SIKIA HII! Miaka miwili ya ulokole wa Ruby
Muktasari:
- Wapo ambao hudumu katika wokovu huo na wapo wengine ambao shetani huwavuta shati na kujikuta wakirudi kwenye himaya yake. Matukio yote hayo yanasogeza siku za maisha mbele!
SUALA la wasanii na watu maarufu kutangaza kuacha maovu na kumrudia muumba wao si geni. Kwa hapa Bongo wapo wengi ambao wamewahi kufanya hivyo, huku wasanii wengi wakiamua kuokoka.
Wapo ambao hudumu katika wokovu huo na wapo wengine ambao shetani huwavuta shati na kujikuta wakirudi kwenye himaya yake. Matukio yote hayo yanasogeza siku za maisha mbele!
Mwanaspoti linamuangazia msanii wa muziki wa bongofleva, Ruby, ambaye alitangaza kuokoka mwaka 2024 na kwasasa ametimiza miaka miwili katika wokovu.
Tukio hili lilipokewa na watu wengi sana, lakini kitendawili kikabaki kwa mashabiki wake wa muziki wa bongofleva kama ataendelea na muziki huo ama ataachana nao na kubaki sehemu moja ya wokovu na kupata ladha za nyimbo za injili.
Kitendawili hicho kimeteguliwa hivi karibuni, baada ya Ruby kupiga stori na Mwanaspoti na kufunguka haya:
Kuhusu kuacha muziki
Wimbo wa mwisho wa bongofleva kuimbwa na Ruby ilikuwa ni mwaka juzi Aprili 2024, uitwao ‘Leo’ ambao alimshirikisha mzazi mwenzake Kusah.
Tangu hapo Ruby akawa kimya, na kuonekana zaidi kwenye makanisa katika mahubiri tofauti na hapa anafafanua:
“Siwezi kusema kama nimeacha muziki wa bongofleva, ila naweza kusema kwasasa nasukumwa na imani ya wokovu, na namshukuru Mungu huu wokovu wangu umeniponya vitu vingi sana, ambavyo siwezi kusimulia kila kitu hadharani.
“Nilikuwa naishi maisha ya ajabu sana jamani, nashukuru tangu niokoke hivi sasa sina matatizo kabisa,” alisema Ruby.
“Unajua mwanzo nilikuwa kama namtania Mungu, nilisema nimeokoka, lakini kimyakimya nilikuwa naendeleza mambo ya kidunia, lakini sasa nasema basi, yaani huwezi kunikuta nafanya vitu ambavyo haviwezi kunivua wokovu wangu.”
Kitu ambacho amejifunza kabla ya kuokoka
“Nimejifunza mengi, licha ya kupitia vikwazo vingi pia. Uvumilivu na utiifu ni vitu ambavyo vimenifanya nifikie kuitwa Ruby mwenye mashabiki wengi,
Una mpango gani na kuimba nyimbo za Injili?
“Mimi nimeshaanza kuimba nyimbo za Injili tangu nilivyobadilisha maisha yangu kuwa mwokovu, nikienda kanisani huwa, nahudumu kwa baraka kubwa sana kwa kuimba nyimbo za kusifu na kuabudu zenye ujumbe mzito wa imani.
“Na pia nimeshaanza kuingia studio kwa ajili ya kurekodi nyimbo za injili, ambazo zikikamilika tu nitaziachia kwa mashabiki zangu na nina imani watazipenda.”
anavyowagusa watu akiimba Kanisani
“Ninapokuwa naimba nyimbo za Injili, kuna tofauti kubwa sana, na ninapokuwa naimba nyimbo za bongofleva, maana huduma yangu huwa inageuka kuwa muda wa kutafakari upendo na uaminifu wa Yesu kama rafiki wa kweli katika nyakati zote za maisha.
“Na waumini walionyesha furaha na shukrani, tukimsifu Mungu kwa pamoja, huku wengi wakieleza kuguswa mioyoni mwao”.
Ruby alizaa mtoto mmoja na Kusah, ambaye baadaye alitua kwa Aunty Ezekiel.