Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yasisitiza mapambano dhidi ya uharamia wa maudhui

UHARAMIA Pict

Serikali imetoa wito kwa wadau wa sekta ya utangazaji kuimarisha mapambano dhidi ya uharamia wa maudhui, ikisema vitendo hivyo vinahatarisha ukuaji wa sekta ya ubunifu, uwekezaji na upatikanaji wa maudhui bora nchini.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma, alisema ulinzi wa haki miliki ni muhimu katika kuhakikisha wabunifu, watangazaji na wawekezaji wanapata stahiki zao na hivyo kuendelea kuwekeza katika uzalishaji na usambazaji wa maudhui yenye ubora.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kampeni ya DStv ya “Pata Zaidi” iliyofanyika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam, Mwinjuma alisema uharamia wa maudhui unadhoofisha mnyororo mzima wa thamani katika sekta hiyo kwa kuwanyima wabunifu na wamiliki wa maudhui mapato yanayostahili.

“Uharamia wa maudhui unadhoofisha mnyororo wa thamani unaosaidia uundaji, usambazaji na ubunifu wa maudhui. Ni lazima tushirikiane kulinda haki miliki na kujenga mazingira yatakayowezesha ubunifu na uvumbuzi kustawi,” alisema.

UHA 02

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma, akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya DStv ya Pata Zaidi.

Alisema mapambano hayo yanahitaji ushirikiano wa Serikali, mamlaka za udhibiti, wamiliki wa maudhui, watangazaji na watumiaji wa huduma hizo ili kuhakikisha haki miliki zinalindwa na uwekezaji katika sekta unaendelea.

Mwinjuma pia aliipongeza MultiChoice Tanzania kwa mchango wake katika kukuza maudhui ya ndani na kuendeleza sekta ya ubunifu nchini.

Katika uzinduzi huo, DStv ilitangaza maboresho ya huduma zake kupitia kampeni ya “Pata Zaidi”, ikiwemo kupunguza idadi ya vifurushi kutoka sita hadi vinne na kushusha bei za baadhi ya huduma ili kupanua wigo wa Watanzania wanaoweza kupata burudani na michezo ya kiwango cha juu.

Afisa Mtendaji Mkuu wa MultiChoice Tanzania, Sophie Tchatchoua, alisema maboresho hayo yanalenga kuongeza thamani kwa wateja kwa kuzingatia mahitaji na mapendeleo ya watazamaji wa Tanzania.

“Pata Zaidi ni kuwapatia wateja wetu thamani zaidi kupitia vifurushi vilivyoboreshwa, bei nafuu zaidi, maudhui mengi ya ndani na huduma zinazozingatia mahitaji ya watazamaji wa Tanzania,” alisema Sophie.

UHA 01

Afisa Mtendaji Mkuu wa MultiChoice Tanzania,Sophie Tchatchoua, akizungumza  wakati wa hafla ya uzinduzi wa Expect More katika Hoteli ya Serena, akisisitiza thamani zaidi, maudhui mengi zaidi ya ndani, na burudani iliyoboreshwa kwa wateja wa DStv.

Katika maboresho hayo, wapenzi wa michezo watapata kifurushi kipya cha DStv Sports kwa Sh50,000 badala ya Sh118,000 za awali, kikiwa na maudhui ya michezo ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya. Aidha, mashabiki wa Ligi Kuu ya England (EPL) wataweza kutazama mashindano hayo kupitia kifurushi cha DStv Select kwa Sh25,000, ikilinganishwa na Sh68,000 ya bei ya awali ya kifurushi cha Compact.

DStv pia imeanzisha SuperSport Kiswahili, chaneli maalumu ya michezo inayotoa matangazo na uchambuzi kwa lugha ya Kiswahili, hatua inayolenga kuwafikia mashabiki wengi zaidi na kurahisisha ufuatiliaji wa mashindano mbalimbali.

Kwa upande wa maudhui ya burudani, kifurushi cha DStv Starter kitapatikana kwa Sh15,000 badala ya Sh27,500, huku kampuni hiyo ikiendelea kuongeza tamthilia, filamu na vipindi vinavyozalishwa Tanzania na Afrika.

Miongoni mwa maudhui mapya ni tamthilia ya KARATA, inayotarajiwa kuanza kurushwa Novemba 2026, pamoja na Ubongo Kids inayolenga kuunganisha burudani na elimu kwa watoto.

Sophie alisema kampuni hiyo itaendelea kuwekeza katika michezo, maudhui ya ndani na vipindi vya elimu, akisisitiza kuwa uwekezaji endelevu unahitaji ulinzi wa haki za wabunifu na wamiliki wa maudhui.