TUONGEE KISHKAJI: Kila msanii anajiona bora, nani mbovu?
Muktasari:
- Rayvanny kisa tu hajatajwa kama msanii bora wa kiume aliichafua Instagram yake kwa video na picha za mwaka jana akionyesha shoo za kimataifa alizofanya huku akiuliza swali, msanii gani kati ya wale waliotajwa pale amefanya kufuru ya shoo za kimataifa kama yeye?
MAJINA ya wasanii waliochaguliwa kuwania tuzo za muziki yalipotajwa kila msanii ambaye hakuwa kwenye orodha alikimbilia Instagram na kuanza kushangaa kwamba kwanini hakutajwa. Na siyo kushangaa kwa kuuliza tu, hapana. Bali kwa kujimwambafai kwamba yeye ni bora kuliko waliotajwa. Nyimbo zake ni bora kuliko za waliotajwa na kwa sababu hiyo tuzo zimejaa kupendeleana na uonevu.
Rayvanny kisa tu hajatajwa kama msanii bora wa kiume aliichafua Instagram yake kwa video na picha za mwaka jana akionyesha shoo za kimataifa alizofanya huku akiuliza swali, msanii gani kati ya wale waliotajwa pale amefanya kufuru ya shoo za kimataifa kama yeye?
Rosa Ree alijirekodi video ya zaidi ya dakika mbili akiwashangaa waandaji kwanini hawakuuweka wimbo wake wa Mama Omolo kwenye tuzo, anadai mwaka jana hakuna wimbo uliobamba kuzidi huo.
Ibra wa Konde Gang naye eti alisema hana shida ya kutajwa kwenye tuzo hizo kwani mtaa ulishampa ushindi na tuzo kwa kumfanya kuwa msanii bora.
Siyo hao tu, karibu kila msanii ambaye hakutajwa kwenye tuzo alilalamika kwa namna moja ama nyingine. Binafsi wakati natazama hizo sarakasi nilikuwa nawaelewa wasanii na nilikuwa upande wao. Kuwa upande wao simaanishi kwamba nilikuwa nadhani wako sahihi, hapana. Nilikuwa nawaelewa kwa sababu nimeshawahi kupitia sehemu kama hiyo kwa sababu mimi pia ni msanii. Mimi huandika miswada ya filamu. Mwanzoni kabisa mwa tasnia hii nilikuwa nadhani ni mwandishi bora kuliko yeyote duniani. Nilikuwa natukuza kila skripti nayoandika huku nikimtukuza zaidi mwandishi wa skripti hiyo ambaye ni mimi mwenyewe.
Kama ambavyo Rayvanny anawashangaa waandaji wa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kutomchagua, ndivyo ambavyo nilikuwa nashangaa kwanini waandaaji wa filamu hawaji kwangu kununua au kuchukua skripti kali za kufanya mapinduzi kwenye tasnia, badala yake wanatengeneza muvi zenye skripti za hovyo zisizoeleweka? Mpaka miaka kadhaa mbele nilipokuja kujifunza kwamba, kwanza skripti siyo kweli kwamba zangu zilikuwa bora kuliko za wengine kwa kiasi nilichokuwa nadhani, bali zangu zilikuwa bora kwa sababu tu hazijawahi kutengenezwa kuwa filamu hivyo pengine sijui makosa yake kwa sababu mimi ndiye mwandishi na ndiye ninayezihukumu. Pili nilijifunza kwamba hata waandishi wengine wengi wana mtazamo kama mimi. Kwamba wao ni bora kuliko mtu yeyote yule duniani. Na tatu nilijifunza kuna waandishi mamilioni, lakini kuna nafasi chache hivyo wengine watapata fursa ya kazi zao kutengenezwa kuwa filamu na wengine hawatapata fursa hiyo.
Nadhani Rayvanny na wasanii wengine wote wanatakiwa kukumbuka na kujifunza haya. Wanatakiwa wajue kwanza nafasi kwenye kila kipengele cha tuzo ni tano na Tanzania ina wasanii zaidi ya milioni.
Na kila msanii anadhani yeye ni bora na alistahili kuwa kwenye tuzo hizo sasa kama kila msanii anayetamani kutajwa atatajwa kwenye tuzo hizo zitakuwaje? Kwamba zitakuwa na kipengele cha wasanii milioni na vipi kuhusu mshindi, maana anatakiwa kuwa mmoja au nako pia washinde wasanii wote milioni? Sasa kama ni hivyo kutakuwa kuna haja gani ya kuwa na tuzo kama kila mtu tayari anajijua ni bora, yeye ni mshindi? Tuzo iondolewe tupanguse makalio tukatafute mambo mengine ya kufanya. Wasanii wafanye muziki siyo kwa ajili ya kupata tuzo, bali kwa ajili ya mashabiki. Kisha kama watachaguliwa kwenye tuzo iwe ni kama nyongeza na washukuru. Haya malalamiko ya kila mtu kutaka kuwa kwenye tuzo yatawachosha waandaaji, watajitoa na mwisho wa siku mtarudi kulekule. Waache malalamiko.