Viatu saba vya kiume visivyopoteza mvuto
Muktasari:
- Hawa wanajua kuchagua viatu ambavyo havipotezi nafasi yake kwenye ulimwengu wa mitindo, iwe ni kwenye matembezi, kazini au kwenye hafla zinazohitaji mwonekano wa kuvutia. Hivi hapa ni viatu saba ambavyo mwanaume akivimiliki hawezi kujutia kuvihifadhi kwenye kabati lake.
KUNA viatu ukiviona miguuni mwa mwanaume leo, kesho, mwakani na hata miaka mitano ijayo bado vitakuwa na mvuto uleule. Wakati baadhi ya wanaume wanahangaika kukimbizana na kila mtindo mpya unaoingia sokoni, wengine wana siri ya kuonekana nadhifu bila kutumia fedha kila mara kununua viatu vipya.
Hawa wanajua kuchagua viatu ambavyo havipotezi nafasi yake kwenye ulimwengu wa mitindo, iwe ni kwenye matembezi, kazini au kwenye hafla zinazohitaji mwonekano wa kuvutia. Hivi hapa ni viatu saba ambavyo mwanaume akivimiliki hawezi kujutia kuvihifadhi kwenye kabati lake.
1. RABA NYEUPE
Hivi ni miongoni mwa viatu ambavyo vimeendelea kuwa na nafasi kubwa kwenye mitindo ya wanaume. Uzuri wake ni kwamba vinaweza kuvaliwa na aina mbalimbali za mavazi, kuanzia suruali za jeans, kaptula hadi suruali za kitambaa. Rangi yake nyeupe pia inarahisisha kuvichanganya na mavazi yenye rangi tofauti. Vinafaa kwa matembezi, kukutana na marafiki na hata shughuli zisizohitaji mavazi rasmi. Mwanaume anaweza kuvivaa na shati, fulana au sweta na bado akaonekana nadhifu. Siri kubwa ni kuhakikisha vinakuwa safi kwa sababu uchafu unaweza kuharibu mwonekano wake.
2. VIATU VYA NGOZI VYA KAMBA
Hivi vinafaa zaidi kwa wanaume wanaopenda kuvaa mavazi maalum. Vina muonekano wa heshima na vinaweza kuvaliwa kwenye mikutano, ofisini, sherehe na shughuli nyingine zinazohitaji mavazi maalumu kama suti. Rangi nyeusi na kahawia ni chaguo zuri kwa sababu ni rahisi kuendana na mavazi mengi.
Pia, viatu hivi vinaweza kuvaliwa na suruali za kitambaa, kadeti pamoja na shati la mikono mirefu kwa mwanaume ambaye hataki kuvaa suti nzima. Ni aina ya viatu vinavyoweza kukusaidia kuonekana nadhifu bila kulazimika kutumia mapambo mengi kwenye mavazi yako.
3. VIATU VYA WAZI
Hivi ni maarufu kwa urahisi wake wa kuvaa na kuvua. Vinaweza kuvaliwa na suruali za kitambaa, jeans na mavazi mengine yasiyo rasmi sana. Mwanaume anayevipenda anaweza kuvivaa kwenye matembezi, chakula cha jioni na shughuli za kawaida hasa wikiendi.
Uzuri wake ni kwamba havihitaji maandalizi mengi kabla ya kuvaliwa. Vikiwa na muundo mzuri na rangi inayovutia vinaweza kuongeza mvuto wa mavazi ya kawaida. Hata hivyo, ni muhimu kuchagua vinavyokaa vizuri mguuni na kuendana na mazingira unayokwenda.
4. BUTI FUPI
Hivi ni viatu vinavyofunika kifundo cha mguu na kuwa na sehemu za mpira pembeni badala ya kamba. Vinaweza kuvaliwa na jeans au kaptula, huwa vinachagua sana sio kila suruali utaweza kuvalia.
Buti hizi zinafaa kwa mwanaume anayependa kuonekana tofauti bila kuachana na mtindo wa kawaida. Zinaweza kuvaliwa na shati, koti au sweta na kutoa mwonekano wenye mvuto. Pia ni chaguo zuri kwa wanaopenda mavazi yanayochanganya mtindo wa kawaida na ule rasmi.
5. VIATU VYA KUFUNGA KAMBA
Hivi vina mfumo wa kamba unaoonekana wazi na ni vizuri kwa wanaume wanaopenda kuvaa mavazi maalumu lakini hawataki kuwa na viatu vinavyofanana kila wakati. Vinaendana na suti, suruali za kitambaa na mashati ya mikono mirefu.
Tofauti yake na viatu vingine ipo kwenye namna vinavyofungwa, jambo linalovipa mwonekano wa kipekee. Mwanaume anaweza kuchagua rangi nyeusi kwa nguo ambazo sio nyeus. Lakini ni viatu vinavyofaa kuwa navyo kwa sababu vinaweza kutumika kwenye shughuli nyingi tofauti.
6. VIATU VYA MICHEZO
Kuna viatu vya michezo ambavyo vilianza kupendwa miaka mingi iliyopita lakini bado vina nafasi kwenye mitindo ya sasa. Mara nyingi huwa na muundo wenye soli nyembamba na mchanganyiko wa rangi chache. Vinafaa kwa jeans, kaptula na suruali za kawaida, wengine huenda mbali zaidi na kuvivalia na suti siku hizi.
Kinachovifanya viatu hivi viendelee kupendwa ni urahisi wa kuvivaa na uwezo wake wa kuendana na mavazi tofauti. Pia vinafaa kwa wanaume wanaotaka kuwa na mwonekano wa kisasa bila kuvaa viatu vizito. Ni muhimu kuchagua vinavyokuwa na muundo rahisi ili visipoteze mvuto haraka.
7. VIATU VYA NGOZI VYENYE MIKANDA
Hivi ni viatu rasmi vinavyofungwa kwa kutumia mikanda badala ya kamba. Vinatoa mwonekano wa tofauti na vinaweza kuvaliwa na suti au suruali za kitambaa. Mwanaume anayependa kuonekana nadhifu na mwenye mtindo wa kipekee anaweza kuvifanya sehemu ya mavazi yake ya hafla.
Vinafaa zaidi kwa wanaume wanaotaka kutoka kwenye mazoea ya kuvaa viatu vya kawaida vya kamba. Muundo wake unavifanya vionekane vya kipekee, lakini bado vinaendana na mavazi rasmi. Rangi nyeusi na kahawia zinaweza kuwa chaguo zuri kwa matumizi ya muda mrefu.