Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tolami: Mchumba wa Saka anayependa pamba kali!

Muktasari:

  • Mwanamitindo huyo na mshawishi wa mitandao ya kijamii alianza uhusiano na Saka mwaka 2020, kabla ya kuonekana pamoja kwa mara ya kwanza katika michuano ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.

Mchezaji wa Arsenal, Bukayo Saka amemchumbia mwanamitindo wa Uingereza, Tolami Benson ambaye kwa muda sasa ameendelea kuwavutia mashabiki kupitia mitindo yake ya mavazi anayoivaa pindi anapokwenda viwanjani kutazama mechi ikiwa ni sehemu ya kumuunga mkono mchumba wake huyo.

Mwanamitindo huyo na mshawishi wa mitandao ya kijamii alianza uhusiano na Saka mwaka 2020, kabla ya kuonekana pamoja kwa mara ya kwanza katika michuano ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.

Tangu wakati huo, Tolami amekuwa akionekana mara kwa mara uwanjani akimshangilia Saka huku akiwa amevalia mtindo wa mavazi unaouita Sports Chic.

“Nilipoingia katika ulimwengu wa soka, nilikuwa navalia jezi za timu pamoja na jeans au kaptula, lakini mavazi hayo hayakunikaa vizuri, hivyo niliacha kujaribu kuendana na mitindo ya wengine na kuanza kuvaa vitu vinavyonifaa,” alisema Tolami wakati akiongea na Jarida la British Vogue hapo Mei 2026.

“Kwa sasa mtindo wangu wa mavazi umejikita kuchanganya mavazi ya gharama kubwa na yale ya kawaida. Kwa mfano, ninaweza kuvaa viatu vyangu vya Louis Vuitton pamoja na jezi ya Arsenal na kaptula za Zara. Mtindo huo ndio ninaouita Sports Chic,” aliongeza.

Mbali na Jarida la British Vogue, mitindo ya mavazi ya Tolami anapokwenda kutazama mechi imekuwa ikivutia pia majarida mengine ya mitindo likiwemo Who What Wear. Vilevile amekuwa akipigwa picha katika matukio makubwa ya kimataifa ya mitindo kama London Fashion Week.

Baada ya kuonekana katika michuano ya Euro 2024, Tolami alipata fursa ya kuwa balozi wa bidhaa za kampuni ya L’Oréal Paris, pamoja na kuzindua toleo jipya la mkusanyiko wa mavazi yao kwa kushirikiana na kampuni ya River Island.

“Ninapenda kutafuta njia tofauti za kuvaa mavazi ya kawaida na kuchanganya mitindo mbalimbali ili kupata muonekano mpya kwa kutumia nguo ambazo tayari zipo kwenye kabati langu. Jambo hilo linalifanya kabati lako la nguo lionekane kuwa na mavazi mengi zaidi na kufanya uvaaji kuwa wa kufurahisha zaidi,” alisema.

Kwa mujibu wa gazeti la The Sunday Times, Tolami alikulia katika familia kubwa huko Hertfordshire, Uingereza. Akizungumza na gazeti hilo mnamo Julai 2026, alijitambulisha kama msichana aliyezaliwa na kukulia katika mazingira ya vijijini nchini humo.

Alisoma katika shule ya Bishop’s Hatfield Girls’ School kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Birmingham City, ambako alihitimu shahada ya kwanza katika fani ya Uhusiano wa Umma na Habari.

Kwa mujibu wa taarifa zake zilizopo kwenye ukurasa wake wa LinkedIn, baada ya kuhitimu masomo yake, Tolami alianza kufanya kazi katika kampuni mbalimbali za mawasiliano ya umma (PR) na mashirika ya matangazo.

Ingawa yeye na Saka walianza uhusiano wa kimapenzi mwaka 2020, wawili hao waliamua kufanya uhusiano huo kuwa wa siri, kwa kipindi chote hakuna aliyewahi kumposti mwenzake katika mitandao ya kijamii au kutoa taarifa zinazohusiana na uhusiano wao.

“Ni vizuri kuwa na baadhi ya mambo ambayo unayahifadhi kwa ajili yako mwenyewe,” Tolami aliliambia Gazeti la The Sunday kuhusu uamuzi wao huo.

Mwaka 2022, Tolami alionekana akimshangilia Saka wakati wa michuano ya Kombe la Dunia nchini Qatar. Baadaye, wawili hao walipigwa picha pamoja wakiwa kwenye viti vya mashabiki ikiwa ni baada ya timu ya taifa ya England kuifunga Wales katika hatua ya makundi.

“Kwangu mimi, Saka anabaki kuwa mpenzi wangu tu maana ninamfahamu kwa upande tofauti kabisa na ule ambao watu wengine wanamfahamu. Nimezoea kuona watu wakimfuata na kumsogelea, lakini zaidi ya hilo, tunaishi maisha ya faragha ambayo hawayajui," alisema Tolami.

Akizungumza na The Sunday Times, Tolami alisema ingawa hajui mambo mengi kuhusu soka, lakini hilo halijamzuia kuendelea kumshangilia mchumba wake, Saka, akiwa jukwaani kila anapokuwa akicheza uwanjani.

“Watu wanaponiuliza kuhusu soka, huwa ninawaambia kwamba ninajua yale mambo ya msingi tu. Ninachokijua ni kwamba mwanaume wangu anacheza vizuri uwanjani kila wakati.

“Jambo hili halinihusu mimi, bali linamhusu yeye. Ninapofika uwanjani, kumuona na kisha tunapopeana ishara ya kusalimiana kwa mikono, huwa ni jambo zuri. Unaweza kuona furaha kwenye uso wake. Kufika uwanjani kumuunga mkono na  kumshuhudia akicheza ni jambo la muhimu sana,” alisema Tolami.

Saka na Tolami walitangaza rasmi uchumba wao kupitia mtandao wa Instagram hapo Novemba 2025, ambapo waliposti mfululizo wa picha zao na kisha kuandika tarehe ya tukio hilo - 17.11.25. Katika picha hizo, wawili hao walionyesha pete kubwa ya almasi aliyovishwa Tolami kama ishara ya uchumba wao.

Akizungumzia maandalizi ya harusi yao, Tolami alisema anapenda harusi iwe tukio la kuwafurahisha wao na si kujikita kuwafurahisha watu katika mitandao ya kijamii.

"Hivyo mimi si mtu wa kusema, ‘Mungu wangu, lazima niwe na harusi ambayo kila mtu atataka kupiga picha na kuiposti Instagram.’ Kama ningekuwa na uwezo wa kufanya harusi ya siri, ningefanya hivyo lakini mama yangu atapatwa na mshtuko... Ndoa ni jambo takatifu,” alisema Tolami Benson.