Sanaa, silaha ya kumuenzi Mwalimu Nyerere
Muktasari:
- Kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, huadhimishwa nchini kila mwaka tarehe 14 Oktoba.
SANAA imepewa jukumu la kuendeleza urithi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kuibua fikra, maandiko na misingi aliyoisimamia katika maisha yake.
Hayo yameelezwa katika maadhimisho ya Mwalimu Arterial Konekti, yaliyoandaliwa na Arterial Network Tanzania kwa lengo la kuwaunganisha wasanii na wadau wa utamaduni katika kumuenzi Baba wa Taifa.
Kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, huadhimishwa nchini kila mwaka tarehe 14 Oktoba.
Tukio hilo lililofanyika Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Posta, Dar es Salaam, leo Oktoba 13, 2026, lilihudhuriwa na mgeni rasmi, Mzee Joseph Butiku ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, pamoja na baadhi ya wasanii na wadau wa sanaa na Basata.
Maadhimisho hayo yamelenga kutumia sanaa kuendeleza falsafa na mchango wa Nyerere kwa jamii. Akizungumza katika tukio hilo, Butiku amesisitiza kuwa kumuenzi Mwalimu Nyerere kunapaswa kwenda zaidi ya kukumbuka historia yake ya uongozi, akieleza umuhimu wa kuhifadhi fikra na maandiko yake.
“Nyerere hapaswi kukumbukwa kama kiongozi tu, bali pia kama mtu aliyefikiri, aliyeandika na kuacha maarifa kwa jamii,” amesema Butiku.
Akifafanua namna ya kuendeleza urithi huo, Butiku alieleza umuhimu wa kutumia sanaa mbalimbali, zikiwemo uchoraji, mashairi na uandishi, pamoja na kukusanya maandiko ya Mwalimu.
“Tuitumie sanaa kueleza kazi na fikra za Mwalimu ili kizazi cha sasa na kijacho kiweze kuzielewa na kujifunza kutoka kwake,” amesema Butiku.
Maadhimisho hayo yamefungua nafasi kwa wasanii na wadau wa utamaduni kushirikiana kwa kusisitiza kulinda na kuheshimu tamaduni zetu.
Kupitia sanaa, misingi hiyo inaweza kufikishwa kwa watu wengi zaidi, huku historia ya taifa ikiendelea kuhifadhiwa kwa vizazi vijavyo.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Sanaa na Fursa tunakupandisha!”, imeweka msisitizo katika kutumia sanaa kufungua fursa za elimu, masoko, uwekezaji, ajira, biashara na ushirikiano.