Si kila mtoto wa staa anataka kuwa staa
Muktasari:
- Mzazi akiwa na jina kubwa, kila anachofanya kinafuatiliwa, kupigwa picha na kuzungumziwa Lakini nyuma ya pazia kuna watoto wanaokua wakibeba jina la mzazi huyo huku wakati mwingine wakikosa nafasi ya kuishi maisha yao binafsi.
UMAARUFU una upande wake unaong'aa, lakini kwa watoto wa mastaa wakati mwingine unaweza kuwa maisha ambayo hawakuyachagua wenyewe.
Mzazi akiwa na jina kubwa, kila anachofanya kinafuatiliwa, kupigwa picha na kuzungumziwa Lakini nyuma ya pazia kuna watoto wanaokua wakibeba jina la mzazi huyo huku wakati mwingine wakikosa nafasi ya kuishi maisha yao binafsi.
Hilo limeibuka upya kupitia kauli ya Rahma, mtoto wa pili wa staa wa muziki Zuwena Yusuph “Shilole”, amesema hapendi maisha ya umaarufu na wakati mwingine ustaa wa mama yake umekuwa ukimpa shida.
RAHMA: SIPENDI UMAARUFU
Rahma ameweka wazi kuwa hapendi maisha ya umaarufu, akisema wakati mwingine umaarufu wa mama yake umekuwa changamoto kwake.
“Maisha ya umaarufu ya mama yangu ni magumu wakati mwingine. Kitu kidogo kinaweza kuwa kikubwa, mimi napenda kuwa na mipaka katika maisha yangu na sipendi kunyooshewa vidole na hadhira. Sitamani maisha ya aina hiyo,” amesema Rahma.
Kwa Rahma, inaonekana suala kubwa ni kupata nafasi ya kuishi maisha yake binafsi kwa utulivu, bila kila hatua yake kuangaliwa kupitia umaarufu wa mama yake.
UMAARUFU WA MAMA, KWA WATOTO PRESHA
Hali kama hiyo imewahi pia kuonekana kwa Naya, mtoto wa mwanamuziki maarufu wa Bongofleva, Nandy, ambaye mama yake amewahi kueleza kuwa binti yake hapendi umaarufu kutokana na hasa akiwa shuleni.
“Naya hapendi umaarufu, hasa watoto wenzake wanapomshangaa shuleni wakati mwingine huuliza, kwa nini wananishangaa? inaonyesha wazi kuwa hapendi maisha ya umaarufu," Nandy aliwahi kueleza.
Kwa Naya, shule inapaswa kuwa sehemu ya kusoma, kucheza na kukua kama watoto wengine, lakini umaarufu wa mama yake wakati mwingine humfanya aangaliwe tofauti.
KAJALA: NINGEMUWEKA PAULA ‘LOW KEY
Hata mwigizaji mkongwe Kajala Masanja amewahi kuzungumzia namna alivyojutia binti yake, Paula, kumfanya maarufu kupitia mitandao ya kijamii tangu akiwa mdogo.
“Wakati mwingine najutia kumweka Paula kwenye mitandao tangu akiwa mdogo natamani ningemuweka ‘low key’ nje ya mitandao”. Kajala aliwahi kusema Kajala.
Kauli hiyo inaonyesha kuwa hata mzazi mwenyewe anaweza kubadilisha mtazamo kadri mtoto anavyokua kwani Picha na taarifa za mtoto zinapowekwa hadharani, zinaweza kubaki mtandaoni kwa muda mrefu, wakati mtoto mwenyewe hana nafasi ya kuamua kuhusu hilo akiwa bado mdogo.
UMAARUFU UNA FAIDA PIA
Pamoja na changamoto hizo, kuwa mtoto wa staa si hasara kila upande kwani umaarufu wa mzazi unaweza kufungua milango mbalimbali kwa mtoto.
Anaweza kupata nafasi ya kukutana na watu wengi, kupata nafasi ya ubalozi wa bidhaa, kujifunza mambo mapya na kupata fursa ambazo huenda asingezipata kwa urahisi.
Kwa mtoto anayependa sanaa, biashara au shughuli nyingine za kijamii, mazingira hayo yanaweza kuwa mwanzo mzuri wa safari yake.
Pia, mtoto anaweza kukua akiwa na uelewa wa namna ya kujiamini, kuwasiliana na watu na kukabiliana na mazingira yenye watu wengi.
SIO KILA MTOTO ANATAKA KUWA STAA
Watoto kama Rahma na Naya wanaonyesha kwamba siyo kila anayezaliwa kwenye familia yenye jina kubwa anataka kuishi maisha hayo hayo.
Wengine wanataka maisha ya kawaida, kwenda shule bila kunyooshewa vidole na hadhira na kujenga utambulisho wao wenyewe bila kutambulishwa kwanza kwa majina ya wazazi wao.
Na kwa wazazi mastaa, huenda changamoto ikawa kujua wakati gani wawashirikishe watoto wao na umma na wakati gani wawape nafasi ya kuwa watoto tu. Kwa sababu mwisho wa siku umaaarufu ni wa mzazi, lakini maisha ya mtoto ni yake mwenyewe.