Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TRA yabaini taarifa zisizo sahihi kwenye G-Wagon ya Ommy Dimpoz

Muktasari:

  • TRA imesema gari hilo lililoonekana kwenye video iliyosambaa mitandaoni, likionyesha maofisa wa mamlaka hiyo wakilikagua. Huku kukiwa na mabishano katika eneo la tukio, lilikuwa sehemu ya operesheni inayoendelea ya ukaguzi wa magari kwa lengo la kubaini uwepo wa ukwepaji kodi.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema imebaini tofauti katika taarifa za forodha za gari aina ya Mercedes-Benz G-Wagon linalohusishwa na msanii wa Bongo Fleva na mfanyabiashara, Omary Nyembo maarufu Ommy Dimpoz, baada ya uchunguzi wa kitaalamu kubaini kuwa gari hilo ni la thamani kubwa zaidi kuliko lilivyoelezwa wakati wa uingizaji nchini.

TRA imesema gari hilo lililoonekana kwenye video iliyosambaa mitandaoni, likionyesha maofisa wa mamlaka hiyo wakilikagua. Huku kukiwa na mabishano katika eneo la tukio, lilikuwa sehemu ya operesheni inayoendelea ya ukaguzi wa magari kwa lengo la kubaini uwepo wa ukwepaji kodi.

Kwa mujibu wa taarifa ya TRA, operesheni hiyo ilianza Septemba 26, 2026, na katika ukaguzi huo maofisa walilikuta gari hilo likiwa limeegeshwa katika Palm Beach Casino jijini Dar es Salaam bila namba za usajili.

Baada ya hapo, TRA ilianza mchakato wa kubaini utambulisho wa gari hilo na historia yake katika mfumo wa forodha.

Mamlaka hiyo imesema uchunguzi wa kitaalamu uliwezesha kubaini namba maalumu ya utambulisho wa gari (VIN) kuwa WDB4632762X322756. Ambayo baadaye ilihakikiwa katika Mfumo wa Forodha wa Tanzania (TANCIS).

TRA ilisema kumbukumbu zilizowasilishwa wakati wa mchakato wa kulipia na kukamilisha taratibu za forodha zililitaja gari hilo kuwa Mercedes-Benz G-Class G350, lililotengenezwa mwaka 2020.

Hata hivyo, uchunguzi wa kitaalamu uliofanywa baadaye ulibaini kuwa gari hilo ni Mercedes-AMG G63, lililotengenezwa mwaka 2018.

Kwa mujibu wa TRA, aina hiyo ya G63 ina thamani kubwa zaidi kuliko G350 iliyotajwa katika nyaraka za forodha, hali ambayo imeibua tofauti katika thamani iliyotumika kukokotoa kodi iliyopaswa kulipwa.

“Tofauti katika taarifa hizo inaonyesha kuwepo kwa taarifa zisizo sahihi ambazo zilisababisha gari hilo kukadiriwa kwa thamani ndogo ya forodha na hivyo kupunguza kiasi halisi cha kodi kilichopaswa kulipwa,” ilisema taarifa ya TRA.

Kutokana na hali hiyo, TRA imesema uchunguzi unaendelea kubaini mazingira ya uingizaji wa gari hilo nchini pamoja na kiasi cha kodi kilicholipwa.

Mamlaka hiyo imesema gari hilo ambalo limesajiliwa kwa jina la Omary Faraji Nyembo, limekamatwa na TRA wakati uchunguzi ukiendelea.

“Uchunguzi kuhusu tukio hili na gari lililokamatwa na TRA bado unaendelea. Na hatua zaidi za kiutawala, kikodi au kisheria zitachukuliwa kulingana na matokeo ya uchunguzi na sheria husika,” ilisema taarifa hiyo.

TRA pia imesema inatambua na kuheshimu ushirikiano uliotolewa na mmiliki wa gari hilo wakati wa mchakato wa ukaguzi.


TRA YAELEZA MAMLAKA YA MAOFISA

Katika taarifa hiyo, TRA pia imeeleza msingi wa kisheria unaowapa maofisa wake mamlaka ya kufanya ukaguzi huo. Baada ya kuwepo kwa mjadala mitandaoni kuhusu namna maofisa walivyotekeleza operesheni hiyo.

