Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kutoka 'Amini wa Linah hadi Amini Afrika' amtaja Ruge, Chama

AMINI Pict

Muktasari:

  • Amini anasema kipindi ambacho mashabiki waliona asikiki  redioni na kwenye televisheni ni kwa sababu alikuwa akijikita zaidi kwenye bendi yake ambayo hujikita kwenye maonyesho mbalimbali.

MWANAMUZIKI Amini THT amefunguka mambo mbalimbali kuhusu safari yake ya muziki, maisha ndani ya THT pamoja na uhusiano wake na marehemu Ruge Mutahaba.

Akizungumza na Mwanaspoti maeneo ya Mwananyamala Komakoma jijini Dar es Salaam, Amini anasema bado yupo kwenye muziki na ukimya wake haukuwa wa kuachana na kazi hiyo, bali alikuwa akijenga bendi yake ya Amini Band ambayo sasa inafanya shughuli mbalimbali.


AMI 01

SABABU YA UKIMYA WAKE 

Amini anasema kipindi ambacho mashabiki waliona asikiki  redioni na kwenye televisheni ni kwa sababu alikuwa akijikita zaidi kwenye bendi yake ambayo hujikita kwenye maonyesho mbalimbali.

“Nilikuwa najenga Amini Band. Tunafanya shughuli mbalimbali, hatuna sehemu moja ya kusema tunapiga kila siku, tunapiga kwenye matukio mbalimbali,” anasema.

Kwa sasa, anasema ameamua kurudi zaidi kwenye kazi zake kama msanii binafsi ili kuongeza thamani yake sokoni na wakati huo huo kuongeza thamani ya Amini Band.

Anaendelea na kazi mpya zikiwemo Kaisari na Unguja, ambazo zote ni nyimbo za mapenzi, pia anasema anaandaa video zake huku akisema kuna kazi nyingine inakuja yenye ladha ya mtindo wa Singeli.


AMI 02

THT ILIMTOA HIP HOP

Amini anasema kabla ya kuingia THT alikuwa msanii wa Hip Hop na wimbo wake wa kwanza aliutoa mwaka 2002.

Anasema baadaye alikutana na Vumilia aliyemwelekeza kwenye THT, ambako aliingia mwishoni mwa mwaka 2004.

“Nilikuwa nimeanza kama Hip Hop. THT ndio walinibadilisha nikaanza kuimba Bongo Flava na Live Band,” alisema.

Kwa Amini, muziki haukuwa jambo la bahati mbaya, anasema familia yao ina historia ya muziki, huku dada zake wakiimba kwaya na kaka yake mkubwa, Bahati Mwenyemkumpila, aliyefariki, akiwa mpiga gitaa wa solo. Anasema muziki upo kwenye damu yao.


AMI 03

RUGE ALIONA MBALI

Anapokumbuka safari yake ndani ya THT, Amini hawezi kumuacha Marehemu Ruge Mutahaba. Anamkumbuka kama bosi aliyekuwa karibu na wasanii wake na aliyekuwa na uwezo wa kuona mbele.

Anasema Ruge alikuwa akisikiliza nyimbo zao kabla hazijatoka na kutoa maoni kama wimbo una uwezo wa kuwa hit au la.

“Ruge alikuwa bosi ambaye alikuwa anatusikiliza nyimbo kabla hazijatoka, anaangalia hii ni chuma au sio chuma,” anasema.

Mbali na muziki, Amini anasema Ruge aliwasaidia hata kwenye changamoto za maisha, akimfananisha na mzazi.

“Ruge alikuwa zaidi ya bosi, alikuwa kama mzazi. kuna wakati unapata shida ya kodi, maisha na mambo mengine, anakusaidia,” anasema.

Hata hivyo, anasema Ruge aliwafundisha pia kujitegemea kwa sababu alijua asingekuwepo milele.


SIRI YA WIMBO 'ROBO SAA'

Miongoni mwa mambo makubwa aliyoyafafanua Amini ni historia ya wimbo wake wa Robo Saa ambao unaendelea kutamba hadi sasa, wimbo uliompa jina kubwa yeye na Barnaba.

Amini anasema kipindi hicho yeye na Barnaba walikuwa THT na walikuwa wakifananishwa na kundi la wanamuziki P-Square wa Nigeria.

Ruge aliwapa kazi za kuimba nyimbo za P-Square, lakini wao wakaona kufanya hivyo kungechelewesha kupata utambulisho wao.

Wakaamua kutengeneza nyimbo zao wenyewe, jambo lililowafanya waondolewe THT mara kadhaa.

Baadaye Amini alipata simulizi kutoka kwa rafiki yake, Mtima Salehe, aliyekuwa ameumizwa na mapenzi baada ya kuachwa na mpenzi wake aliyechagua mwanaume mwingine.

“Anasema, huyo rafiki yake alikuwa akisema anatamani kufa sasa hivi.’ Mimi nikachukua hilo nikaliandika, lakini nikaja kubadilisha nikasema, ‘Bado Robo Saa, kufariki,’” anasema.


AMI 05

HAPO NDIPO WAZO LA ROBO SAA LILIPOANZIA.

Baada ya kurejea THT na nyimbo zao wenyewe, Ruge awali hakuwataka, lakini baadaye aliwasikiliza na kuwaita tena.

