamoto za mvua na mabadiliko ya mipango. Hata jaribio la kuhamishia burudani King Solomon Hall, Kinondoni, liliathiriwa na mvua na mafuriko yaliyofanya baadhi ya barabara kutopitika kwa urahisi. Na sasa, baada ya miaka minane, jina la Werrason linarejea kwenye burudani za Dar es Salaam kupitia Bambataa Royal Night. Hilo linavuta hisia kwa mashabiki wa rhumba na sebene ambao wamekuwa wakifuatilia muziki wake kwa miaka mingi.


WERA 03

Kuhusu maandalizi

Akizungumzia maandalizi msemaji wa ya shoo hiyo, Khamis Dacota ‘Delavida’ ambaye pia ni MC anasema yanaelekea kukamilika.

“Maandalizi mengine yote yapo hatua za mwisho kukamilika mpaka na eneo la tukio Super Dome Masaki,” anasema Dacota na kuongeza kuwa Werrason anatarajiwa kuwasili Novemba 3 akiwa na kikosi chake, huku mwimbaji Gradine Toto anayefahamika kwa wimbo Rachel Mayday akiwasili Novemba 2.

Anasema Werrason atafuatana na rapa Wassabo anayehusishwa na wimbo Kunywa Pombe, mwimbaji Catholic, dansa Cathy Yamal, kiongozi wa bendi na mpiga ngoma Papy Kakol, mpiga besi Gebe na mpiga kinanda Hugo na wengine.


Dacota, mtu wa jukwaani

Mbali na jukumu lake la kuwa msemaji wa Bambataa Royal Night, Dacota ni mmoja wa watu wanaofahamika katika shughuli za uendeshaji wa matamasha ya muziki wa dansi nchini. Uzoefu wake kwenye majukwaa ya burudani umempa nafasi ya kukutana na wasanii wa mitindo mbalimbali, wakiwamo wanamuziki kutoka Kongo na nchi zingine.

Kinachomtofautisha Dacota ni uwezo wake wa kuendana na aina ya muziki na hadhira iliyopo mbele yake. Anapokuwa kwenye matamasha yanayohusisha wanamuziki wa Kongo, uelewa wake wa lugha yao na namna ya kuwasiliana nao humsaidia kuunganisha wasanii na mashabiki, huku akijenga mazingira ya burudani jukwaani.

WERA 06

Kwa upande wa muziki wa dansi wa Tanzania, Dacota pia ana uzoefu wa kuendesha matamasha mengi ya bendi. Uelewa wake wa muziki huo, historia yake na namna mashabiki wanavyoupokea ni sehemu inayompa nafasi ya kuwa kiungo kati ya wanamuziki na watu wanaokuja kupata burudani.

Kwa hiyo, katika Bambataa Royal Night, Dacota hatakuwa tu mtu wa kutoa matangazo ya tukio, bali pia atakuwa na jukumu la kuunganisha burudani ya jukwaani na hadhira inayotarajia kushuhudia Werrason na kikosi chake.


WERA 04

Nyoshi, Bella, Msondo ndani

Werrason hatakuwa peke yake katika usiku huo, kwani wasanii wa Tanzania nao wanatarajiwa kuungana naye kutoa burudani. Miongoni mwa majina yaliyotajwa ni Bogoss Musica ya Nyoshi El Saadat, Malaika Band ya Christian Bella na bendi ya Msondo Ngoma.

Katika shamrashamra za kuelekea tukio hilo, Clouds FM imekuwa ikitembelea maeneo ambayo bendi hizo zinatoa burudani ili kujenga hamasa kwa mashabiki watarajiwa qa kuingia kwenye shoo hiyo

WERA 05

Akizungumza na Mwanaspoti Nyoshi El Saadat anasema: “Nitafanya shoo yangu, nitafurahisha watu na hata werrason aranivulia kofia kwa kusema kweli mimi king of the match , na unavyojua mimi kwenye jukwaa huwa sibahatishi kazi yangu na hata kwenye mavazi.”

Naye Christian Bella anasema: “Hadi sasa mimi na timu yangu ya Malaika band tupo tayari kwa ajili ya shoo ya Bambataa Royal Night, tumeshafanya maandalizi ya kutosha , kunachosubiriwa ni Novemba 6 kwa ajili ya kutumbuiza, tena hii imekaa vizuri zaidi  jukwaa moja na werrason kuna  tutaendelea kujifunza zaidi sisi wanamuziki aidha sisi au yeye Werrason.”

Kwa upande wa Msondo Ngoma kiongozi wa bendi hiyo, Juma Katundu anasema, “kiufupi sisi msondo Ngoma ,tunaendelea na maandalizi, na pia tumefurahi kupata nafasi kubwa hii ya kutumbuiza na wanamuziki wengine kama hivyo Werrason, Nyoshi na Bella, kwetu hatuna neno zaidi ya kwenda kutoa burudani kama kawaida yetu, msondo weee msondo raha.” Ushiriki wa bendi hizo unatarajiwa kuongeza ladha ya muziki wa dansi wa Tanzania katika tukio ambalo jina kuu ni Werrason, anayefahamika kwa mashabiki wa muziki wa Kongo.


WERA 01

‘Solola Bien’, vibao vingine

Kwa mashabiki wa Werrason, matarajio siyo kumuona tu jukwaani, bali pia kusikia nyimbo zilizojenga jina lake katika muziki wa rhumba na staili ya sebene. Miongoni mwa nyimbo zinazohusishwa na safari yake ya muziki ni Solola Bien, Kibuisa Mpimpa, Techno Malewa na Kalayi Boeing.

Hata hivyo, orodha ya nyimbo atakazopiga katika shoo ya Dar es Salaam haijathibitishwa, hivyo mashabiki watalazimika kusubiri siku ya tukio ili kuona atakachowaletea akiwa na bendi yake.