Twanga Pepeta yamuondoa Hassan Rehani, mwenyewe afunguka
Muktasari:
- Taarifa iliyotolewa na Twanga Pepeta Agosti 18, 2026, imeeleza kuwa, Rehani si mfanyakazi wa kampuni hiyo tangu mwisho wa mwezi Juni 2026 na kwamba hana tena mamlaka ya kuiwakilisha bendi hiyo katika masuala ya booking wala malipo.
UONGOZI wa Bendi ya Twanga Pepeta, umetangaza rasmi kumaliza uhusiano wa kikazi na aliyekuwa meneja wake, Hassan Rehani, huku ukitoa tahadhari kwa waandaaji wa shoo kuhusu oda na malipo yoyote yatakayopita kwake.
Taarifa iliyotolewa na Twanga Pepeta Agosti 18, 2026, imeeleza kuwa, Rehani si mfanyakazi wa kampuni hiyo tangu mwisho wa mwezi Juni 2026.
Akizungumza na Mwanaspoti, mmiliki wa Twanga Pepeta, Asha Baraka, amedai hatua hiyo imefikiwa baada ya uongozi kubaini mara kadhaa mwenendo usio mzuri wa Rehani ndani ya bendi hiyo.
Mwanaspoti limemtafuta Hassan Rehani kuzungumzia ishu hiyo ambapo amesema ameamua kumwachia Mungu na kutafuta utulivu wa mambo hayo kwa njia ya kifamilia.
Rehani amesema alijiweka pembeni na shughuli za Twanga Pepeta tangu Agosti 1, 2026.
Alipanga kuzungumza na Baraka, ambaye ni kaka wa Asha, pamoja na Asha mwenyewe ili kulimalizana kwa amani.
"Mimi sina la kusema. Masuala ya kifamilia huwa tunayamaliza kifamilia, siwezi kufunguka au kumjibu mtu yeyote kwenye vyombo vya habari ila ipo sehemu ambayo nitaweza kuzungumza. Asha Baraka kwangu ni kama mzazi wangu,” amesema Rehani.
Hassan Rehani ameitumikia Twanga Pepeta tangu mwaka 2011 akiwa meneja wa bendi, nafasi ambayo imemfanya kuwa sehemu ya shughuli mbalimbali za kundi hilo kwa zaidi ya muongo mmoja.
Katika kipindi chake ndani ya Twanga Pepeta, Rehani amekuwa akihusika na shughuli za kiuendeshaji na uratibu wa bendi, ikiwamo mawasiliano na waandaaji wa shoo.
Mara ya mwisho Rehani kuonekana akifanya kazi za bendi hiyo ilikuwa katika maandalizi ya uzinduzi wa albamu ya 16 ya Twanga Pepeta ambapo siku ya tukio lenyewe Agosti 7, 2026 hakuonekana huku mwenyewe akithibitisha kwamba alijiweka pembeni Agosti 1, 2026.