Sababu wasanii bongo kushobokea nyimbo za Wizkid
STAA wa Nigeria, Wizkid ni miongoni mwa wasanii wa Afrika waliofanikiwa sana duniani akiwa ameshinda tuzo kubwa ikiwemo Grammy, BET na Soul Train, huku akifanya kazi na wasanii wenye ushawishi kama Beyonce, Drake, Justin Bieber, Chris Brown n.k.
Miaka miwili iliyopita Wizkid alifanya vizuri sana na wimbo
‘Essence’ kutoka katika albamu yake ya nne, Made in Lagos (2020), wimbo huo aliomshirikisha Tems ulishinda BET hivyo kuwania Grammy na kuingia chati za Billboard Hot 100.
Kutokana na umaarufu wake, baadhi ya wasanii Bongo walikuwa na mwitikio mkubwa wa kufanya remix na refix za wimbo huo ambao ni wa kwanza Nigeria kuingia Billboard Hot 100 na Billboard Global 200, huku ukishika namba moja U.S. Afrobeats Songs.
Miongoni mwa waliofanya hivyo ni Salmin Swaggz kutoka kundi la OMG, Maarifa wa Manzese Music Baby (MMB), Country Boy na Tommy Flavour kutoka Kings Music.
Kubwa zaidi Diamond Platnumz alichukua vionjo vyake na kuvitumia katika wimbo wake, Loyal (2022) kutoka katika EP yake ya kwanza, First of All (FOA), huku S2kizzy akikiri wazo lilianzia kwa Essence ya Wizkid.
Ikumbukwe huo ni wimbo wa pili kwa Wizkid kupendwa na wasanii wa Bongo na nchi nyingine za Afrika Mashariki, mathalani wimbo wake, Ojuelegba (2014), ulifanyiwa refix na Wakazi kutoka Tanzania na Khaligraph Jones wa Kenya.
Je, kwa nini nyimbo za Wizkid zinafikia hatua hii huku zile Bongo Fleva zikiwa hazipata nafasi hiyo katika nchi nyingie? na hili linatoa funzo gani hasa kwa wasanii Bongo ambao baadhi yao wamekuwa wakiiga sana muziki wa nje?.
Kwa kulichambua hilo, Jabir Saleh ‘Kuvichaka’, Mtangazaji wa vipindi vya burudani E FM Radio, ameliambia gazeti hili Wizkid anakuwa na ushawishi kutokana ana uongozi unaosimamia uweledi na ubora wa muziki wake.
“Kitendo cha watu kama Ghostface Killah ambaye ni msanii mkubwa sana wa Hip Hop duniani, kurap ule mdundo wa Essence ilishtua watu ulimwenguni, sasa wasanii wengi kama DaBaby ndio wakafuata,”
“Yaani Ghostface Killah kutoka Wu-Tang Clan, kundi la Hip Hop lenye heshima zaidi duniani kwa miaka yote ameweza kufanya na kuheshimu, ina maana kazi ya dogo (Wizkid) ni kubwa. Kwa nini na mimi nisifanye, ndio msingi wa kuvutia wasanii wengi hata kutokea hapa nyumbani, hivyo ni msukumo wa wasanii wengine duniani,” anasema Jabir.
Anasema kikawaida wimbo ukiwa unafanya vizuri duniani huwa unapata usikivu wa watu wengi sana na wasanii kama wakipenda mdundo na jinsi ulivyoweza kuvuma, ndipo nao wao wanajaribu kufanya mitindo yao (new version) ndio inakuwa kama ni remix, refix au cover.
“Ubora wa kazi ndio unaleta hilo, ukiangalia jinsi wasanii wetu wanavyotoa kazi zao na wanavyozitangaza, bado. Tusiwalaumu kutokana na vipato vyao na menejimenti zao zilivyo, nyingi zipo kimagumashi, sasa hiyo inakuwa ni ngumu sana kufanikiwa.”
“Kuna shida moja hapa Tanzania, wasanii wanazingatia ubora wa video kuliko audio (wimbo wenyewe) wakati wanapaswa kuipigania zaidi audio,” anasema Jabir na kuongeza;
“Kuna mtu wa kimataifa aliniambia audio za Tanzania zina shida sana, yaani production ni mbovu mno!, unaweza kuvutia na video lakini audio unakuta hamna kitu, hivyo wanakosa nafasi sehemu nyingi za nje ambazo watu wanasikiliza muziki tu.”
Kwa upande wa Rapa ZaiiD ambaye aliwakosoa vikali wasanii wenzake kukimbilia kufanya remix ya ngoma hiyo, Essence, naye anasema hilo halina faida kwa ukuaji wa Bongo Fleva.
“Nadhani haileti maana kwa sababu waliitangaza hiyo ngoma huku zaidi, kuliko msanii kujitangaza kule kwao, hata mtandaoni nilipoona wasanii wengi Bongo wamefanya, niliuliza kwa nini Essence?, kuna faidi gani ambayo Wizkid atakupa wewe, ukweli ni kwamba haipo,” anasema.
ZaiiD ambaye amewahi kufanya cover za ngoma kama Who Dat ya J Cole na Trap Queen ya FettyWap miaka nyuma, ametupia lawama vyombo vya habari kwa kile alichodai vinazipa nafasi zaidi baadhi ya ngoma kutoka nje na kusahau nzuri za nyumbani.
“Niwe mkweli tu bila kupindisha maneno, media zetu kubwa zimekuwa zikisapoti moja kwa moja muziki wa nje kuliko wasanii wengi wa hapa. Kwa mfano wanaweza kuangalia chati ya Billboard au ya Nigeria na Afrika Kusini, kisha wakatoa ngoma huko wakaileta hapa na kuicheza na kuipa chati kubwa lakini hapa kuna kubwa hazipati hiyo nafasi,” anasema na kuongeza;
“Wenzetu Wanigeria wanapendana, ukifumba macho ukawaza Nigeria ipoje, utaona kuna wasanii wakubwa wengi sana ila leo tukiulizana hapa Bongo wasanii wakubwa wangapi, unaweza kukuta mmoja au wawili, wengine wanasuasua tu,” anasema ZaiiD aliyetamba na wimbo, Wowowo (2017).