Rayvanny, Fahyma hii sasa sifa!
Muktasari:
- Rayvanny, mwanzilishi wa Next Level Music (NLM), amekuwa katika uhusiano na Fahyma kwa miaka zaidi ya 10 sasa huku wakijaliwa kupata mtoto mmoja, Jaydan, 9.
STAA wa Bongofleva, Rayvanny, 33, na mpenzi wake wa muda mrefu, mwanamitindo Fahyma, 29, ni kama tayari wameiumba dunia yao linapokuja suala la kufanya kazi kwa pamoja.
Rayvanny, mwanzilishi wa Next Level Music (NLM), amekuwa katika uhusiano na Fahyma kwa miaka zaidi ya 10 sasa huku wakijaliwa kupata mtoto mmoja, Jaydan, 9.
Fahyma ameshatengeneza jina lake katika mitindo akishinda tuzo mbalimbali za kimataifa kama Scream Awards (Nigeria), Starqt Awards (Afrika Kusini) na Swahili Fashion Week Awards (Tanzania).
Wiki hii mwanamitindo huyo ameonekana tena katika video ya wimbo mwingine wa Rayvanny, hatua ambayo inamfanya kuzidi kuitunza rekodi yake ya kipekee kwa mwanamuziki huyo.
Katika wimbo huo, Touch (2026) uliotayarishwa na S2kizzy kutokea studio za Pluto Republic, Fahyma ameonekana kuanzia mwanzoni hadi mwisho ambapo wameonyesha jinsi mapenzi yao yalivyo.
Hiyo inakuwa video ya saba ambayo Rayvanny amefanya na Fahyma, mrembo ambaye pia hajawahi kutokea katika video ya mwanamuziki mwingine yeyote zaidi ya Rayvanny, mshindi wa BET 2017.
Mbali na Touch (2026), video nyingine ni za nyimbo kama Kwetu (2016), Natafuta Kiki (2016), Siri (2017), Forever (2023), Habibi (2023) na Mwambieni (2023).
Katika wi mbo uliomtoa Rayvanny kimuziki wakati huo akiwa chini ya WCB Wasafi, Kwetu (2016), Fahyma alicheza uhusika mdogo ikiwa ndio kazi ya kwanza kufanya pamoja.
Hata hivyo, baada ya hapo video zote zilizofuatia Fahyma amecheza kama mhusika mkuu, yaani video vixen, ambaye ni mrembo anayejua kuonyesha mitindo ya uchezaji au uigizaji katika video kulingana na hadithi ya wimbo husika kwa lengo la kuipendezesha.
Ikumbukwe neno video vixen lilianza kushika kasi mapema miaka ya 2000 katika muziki huko Marekani kwa sababu video zilikuwa na matumizi makubwa ya wanawake warembo waliokuwa wakicheza au kuigiza.
Sasa Fahyma ndiye amekuwa kinara wa kufanya kazi hiyo katika video za Rayvanny, amefanya hivyo tangu 2016 hadi sasa 2026. Kwa hiyo ndani ya miaka hii 10, ni hizo video saba ambazo wameshuti pamoja.
Hata hivyo, Rayvanny si mwanamuziki wa kwanza kushuti video saba pamoja na mpenzi na mzazi mwenzie, rekodi hiyo tayari ilishawekwa na Marioo na Paula tangu mwaka uliopita.
Paula ameonekana katika video saba za Marioo ambazo ni Lonely (2023), Tomorrow (2023), Sing (2023), Hakuna Matata (2024), My Daughter (2024), Unachekesha (2024) na Tete (2025), na ndiye mrembo aliyetokea mara nyingi zaidi katika video zao mwanamuziki huyo.
Marioo na Rayvanny ni kama wamekuwa wakishindana kuwatumia wapenzi wao katika video za nyimbo zao. Mathalani, ukitazama mtiririko wa kazi zao utabaini kuwa mwaka 2023 kila mmoja alishuti video tatu na mpenzi wake!.
Lakini sifa moja inayomtofautisha Fahyma na Paula, ni kwamba Fahyma hajawahi kushuti video na msanii mwin gine yeyote yule zaidi ya Rayvanny. Lakini Paula kabla ya Marioo, alishashuti na Rayvanny video ya wimbo, Wana weweseka (2021).
Katika video saba za Rayvanny na Fahyma, iliyofanya vizuri zaidi YouTube hadi sasa ni ya wimbo Kwetu (2016) uliotayarishwa na Laizer Classic, huku video yenyewe ikiongozwa na Godfather kutokea Afika Kusini.
Video hiyo imeshatazamwa (views) zaidi milioni 48.5, ikishika nafasi ya sita katika orodha ya video za Rayvanny zilizofanya vizuri zaidi katika mtandao huo.
Katika video hiyo Fahyma alitokea mwishoni kabisa, huku video vixen akiwa Lyyn ambaye baadaye alikuja kuzungumziwa zaidi alipotokea katika video ya Mbosso, Hodari (2018) akionyesha uwezo mkubwa wa kucheza.
Utakumbuka baada ya video hizo mbili, Lynn aliingia katika Bongofleva kama mwanamuziki, wimbo wake wa kwanza, Chafu (2018) ulipata mapokezi mazuri kwa kiasi chake, lakini hakuwa na mwendelezo mzuri.
Hivyo licha ya panda shuka, kuachana na kurudiana, tunaweza kusema Fahyma ni mwanamke nyuma ya mafanikio ya Rayvanny kwa kipindi chote ambacho wamekuwa pamoja. Amekuwa naye kabla ya kutoa wimbo wake wa kwanza chini ya WCB Wasafi, hadi sasa anapomiliki lebo yake ya NLM.
Ni Rayvanny ambaye ni msanii wa kwanza aliyetolewa na WCB Wasafi kushinda tuzo nyingi za kimataifa, ambapo ameshinda tuzo kama BET (Marekani) 2017, Zikomo (Zambia) 2022, Afrimma (Marekani) 2022, EAEA (Kenya) 2022, DIAFA (Dubai) 2022 na kadhalika.