Ubabe wa WCB Wasafi katika tuzo!
Muktasari:
- Tofauti na lebo nyingine, mara nyingi wasanii wa WCB Wasafi wamekuwa wakipokelewa vizuri pindi wanapoachia kazi zao, kitu kinachosababisha kufanya vizuri katika tuzo.
REKODI lebo ya WCB Wasafi imeanzishwa na Diamond Platnumz zaidi ya miaka 10 iliyopita na ndani ya muda huo imetengeneza majina makubwa na maarufu katika muziki wa Bongo Fleva.
Tofauti na lebo nyingine, mara nyingi wasanii wa WCB Wasafi wamekuwa wakipokelewa vizuri pindi wanapoachia kazi zao, kitu kinachosababisha kufanya vizuri katika tuzo.
1. Kuna wanamuziki wawili wa WCB Wasafi walioshinda tuzo za African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) zinazofanyika Marekani na kila mmoja alitakata katika kipengele cha Msanii Bora Chipukizi. Harmonize ambaye ni msanii wa kwanza kutambulishwa na lebo hiyo alishinda AFRIMMA mwaka 2016, huku Zuchu ambaye ni msanii wa pili wa kike ndani ya WCB Wasafi akishinda mwaka 2020.
2. Harmonize alishinda tuzo nyingine ya Msanii Bora Chipukizi 2016 kutoka African Entertainment Awards USA (AEAUSA), kabla ya baadaye kuja kuandika rekodi katika tuzo hizo lakini akiwa tayari ameondoka WCB Wasafi.
3. Mwaka 2023, Harmonize aliandika rekodi kama msanii wa kwanza Bongo kushinda tuzo tatu kwa mpigo za AEAUSA, tuzo ambazo zilianza kutolewa Oktoba 2015 huko New Jersey, Marekani zikiwa na vipengele 30. Harmonize alishinda katika vipengele vya Msanii Bora wa Mwaka, Video Bora ya Mwaka (Single Again) pamoja Mfalme wa Afro-Bongo Afrika Mashariki.
4. Tangu mwaka 2015 hadi 2022, Diamond ameshinda tuzo nane za AEAUSA akiwa ndiye mwanamuziki pekee Afrika Mashariki aliyeshinda tuzo hizo mara nyingi zaidi kwa muda wote.
5. Ni vipengele viwili tu alivyoshinda Harmonize katika tuzo za AEAUSA ambavyo Diamond hajawahi kuvishinda, navyo ni Msanii Bora Chipukizi na hicho cha Mfalme wa Afro-Bongo Afrika Mashariki ambacho ni kipya. Ila kama ni Msanii Bora wa Mwaka, Diamond ameshinda mara tatu; 2018, 2020, 2021. Kama ni Video Bora, Diamond kashinda mara mbili; 2016 na 2016 (Nitampata Wapi na Utanipenda).
6. Diamond ndiye msanii wa kwanza kutokea Afrika kushinda tuzo mbili kwa mpigo za MTV Europe Music Awards (EMAs) na alifanya hivyo mwaka 2015.
7. Hadi sasa Diamond ameshinda tuzo za MTV EMAs mara tatu, sawa na Tyla kutokea Afrika Kusini na hawa ndio wanamuziki wa Afrika walioshinda tuzo hizo mara nyingi zaidi kwa muda wote.
Tuzo hizo ambazo kila mwaka hufanyika barani Ulaya, tayari Diamond amechaguliwa kuwania mara tano na kushinda mara hizo tatu akiwa ni mwanamuziki pekee kutokea Afrika Mashariki aliyewania mara nyingi zaidi.
8. Diamond anashikilia rekodi kama msanii akiyeshinda tuzo nyingi za muziki Tanzania (TMA) kwa usiku mmoja na mwaka 2014 alishinda tuzo saba. Vilevile kwa ujumla ndiye mwanamuziki aliyeshinda tuzo mara nyingi kwa muda wote.
Wanaofuatia katika rekodi hiyo ya Diamond ni 20 Percent ambaye mwaka 2011 alishinda tano, sawa na Zuchu mwaka 2022, pia Alikiba ameshinda tano mara mbili ambapo ni mwaka 2015 na 2021.
9. Msanii wa pili kutambulishwa WCB Wasafi, Rayvanny ndiye mwanamuziki wa pili Afrika Mashariki kushinda tuzo ya BET Marekani akifanya hivyo mwaka 2017, akiwa ametanguliwa na Eddy Kenzo wa Uganda aliyeshinda 2015.
10. Rayvanny ambaye ni mwanamuziki wa kwanza Afrika kutumbuiza katika hafla ya tuzo za MTV EMAs, ndiye msanii aliyeshinda tuzo nyingi zaidi za kimataifa akiwa chini ya WCB Wasafi, lebo ambayo imeshasaini wasanii nane.