Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ulevi wa Shisha wavamia Dar

Vijana wengi hususani wanafunzi wa vyuo huchangishana fedha za kunywa viroba lakini lengo lao ni kwenda kuvuta Shisha ambapo hupokezana ulevi huo bila kujali athari za magonjwa ya kuambukiza.

Muktasari:

  • Katika ulevi wa Shisha, watengenezaji hutumia chombo maalumu chenye bomba la kutolea moshi, ambacho huwekwa tumbaku, maji na moto.

KUNA ulevi mpya umeibuka Dar es Salaam na imethibitika kwamba umeteka asilimia kubwa ya vijana wa jiji hilo. Kitaalam imeelezwa kwamba ulevi huo una athari kubwa za kiafya kwa watumiaji.

Ulevi huo ni uvutaji Shisha; Kwa mashabiki wa soka wanamkumbuka nyota wa zamani wa Arsenal, Morouane Chamakh kutoka Morocco ambaye Februari 2012 akiwa bado mchezaji Arsenal alimkera kocha wake, Arsene Wenger baada ya kufumwa akitumia ulevi wa Shisha katika klabu moja ya usiku jijini London.

Hatua hiyo iliwafanya baadhi ya wachambuzi wa soka kuutabiri mwisho wa Chamakh Arsenal kwani baada ya kutoridhishwa na kiwango chake, Shisha nayo ikakoleza moto, ikawa kama tatizo lingine lililomponza, na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwani Chamakh hakudumu Arsenal.

Mbali na Chamakh, mchezaji mwingine aliyewahi kuhusishwa na ulevi huo ni Mario Balotelli wa AC Milan ambaye amewahi kupigwa picha akiwa katika klabu za usiku akiburudika na ulevi huo wakati huo akiwa mchezaji wa Manchester City.

Wakati wachezaji wenzake wakionekana na chupa za pombe mikononi mwao, Balotelli yeye alikuwa na chupa ya pombe huku akiburudika na Shisha.

Katika ulevi wa Shisha, watengenezaji hutumia chombo maalumu chenye bomba la kutolea moshi, ambacho huwekwa tumbaku, maji na moto.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa tumbaku huwekwa katika chombo hicho na kuunguzwa kwa moto, kisha moshi wa tumbaku hupita kwenye maji na huingia kwenye bomba, kisha watumiaji huanza kuvuta.

Sehemu maarufu ambako Shisha inauzwa ni Ufukwe wa Coco, maeneo ya Kinondoni, Mwananyamala, Masaki, Mbezi Beach, Sinza maeneo ya Barabara ya Shekilango na maeneo kadhaa ya mitaa ya mjini.

Shisha imekuwa na wapenzi wengi na ndio maana wamiliki wa baa Dar es Salaam wamegundua kwamba ulevi huo unapendwa zaidi na vijana na ndio maana kila anayeanzisha baa mpya amekuwa akiweka na Shisha.

Vijana wengi hususani wanafunzi wa vyuo huchangishana fedha za kunywa viroba lakini lengo lao ni kwenda kuvuta Shisha ambapo hupokezana ulevi huo bila kujali athari za magonjwa ya kuambukiza. Mmoja wa watumiaji Shisha, Ismail Ndunguru anasema yeye na vijana wenzake hutumia siku za mwisho wa wiki kwenda kuburudika kwa uvutaji katika hoteli moja iliyopo Mtaa wa Garden jijini Dar es Salaam.

“Kuvuta Shisha kwa siku ni Sh 10,000, mkimaliza, mnarudisha bomba. Tukiwa wengi inafurahisha kuvuta,” anasema Ndunguru.

Taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaeleza kuwa, mkupuo mmoja wa Shisha, una kemikali hai 4,800 na kwamba kemikali hizo husababisha saratani ya mapafu, maradhi ya moyo na maradhi ya mfumo wa upumuaji.

WHO inaeleza kuwa, kiasi cha uvutaji Shisha kwa saa moja ni sawa na kuvuta sigara 100 au 200.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya ndani ya mwili na mfumo wa hewa, Meshack Shimwela anasema madhara ya Shisha ni kama yale yanayosababishwa na uvutaji wa sigara pengine ni zaidi kutokana na kilevi hicho kuwa na tumbaku nyingi.

Anasema licha ya kuwa watengenezaji na wavutaji Shisha kudai kuwa haina madhara kwa sababu huchanganywa na maji, lakini bado madhara yake ni makubwa.

“Maradhi yote yanayosababishwa na uvutaji wa sigara ndiyo yanayosababishwa na Shisha, mfano saratani ya mapafu na mdomo, kifua kikuu na mzio ambao unaweza kusababisha pumu,” anasema Dk. Shimwela.

Profesa Twalib Ngoma, Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, anasema asilimia 40 ya saratani zote nchini zinasababishwa na matumizi ya tumbaku.

Biashara inavyofanyika

Shisha inauzwa sehemu kadhaa za starehe za Jiji la Dar es Salaam na maeneo yanayouza bidhaa hiyo yanafahamika kama ‘Shisha lounge au Shisha point’.

