Hatua kwa hatua hadi kuja kuwa Jay Melody
Muktasari:
- Hata hivyo, Jay Melody ambaye tayari ameachia albamu mbili (Therapy 2024 & Addiction 2025), haikuwa rahisi kufikia hapo alipo kwa sasa, ni mchakato uliochukua miaka kadhaa ya kupambana kama ifuatavyo.
MWIMBAJI wa Bongofleva, Jay Melody amezidi kujenga ushawishi katika tasnia hiyo kutokana na umaarufu wa nyimbo zake ambazo zimebeba ujumbe unaogusa maisha ya wengi hasa upande wa mapenzi na mitindo ya maisha.
Hata hivyo, Jay Melody ambaye tayari ameachia albamu mbili (Therapy 2024 & Addiction 2025), haikuwa rahisi kufikia hapo alipo kwa sasa, ni mchakato uliochukua miaka kadhaa ya kupambana kama ifuatavyo.
1. Ndoto ya muziki ilianzia sehemu alipozaliwa yaani Tandale jijini Dar es Salaam ingawa wazazi wake wana asili ya Morogoro, mkoa ambao umewakuza mastaa kama Afande Sele, Belle 9, Stamina, Dayna Nyange na kadhalika.
2. Baada ya kuhitimu kidato cha nne na kushindwa kuendelea na masomo, Jay Melody hakuwa na kazi rasmi hivyo alifanya vibarua mbalimbali kama kuuza mitumba na kupiga msasa katika karakana za mbao.
3. Alianza kufukuzia ndoto kwa kujaribu kupata nafasi katika taasisi ya kukuza vipaji vya muziki ya Tanzania House of Talent (THT), lakini haikuwa rahisi kwani ilimlazimu kufunga safari za kwenda na kurudi kila mara. Utakumbuka THT ndio imewatoa wanamuziki maarufu kama Barnaba, Mwasiti, Amini, Linah, Recho Kizunguzungu, Ally Nipishe, Jolie, Ibraah Nation na kadhalika.
4. Usahili uliompitisha Jay Melody ndani ya THT, ulisimamiwa na Mwasiti ambaye kupitia taasisi hiyo ndipo naye alisikika katika Bongofleva kwa mara ya kwanza kupitia wimbo wake, Niambie (2006) uliotayarishwa katika studio ya Lady Jaydee.
5. Takribani vijana 50 waliopimwa uwezo wao wa kuimba, ni watano tu ambao Mwasiti na jopo lake waliona wana vipaji ambavyo vikinolewa kidogo vitafaa kwa tasnia, na Jay Melody alikuwa miongoni mwa hao watano waliochaguliwa.
6. Wimbo wa kwanza Jay Melody kurekodi THT, alipewa kazi ya kuurudia (cover) wimbo wa Mwanahela ‘Mahaba ya Dhati’ ambao umerudiwa na wanamuziki mbalimbali akiwemo Ray C chini ya Smooth Vibes.
7. Hadi anakaribia kuachia wimbo wake wa kwanza, Goroka (2017) bado alikuwa hajapata jina rasmi la kutumia katika muziki, wakati huo alikuwa akijiita ‘Jay Sana’ ila THT wakaja kupendekeza atumie ‘Jay Melody’ ambalo limesimama hadi sasa.
8. Aliyetayarisha wimbo huo (Goroka) ambao ndio uliomtoa kimuziki, ni Ringtone, mtayarishaji muziki ambaye aliletwa THT na Nandy ambaye alikuja kuandikiwa nyimbo nyingi na Jay Melody ambazo zilifanya vizuri. Baadhi ya nyimbo hizo ni Kivuruge (2017), Njiwa (2018), Hallelujah (2019) na Hazipo (2018), ambazo kwa sehemu zilijumuishwa katika albamu ya kwanza ya Nandy, The African Princess (2018).
9. Mbali na Nandy, wanamuziki wengine waliopita THT ambao Jay Melody alishiriki kuwaandikia nyimbo ni Benson (Hauzimi), Jolie (Sina), Malkia Karen (Tunaendana) na kadhalika.
10. Wimbo uliokuja kubadili kila kitu katika safari ya muziki yake Jay Melody, ni Nakupenda (2022) ambao umetayarishwa na Jinix66, huku video yake imeongozwa na Director Kenny, mshindi wa tuzo za AFRIMMA 2021. Hadi sasa, Nakupenda ndio wimbo wa Jay Melody uliouza zaidi mtandaoni (digital streaming), na ulishinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2022 katika kipengele cha Wimbo Bora wa Mwaka, ikiwa ni tuzo yake ya kwanza kutoka TMA.