Moza Kinanda ndiye aliyefanya beat ya Robo Saa na Njia Panda kwa kutumia Yamaha keyboard. Amini alirekodi kwa M-Lab huku Barnaba akirekodi Enrico.

Amini pia anakumbuka jinsi Ruge alivyokuwa makini hata kwenye backing vocals. Anasema Ruge hakupendezwa na baadhi ya sauti za Dito alizoziona kuwa za zamani, akitabiri kuwa baada ya miaka kadhaa wangeona tofauti yake.

Kwa Amini, hilo linaonyesha Ruge alikuwa na maono makubwa.

“Bosi alikuwa yuko mwaka wa mbele sana na kiatu chake ni kikubwa sana, hakuna mtu ambaye anaweza akakivaa maana vitu ambavyo alikuwa akisema Ruge Leo ndio anaviona” anasema.


AMI 04

LINAH, BARNABA NA ‘BIFU’

Kuhusu uvumi wa aliwahi kuwa na bifu na Barnaba kuhusu Linah, Amini anasisitiza kuwa hakukuwahi kuwa na ugomvi kati yake na Barnaba, bali watu walikuwa wakizungumza bila ya kuwa na uhakika.

Alieleza kuwa kipindi hicho Barnaba alikuwa karibu na mdada anayeitwa Lulu, ambaye alikuwa rafiki wa Linah, huku yeye akiwa karibu na Linah. Hivyo watu wakaanza kuwaunganisha kwa namna yao, anasema yeye na Linah walikuwa wapenzi ila kwasasa kila mmoja anaendelea kama ndugu na wanamuziki wanaosaidiana.

"Sikuwa kuwa na bifu na Barnaba kuhusu Linah,kwani Linah alikuwa mpenzi wangu mimi na Barnaba alikuwa na mpenzi wake aliyekuwa anaitwa Lulu, sasa Lulu na Linah walikuwa ni marafiki, hivyo watu walikuwa wanachanganya mambo kusema tuna bifu kisa Linah."

Hata hivyo, alisema amechoka kuitwa kwa majina yanayomrudisha kwenye kazi zake za zamani.

Mashabiki wamekuwa wakimwita “Amini wa Linah”, “Amini wa THT” au “Amini wa Robo Saa”, lakini sasa anataka jina lake litumike kama Amini Africa.

Amini anasema ameongeza jina la Africa kwa sababu anaamini sauti na aina ya muziki anaoufanya vina ladha ya Kiafrika.

Anataka mashabiki waanze kumtafuta kwenye majukwaa ya muziki kwa jina Amini Africa, ambako watakutana na nyimbo zake mpya na zile za zamani kama Robo Saa, Unikimbie na Mtima Wangu.


AMI 06

HAWA HAPA ANATAKA KUFANYA NAO COLLABO

Amini pia anasema anataka kushirikiana na wasanii wengi zaidi, akiwataja Marioo, Harmonize, Alikiba na J Melody.

Lakini mmoja anayemtamani zaidi ni Barnaba, ambaye anamuita pacha wake.

“Barnaba ni pacha wangu. Kuna kazi tumesharekodi, bado haijatoka. Iko kwenye mixing na mastering kwa Duly Thomas,” anasema.


AMI 07

NDOTO YA CHUO CHA MUZIKI

Amini anasema ndani ya miaka mitano ijayo anataka kuwa mkubwa zaidi kwenye muziki na katika maeneo mengine ya maisha.

Miongoni mwa ndoto zake kubwa ni kuwa na chuo cha muziki kitakachowasaidia vijana wenye ndoto za kutumia sanaa kujiajiri na kusaidia familia zao.

“Natamani kuwa na music college yangu, niweze kuwasaidia vijana ambao wana ndoto za kutumia muziki na sanaa kusaidia familia zao,” anasema.

Amini pia alifichua kuwa kitu ambacho hakipendi ni kudharauliwa au kusemwa vibaya nyuma yake.

Anasema mtu mwenye tatizo naye ni bora amfuate na kuzungumza naye moja kwa moja kuliko kumsema kwa watu wengine.


AMI 08

AMINI NI SHABIKI WA SIMBA, KUMKUBALI CHAMA

Kutoka kwenye muziki hadi mpira, Amini ni shabiki wa Simba na anasema anamiliki jezi za timu hiyo za misimu tofauti.

Kuhusu Dabi, ya Jumamosi ya Simba na Yanga, anasema ni mchezo ambao hauwezi kutabirika na kila upande unaweza kushinda au sare.

“Mchezo ni mgumu. Ila kuna mtu atakufa,” anasema kwa mzaha akielezea ushindani mkubwa uliopo kwenye mchezo huo.

Miongoni mwa wachezaji anaowakubali zaidi ni Clatous Chama, ambaye kwa amini ana akili kubwa ya mpira.

“Anaweza akakosea hata mara 20, lakini mara ya 21 akakupa furaha. Yule jamaa ana brain kubwa sana ya mpira,” anasema.

Kuhusu wachezaji wapya wa Simba yaani usajili, Amini anasema mashabiki wanapaswa kuwapa muda ili waizoe mazingira na wenzao.

Kwa uongozi wa klabu hiyo, ujumbe wake ni mmoja umoja.

“Simba Nguvu Moja,” anasema, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano ndani na nje ya uwanja ili kufikia malengo ya klabu.