Paula, Fahyma wafunguka sababu ya bifu lao kumalizika
Muktasari:
- Bifu hilo liliibuka zaidi mwaka 2021, wakati Paula alipokuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na Rayvanny, ambaye kabla yake alikuwa kwenye uhusiano na Fahyma na tayari walikuwa wamejaliwa mtoto.
BAADA ya miaka kadhaa ya kuhusishwa na bifu lililozua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, Paula Kajala na Fahyma, wamefunguka kuhusu hatua ya kuweka tofauti zao pembeni, huku wakisisitiza kuwa umri, muda na maisha vimewafanya kufikia hapo.
Bifu hilo liliibuka zaidi mwaka 2021, wakati Paula alipokuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na Rayvanny, ambaye kabla yake alikuwa kwenye uhusiano na Fahyma na tayari walikuwa wamejaliwa mtoto.
MWANZO WA BIFU
Mwaka 2021, uhusiano wa Paula na Rayvanny ulipoanza kuwa wazi, hali hiyo ilizua mjadala mkubwa kwa sababu Rayvanny alikuwa na historia ya uhusiano na Fahyma.
Kwa kipindi hicho, Paula alijikuta akitajwa kama mtu aliyekuwa ameingia katikati ya uhusiano wa Rayvanny na Fahyma, jambo lililofanya jina lake lihusishwe na lawama kutoka kwa baadhi ya watu waliokuwa wakifuatilia sakata hilo.
Hata hivyo, baadaye taarifa zilizochapishwa wakati huo zilieleza kuwa Rayvanny na Fahyma walikuwa tayari wamekwishatengana kabla ya uhusiano wa Rayvanny na Paula kuanza.
MIAKA IKAPITA
Baada ya uhusiano wa Paula na Rayvanny kufikia mwisho, kila mmoja aliendelea na maisha yake. Paula baadaye alihusishwa kimapenzi na Marioo, huku Rayvanny na Fahyma wakionekana kurejea pamoja.
Mwanaspoti pia iliripoti Machi 2026 kwamba ushindani uliokuwa ukihusishwa na Paula na Fahyma ulikuwa umehamia zaidi kwenye eneo la maudhui, mitindo na maisha yao ya mitandaoni, huku wote wawili wakiwa wameendelea kujenga majina yao kupitia shughuli mbalimbali. Hata hivyo, sasa inaonekana ukurasa huo umeanza kufungwa.
HUYU HAPA PAULA
Akizungumza na Mwanaspoti, Paula amesema hakuna sababu ya watu kuendelea kuwekeana mabifu kutokana na mambo ambayo tayari yamepita na wakati umeendelea.
Kwa mtazamo wake, maisha hayapaswi kusimama kwa sababu ya migogoro ya zamani, hasa pale ambapo wahusika wameendelea kukua na kubadilika.
Kauli ya Paula imekuja baada ya yeye na Fahyma kuanza kuonekana katika mazingira ambayo yanaonyesha kuwa tofauti zao za zamani hazina tena nafasi kubwa kama ilivyokuwa miaka iliyopita.
FAHYMA NAYE AFICHUA
Kwa upande wake, Fahyma ameliambia Mwanaspoti kuwa sababu kubwa ya kuweka yaliyopita pembeni ni kwamba sasa wote wamekuwa watu wazima na wamefikia hatua ya maisha ambayo wanapaswa kuangalia mambo yenye umuhimu zaidi.
“Kwa sasa tumeshakuwa watu wazima, haina haja ya kuwa na kinyongo na vitu, muda uliopo ni kutafuta pesa,” amesema Fahyma.
Kauli hiyo inaweka wazi kwamba kwa Fahyma, kuendelea kubeba hasira za miaka iliyopita hakutawasaidia katika maisha yao ya sasa.
NANDY AWAWEKA PAMOJA
Hatua hiyo pia imekuja baada ya wawili hao hivi karibuni kuonekana wakiwa pamoja na mwanamuziki Nandy, ambaye amekuwa na ukaribu na Fahyma.
Kuonekana kwao pamoja kulizua mjadala mitandaoni kwa sababu kwa miaka mingi walikuwa wamehusishwa na ushindani uliotokana na historia ya Rayvanny.
Lakini sasa, badala ya kuendeleza tofauti hizo, wanaonekana kuchagua kukaa pamoja na kuendelea na maisha.