Juma Jux, Prisiclla mapenzi yalivyoandika rekodi
Muktasari:
- Jux na Priscilla ambaye ni binti wa mwigizaji maarufu wa Nollywood, Iyabo Ojo, ni miongoni mwa mastaa wenye nguvu kubwa ya ushawishi katika mitandao ya kijamii hasa Instagram.
ZIMESALIA siku chache kutimia mwaka mmoja tangu mwanamuziki wa Bongofleva, Jux na mkewe Prisiclla kuusimamisha mtandao wa Instagram kufuatia chapisho lao ambalo hadi sasa linashikilia rekodi Bongo.
Jux na Priscilla ambaye ni binti wa mwigizaji maarufu wa Nollywood, Iyabo Ojo, ni miongoni mwa mastaa wenye nguvu kubwa ya ushawishi katika mitandao ya kijamii hasa Instagram.
Wawili hao waliweka wazi uhusiano wao mnamo Julai 2024 ikiwa ni miezi michache tangu mwanamuziki huyo kuachana na aliyekuwa mpenzi wake, Karen Bujulu ambaye walidumu kwa takribani mwaka mmoja.
Julai 24, 2025, Priscilla na Jux katika posti yao ya ushirikiano Instagram, ndipo walitangaza kuwa wanatarajia kupata mtoto wao wa kwanza.
Posti hiyo ilishindikizwa na maneno: Mom & Dad. Blessed, grateful, thankful - wakiwa na maana kuwa ni wazazi waliobarikiwa na waliojawa na shukrani kwa kufikia hatua hiyo muhimu katika maisha.
Sasa hadi kufikia wakati huo zikiwa zimesalia siku tano kutimiza mwaka mmoja, posti hiyo ndio iliyofanya vizuri zaidi katika mtandao wa Instagram kwa mastaa hao na Tanzania kwa ujumla.
Ni posti ambayo imepata likes (imependwa) milioni 1.1, comments (maoni) 91,500, na share (idadi ya posti husika kusambazwa) 110,000. Hakuna staa yeyote Bongo ambaye chapisho lake Instagram limewahi kupata namba kama hizo.
Ikumbukwe duniani posti ambayo imepata likes nyingi zaidi, ni Lionel Messi ambayo aliiposti Desemba 19, 2022 akimuuonyesha akiinua juu Kombe la Dunia ambalo Argentina walishinda nchini Qatar, ikiwa ni mara yake ya kwanza. Hadi sasa posti hio ina likes milioni 74.5.
Posti hiyo ya Jux na mkewe ilifanya vizuri kutokana na um aarufu na ukubwa wa tukio hilo ambapo miezi kadhaa nyuma tayari zilikuwepo tetesi kuwa Priscilla ni mjamzito. Katika posti hiyo yenye picha nane, Priscilla alithibitisha ukweli wa jambo hilo.
Siku wanatangaza kuwa Priscilla ni mjamzito, ndipo Jux alipoachia wimbo wake mpya, Thank You (2025) ambao anamshukuru mkewe kwa zawadi hiyo ambayo ni mara ya kwanza kuipata maishani mwake.
Katika video ya wimbo huo uliotayarisha na S2kizzy huku ikiongozwa na Director Kenny, Priscilla anaonekana mwenye furaha sana kwa muziki huo mzuri lakini hasa kile alichokuwa akitarajia.
Hiyo ikawa video ya nne yake Jux kwa Priscilla kutokea baada ya kufanya hivyo katika Ololufe Mi (2024), Si Mimi (2025) na God Design (2025) kutoka katika Extended Playlist (EP) yake ya kwanza, A Day To Remember.
Kufikia mwishoni mwa Agosti, 2025, wakatangaza kuwa wamejaliwa mtoto wa kiume na kumpa jina la Rakeem, na mtoto huyu alizaliwa nchini Canada.
Jux alidai sababu ya mtoto wake kuzaliwa Canada ili kutoka fursa kwa mtoto wake hapo baadaye kuweza kuchagua uraia anaotaka!.
“Lakini akienda kuzaliwa nje labda akapata passport ya Marekani au Canada, akifika hapa Tanzania pia watampa hadi afikishe miaka 18 ndio achague uraia.
Wakati wanatangaza uhusiano wao, Priscilla alikuwa na wafuasi milioni 2.8 katika ukurasa wake wa Instagram ila sasa ikiwa ni miaka miwili, wamefikia milioni 4.7, hivyo akiwa na staa huyo wa Bongofleva ameongeza wafuasi milioni 1.9.
Hii ina faida kwa Priscilla upande wa kazi yake ya ushawishi wa chapa mtandaoni ambapo amewahi kufanya kazi na kampuni ya cryptocurrency ChiJ14Exchange, kampuni ya utengenezaji wa filamu ya Viskit, chapa ya vipodozi Hegai and Esther.
Kwa mujibu wa Priscilla akizungumza katika podcast ya Chude Jideonwo mnamo Mei, yeye na Jux kwa mara ya kwanza walikutana kwa mara ya kwanza nchini Rwanda.
“Nilikutana na mume wangu nchini Rwanda, na alivutiwa na mimi ghafla. Alinipa namba yake na kuniomba nimtumie ujumbe…” alisema Priscilla Ojo.
Katika hatua nyingine, Priscilla alidai kipindi anaanzisha uhusiano na mwanamuziki huyo walipanga kupata watoto 16 lakini kwa sasa wamebadili mipango.
“Nilipokutana na mume wangu, tulisema tutakuwa na watoto 16, lakini sasa baada ya kupata mtoto mmoja, mpango unabadilika,” alieleza.
Ikumbukwe baada ya wawili hao kufunga ndoa ndoa Februari 7, 2025, walienda Nigeria anapotokea Priscilla kwa ajili ya taratibu nyingine ambazo ziliambatana na sherehe zenye ufahari mwingi, kitu kilichochochea mijadala mtandaoni. Mpangilio wa tukio zima hadi kufikia tamati ilikuwa ni gumzo huku baadhi wakihoji kuhusu gharama hadi kuibuka madai kuwa Jux amekopa fedha kiasi cha Sh1 bilioni ili kufanikisha hilo, madai aliyoyakanusha vikali.
Hatimaye Mei 28, 2025, katika ukumbi wa The Superdome, ndipo Jux na Priscilla walifanya harusi yao kubwa ikiwa ni kilele cha mfululizo wa sherehe tangu walipofunga ndoa Februari 7 ikiwa ni miezi nane ya uhusiano wao.