Mwandishi wa gazeti hili akiambatana na Ndunguru walikwenda hadi Kinondoni katika hoteli moja ambako wavutaji wa Shisha walikuwa wakiendelea kuburudika huku wakipuliza moshi hewani. Walitozwa Sh 15,000 kisha waliletewa chombo cha kuvutia. Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa bei ya Shisha hutegemea sehemu inapouzwa, hivyo huuzwa kati Sh 10,000 na 70,000.

Sinza na Mikocheni bei huwa nafuu kutokana na ushindani wa kibiashara, lakini bei hizo hutegemeana na ladha ya Shisha kwa kuwa zipo aina tofauti ambazo ni vanila, strawberry, mint, chocolate au kahawa ili kuwavutia wavutaji. Ladha hizo zinatajwa kuwa kivutio cha mabinti ambao wameingia kwa kasi kwenye uvutaji huo.

Ndunguru anasema Shisha haina madhara kwake ingawa alipovuta mara ya kwanza, alikohoa sana lakini sasa anaiona ni kiburudisho kinachomfariji.

Uchunguzi ulibaini kwamba wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo vikuu, kwa makundi hujikusanya na kuchanga fedha kwa ajili ya Shisha.

Inadaiwa kwa sasa wapo wafanyabiashara wa Shisha ambao huchanganya dawa za kulevya kama heroin na bangi katika Shisha kama kivutio kwa watumiaji.

“Hii ni biashara kubwa sana kwa wakati huu, kwa siku moja, naingiza zaidi ya Sh 150,000 kwa kuuza bomba la Shisha,” anasema mfanyabiashara mmoja wa Kinondoni.

Muuzaji wa Shisha wa Coco Beach, Said Coco alisema biashara ni nzuri, wateja wamekuwa wakiongezeka kila siku.

Anasema wateja wake wakubwa ni vijana wa umri wa miaka 15 hadi 40 ambao huvuta Shisha kila mwishoni mwa wiki.

Hata hivyo, alikanusha habari kuwa wafanyabiashara wanaweka dawa za kulevya na bangi kwenye Shisha, ingawa anasema kama wapo wanaofanya hivyo basi wanaharibu starehe hiyo ambayo yeye anasema haina madhara.

Serikali inasemaje?

Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid alisema anafahamu kuhusu Shisha na umaarufu wake hususan Dar es Salaam, lakini ni vigumu kuwakamata watumiaji.

“Shisha ni hatari na hatuiungi mkono, lakini hatuwezi kuwakamata watumiaji kama ambavyo hatuwezi kuwakamata walevi wa sigara na pombe. Lakini tunawaasa watengenezaji Shisha kuweka nembo ionyeshayo kuwa ni kilevi hatari,” anasema.

Dk. Rashid anasema matumizi ya tumbaku yanasababisha maradhi mengi hasa saratani ambayo inasababisha kiharusi, maradhi ya moyo na ngozi. Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema hana taarifa za ongezeko la matumizi ya Shisha nchini, ingawa aliwahi kuona kilevi hicho nchini Misri.

Nzowa anasema ikiwa itagundulika kuwa Shisha ina wingi wa Nicotine, atachukua hatua kali dhidi ya wahusika, huku akitoa mfano wa kilevi cha kuber kilichowahi kupigwa marufuku.

Asili ya shisha

Shisha ni jina lenye asili ya Misri (sheesha) lenye maana ya bomba la maji lililounganishwa kwenye kontena.

Tumbaku iliyochanganywa na ladha ya matunda, hujazwa kwenye chombo mfano wa chetezo, moto huwekwa kati na sehemu moja huwekwa maji.

Moshi wenye harufu au ladha hutoka kupitia bomba hilo na kuvutwa. Mvutaji huvuta kwa kutumia bomba (huweza kuwa la plastiki) na mabomba mengine yanaweza kutumiwa na kutupwa (disposable).

Athari zake kiafya

Kuharibu ogani; Shisha inatajwa kuwa na hewa ya carbon monoxide ambayo huingia kwenye mapafu na kuchukua nafasi ya hewa safi ya oksijeni, hivyo ogani muhimu kuharibika.

Saratani; Shisha ina wingi wa nicotine, kiwango cha kemikali za tar, carbon monoxide, metali za kiwango cha juu kama cobalt na lead ambavyo ni visababishi vya saratani.

Utegemezi (adiction); Uvutaji wa Shisha husababisha kutengenezwa kwa kiwango kikubwa cha nicotine kwenye damu, hivyo mtu akishazoea kuvuta hawezi kuacha kwani kilichomo kwenye Shisha huvutwa kwenye neva za fahamu na kusababisha mishipa hiyo kwenye ubongo kuhisi kupata faraja na raha ya kipekee.

Maradhi ya kuambukiza; Uvutaji wa shisha hutumia bomba ambalo watu kadhaa hushirikiana. Hali hii husababisha maradhi ya kuambukiza kama Kifua Kikuu (TB) na hepatitis B (homa ya ini).

Makala hii ilitoka kwa mara ya kwanza kwenye Gazeti la Mwananchi Jumamosi.