Kwa mujibu wa TRA, Kifungu cha 157(1) cha East African Community Customs Management Act pamoja na Kifungu cha 139(1) cha Customs (Management and Tariff) Act, Sura ya 403, vinawapa maofisa mamlaka ya kuingia na kukagua maeneo pale wanapokuwa na sababu za kuamini kuwa kuna bidhaa ambazo ziliingizwa nchini bila kufuata taratibu za forodha.

Mamlaka hiyo imesema maofisa wanaweza pia kuongozana na maofisa wengine au kuomba msaada wa polisi pale inapohitajika, kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, TRA imesisitiza kuwa mamlaka hayo hayaondoi haki za walipa kodi.

Imesema mmiliki ambaye mali yake imekamatwa anastahili kupewa taarifa kwa maandishi pamoja na sababu za kukamatwa kwa mali hiyo kwa mujibu wa Kifungu cha 162(1) cha sheria hiyo.

Aidha, TRA imewakumbusha walipa kodi wajibu wa kutoa taarifa sahihi, kamili na za kweli, kuwasilisha nyaraka halali, kujibu maswali yanayohusu mali inayochunguzwa na kushirikiana na maofisa wakati wanapotekeleza majukumu yao.

Mamlaka hiyo pia imeonya dhidi ya kuingilia utekelezaji wa majukumu ya kikodi, ikisema Kifungu cha 96(1) cha Tax Administration Act, Sura ya 438, kinatambua kuzuia utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa kodi kuwa kosa la jinai.

TRA imesema vitendo vinavyoweza kuchukuliwa kuwa kuzuia utekelezaji wa majukumu hayo ni pamoja na kumpiga au kujaribu kumpiga ofisa, kumzuia au kujaribu kumzuia kutekeleza majukumu yake, pamoja na kuingilia vifaa vinavyotumiwa na ofisa katika utekelezaji wa kazi.


OMMY AJIBU

Wakati TRA ikiendelea na uchunguzi, Ommy Dimpoz amekanusha kuhusishwa na kitendo chochote cha kuzuia maofisa wa TRA kutekeleza majukumu yao.

Katika taarifa aliyoiweka kwenye mitandao ya kijamii, msanii huyo amesema amekuwa akifuata sheria na kushirikiana na mamlaka za Serikali pale anapohitajika.

“Ninajivunia kuwa nimekuwa raia ninayeheshimu sheria katika maisha yangu yote. Sijawahi kuwa, siwezi kuwa na sitarajii kuwa mtu anayevunja sheria za nchi kwa makusudi,” alisema.

Ommy amesema pia hakuwahi kuwa miongoni mwa watu waliowasumbua au kuwazuia maofisa wa TRA katika tukio lililotokea alfajiri ya Septemba 26, 2026.

Amesema wakati mmoja wa watu waliokuwa naye alipokataa kuwapa nafasi maofisa hao, yeye ndiye aliyeingilia kati na kumtaka mtu huyo awaruhusu maofisa kuendelea na kazi yao.

“Hata walipokutana na upinzani kutoka kwa mmoja wa watu niliokuwa nao, mimi ndiye niliyeingilia kati na kumwomba awape nafasi wafanye kazi yao,” alisema.

Pamoja na msimamo huo, Ommy ameomba radhi kwa mtu yeyote aliyekerwa na tukio hilo au aliyelitafsiri tofauti na alivyokusudia.

“Naomba radhi ikiwa kuna tafsiri yoyote isiyofaa iliyojitokeza kunihusu kutokana na tukio hilo, na ninaahidi nitajaribu kuepuka kuwa katika mazingira kama hayo tena,” alisema.

Pia amewataka wananchi kushirikiana na maofisa wa Serikali pale wanapohitaji msaada au wanapotekeleza majukumu yao.

TRA imeendelea kuwataka wamiliki, waagizaji na wafanyabiashara wa magari kuhakikisha taarifa zinazowasilishwa wakati wa uingizaji wa magari nchini. Ikiwamo aina ya gari, mwaka lililotengenezwa, thamani, namba ya VIN au chassis na taratibu za uingizaji, ni sahihi na zinaungwa mkono na nyaraka halali.

Mamlaka hiyo pia imewashauri wanaonunua magari yaliyotumika kuhakiki taarifa za magari hayo kupitia mifumo au ofisi za TRA kabla ya kukamilisha manunuzi, ili kujiridhisha kama kodi stahiki zililipwa wakati gari lilipoingia nchini na kama kuna changamoto nyingine za kikodi.