Mkali wanu na ishu ya kulelewa
MCHEKESHAJI Mkali Wao, amezungumzia suala la wanaume kulelewa na wanawake, akieleza namna ambavyo baadhi ya wanaume hupata fedha kutoka kwa wanawake huku jukumu lao likiwa ni kuwapa raha kupitia mahusiano ya kimapenzi.
Katika maelezo yake, Mkali Wao amejitofautisha na wanaume wanaofanya hivyo, akisisitiza kuwa yeye si miongoni mwa wanaolelewa.
Akizungumzia na Mwanaspoti, Mkali wao amesema, mwanaume anaweza kupewa fedha na mwanamke, huku upande wake ukitoa huduma ya kimapenzi.
“Kulelewa hapana. Unapata eti mwanamke anakupa hela, wewe kazi yako kujihusisha na mapenzi tu, unapata raha na hela,” amesema Mkali Wao.
Aidha Mkali Wao ameshangazwa na namna watu wanavyomuhusisha yeye na suala hilo, akisisitiza kuwa si kweli kwamba analelewa na mwanamke.
"Unakuta mtu ananiambia au anasema Mkali Wao analelewa na mwanamke, kitu ambacho hakipo kabisa kwangu na sijawahi, nawashangaza sana hizi habari watu huzitoa wapi," amesema.
Mbali na hilo, Mkali Wao amezungumzia pia kuonekana kwake kwenye mchezo wa ngumi, akionya kuwa watu wasimchukulie kama mtu wa kufanyiwa majaribio kwa sababu anaweza kupata majeraha.
“Kwanza kabisa kwenye huu mchezo wa ngumi watu wasinichukulie poa kwa kunifanya majaribio, mimi naweza nikavunjika mifupa na huku watu wakiendelea na maisha yao, hivyo sihitaji kabisa,” amesema.