Paula ataja sababu kumtetea Marioo
Muktasari:
- Kauli hiyo inakuja kufuatia tukio la hivi karibuni lililohusisha mwanamuziki Ibraah, ambaye alikuwa akimzungumzia Marioo kwenye mtandao wa kijamii kwa kauli zilizochukuliwa kama kumkejeli msanii huyo. Hali hiyo ilimfanya Paula kuingia kwenye mjadala huo kwa kutoa maoni yake sehemu ya comment na kuonyesha msimamo wake.
PAULA Kajala amefunguka sababu zinazomfanya asiwe tayari kukaa kimya pale mpenzi wake, msanii Omary Mwanga maarufu Marioo, anapozungumziwa kwa namna anayoona siyo sahihi, akisema kwake ni muhimu kusimama naye anapokumbana na changamoto.
Kauli hiyo inakuja kufuatia tukio la hivi karibuni lililohusisha mwanamuziki Ibraah, ambaye alikuwa akimzungumzia Marioo kwenye mtandao wa kijamii kwa kauli zilizochukuliwa kama kumkejeli msanii huyo. Hali hiyo ilimfanya Paula kuingia kwenye mjadala huo kwa kutoa maoni yake sehemu ya comment na kuonyesha msimamo wake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Paula alisema kwake ni wajibu kuingilia changamoto zinazomkabili mpenzi wake au baba wa mtoto wake, kwa kuwa hapendi kumuona akishambuliwa mitandaoni.
“Kwangu ni lazima kuingilia ugomvi au changamoto yoyote inayomtokea mpenzi wangu au baba wa mtoto wangu. Sipendi kumuona akishambuliwa mitandaoni halafu mimi nikakaa kimya,” alisema Paula.
Alieleza kuwa pia hapendi tabia ya watu kudhalilishana kupitia mitandao ya kijamii, akisema mambo yanayochapishwa huko yanaweza kuhifadhiwa na kuendelea kuonekana hata baada ya tukio kupita.
“Mimi sipendi mambo ya kudhalilishana mitandaoni kwa sababu mambo yanayowekwa huko yanahifadhiwa. Pia nina mtoto, hivyo ni lazima nifikirie mambo haya,” amesema.
Paula anaona kuwa kusimama na Marioo katika changamoto zinazomkabili ni sehemu ya nafasi yake kama mpenzi wake na mzazi mwenzake. Hivyo, anapoona kuna jambo linalomhusu, huona ni muhimu kutoa msimamo wake badala ya kukaa kimya.