Albamu 10 Bongo Fleva zenye nyimbo nyingi
Muktasari:
- Hata hivyo, Ibraah kutokea Oyaa Gang Entertainment, si mwanamuziki wa kwanza kutoka albamu yenye idadi kubwa ya nyimbo, wapo wengi ingawa idadi inatofautiana.
MWANAMUZIKI wa Bongo Fleva, Ibraah a.k.a Chinga ameendelea kugonga vichwa vya habari baada ya kuachia albamu yake mpya, 1B (2026) ikiwa na nyimbo 50, idadi ambayo imewashangaza mashabiki.
Hata hivyo, Ibraah kutokea Oyaa Gang Entertainment, si mwanamuziki wa kwanza kutoka albamu yenye idadi kubwa ya nyimbo, wapo wengi ingawa idadi inatofautiana.
Hii ni orodha ya albamu za Bongofleva ambazo zimetoka zikiwa na idadi kubwa ya nyimbo, na zote zimeachiwa katika mfumo wa kidijitali (digital streaming) ambao unaruhusu hilo.
1. 1B (2026) - Ibraah: Nyimbo 50
Kwa Ibraah, albamu hiyo ni mradi wa pili chini ya lebo yake ya Oyaa Gang, na wa pili pia tangu ameachana na Konde Music Worldwide, lebo yake Harmonize ambayo ilimtoa kimuziki miaka sita iliyopita.
Albamu ya 1B ina nyimbo 50 ikiwa ni mara ya kwanza mwanamuziki wa Bongofleva kuachia albamu yenye idadi hiyo ya nyimbo. Albamu hii imekuja baada ya kufanya vizuri na EP yake, Poison Medicine (PM) (2026).
2. The Gift of Life (2021) - Best Naso: Nyimbo 32
Albamu ya tatu kutoka kwa Best Naso, The Gift of Life (2021) ina jumla ya nyimbo 32, na kwa mwaka huo ndio ilikuwa albamu namba moja ya Bongofleva iliyoachiwa ikiwa na idadi kubwa ya nyimbo.
Best Naso ambaye nyimbo zake zina sifa ya kuzungumzia maisha ya kawaida katika jamii, hapo awali alifanya vizuri kupitia albamu zake mbili ambazo ni Mamu wa Dar (2009), na Narudi Kijijini (2013).
3. Yule Boy (2019) - Country Wizzy: Nyimbo 31
Rapa Country Wizzy, zamani Country Boy, albamu yake ya kwanza, Yule Boy (2019) ilitoka ikiwa na nyimbo 31, na tangu wakati huo hajaachia albamu nyingine zaidi ya EP, The Father (2020) chini ya Konde Music.
Kutokana na idadi hiyo ya nyimbo na ushawishi wa rapa huyo, albamu hiyo ilifanya vizuri ikiandika rekodi kama albamu ya kwanza ya Hip Hop Bongo kusikilizwa (streams) zaidi ya mara milioni 1 Audiomack.
4. Silver (2025) - Lady Jaydee: Nyimbo 25
Ikiwa ni albamu ya 10 ya Lady Jaydee, Silver (2025) iliachiwa ikiwa na nyimbo 25 huku lengo la albamu hiyo likiwa ni kuhudhuria miaka 25 ya msanii huyo ndani ya Bongofleva akitambulika kama Malkia wa muziki huo.
Pia albamu yake ya nane, 20 (2021) nayo ilikuwa na idadi kubwa ya nyimbo, 20, na ilitoka kwa ajili ya kuhadhimisha miaka yake 20 katika muziki, ambapo alitoka kupitia wimbo wake, Machozi (2000).
5. Sound From Africa (2021) - Rayvanny: Nyimbo 23
Akiwa chini ya WCB Wasafi ndipo Rayvanny aliachia albamu yake ya kwanza, Sound From Africa (2021) ikiwa na nyimbo 23, huku ikisikilizwa (streams) mtandaoni zaidi ya mara milioni 100 ndani ya wiki moja!.
Na albamu yake ya pili chini ya lebo yake ya Next Level Music (NLM), The Big One (2024), ilitoka na nyimbo 18, ambazo urefu wake wa usikilizwaji unachukua muda wa saa moja na dakika tisa.
6. Slave Becomes A King (2020) - Darassa: Nyimbo 21
Rapa huyu kutokea Classic Music Group (CMG), aliachia albamu yake ya kwanza, Slave Becomes A King (2020) ikiwa na nyimbo 21, ambapo mmoja kati ya hizo ulishinda tuzo za Tanzania (TMA) 2021.
Albamu yake ya pili, Take Away The Pain (2025), nayo haikuwa kinyonge, hii ina nyimbo 15. Albamu hizi mbili zimemfanya Darassa kuwa rapa namba moja Bongo inayesikilizwa zaidi mtandaoni (most streamed).
7. High School (2021) - Harmonize: Nyimbo 20
Kati ya albamu sita ambazo Harmonize ameachia, High School (2021) ndio albamu yake yenye nyimbo nyingi zaidi ambazo ni 20, ikifuatiwa na albamu yake ya kwanza, Afro East (2020) yenye ngoma 18.
Albamu zake nyingine tatu, Made For Us (2022), Visit Bongo (2023), na 31 (2026), zote kila moja ina nyimbo 14. Na albamu yake yenye idadi ndogo ya nyimbo ni Muziki wa Samia (2024) yenye nyimbo 10.
8. Love Sounds Different (2022) - Barnaba: Nyimbo 19
Albamu ya tatu ya Barnaba, Love Sounds Different (2022) ina nyimbo 19, ikishirikisha mastaa kama Diamond Platnumz, Alikiba, Rayvanny, Lady Jaydee na Nandy, huku ilishinda tuzo ya TMA kama Albamu Bora.
Cha kufurahisha kuhusu albamu hii, Barnaba katika nyimbo 18 alishirikiana na wasanii wengine, hivyo ni wimbo mmoja tu ndio hakufanya kolabo ikiwa ni sawa na asilimia 5.26.
9. A Boy From Tandale (2018) - Diamond: Nyimbo 18
Albamu ya tatu na ya mwisho kutoka kwa Diamond Platnumz, A Boy From Tandale (2018) ina nyimbo 18, huku ikiwa na kolabo za mastaa wa nje kama P-Square, Ne-Yo, Rick Ross, Tiwa Savage, Omarion, Davido n.k.
Vilevile albamu ya kwanza ya Jux, The Love Album (2019) nayo ina nyimbo 18, huku albamu yake ya pili, King of Hearts (2022) ikiwa na nyimbo 16. EP pekee aliyotoa, A Day To Remember (2025) ina nyimbo saba.
10. Money Mondays (2018) - Vanessa Mdee: Nyimbo 17
Kabla ya kuacha muziki, Vanessa Mdee aliachia albamu moja, Money Mondays (2018) ikiwa na nyimbo 17, huku akishirikiana na mastaa kama Cassper Nyovest, Maua Sama, Joh Makini, K.O, G Nako na Reekado Banks.
Pia kuna wasanii wengine ambao albamu zao zina nyimbo 17, wanamuziki hao ni Marioo (The Kid You Know - 2022), Stereo Singasinga (Experience - 2021), Stamina (Msanii Bora wa Hip Hop - 2024), Marioo (The God Son - 2024) n.k.