Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nyuma ya hukumu ya P Diddy kuna mengi

P DIDY Pict

Muktasari:

  • Hukumu hiyo ilisomwa na Jaji Arun Subramanian katika Mahakama ya Shirikisho, jijini New York jana, Oktoba 3, 2025 baada ya kupatikana na hatia ya makosa mawili ya kusafirisha watu na kushiriki katika ukahaba.

MKONGWE wa Hiphop na mfanyabiashara maarufu wa Marekani, Sean Combs 'P Diddy' hatimaye amehukumiwa kifungo cha miezi 50 gerezani, faini ya Dola 500,000 na uangalizi wa miaka mitano baada ya kumaliza kifungo.

Hukumu hiyo ilisomwa na Jaji Arun Subramanian katika Mahakama ya Shirikisho, jijini New York jana, Oktoba 3, 2025 baada ya kupatikana na hatia ya makosa mawili ya kusafirisha watu na kushiriki katika ukahaba.

Hata hivyo, alipona kwenye makosa makubwa zaidi ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono (sex trafficking) na uhalifu wa kimtandao (racketeering conspiracy) ambayo kama angekutwa na hatia yangemweka kifungoni kwa muda mrefu.

Hukumu hiyo imehitimisha mjadala uliodumu kwa miezi kadhaa, huku mashabiki na familia wakisubiri kwa wasiwasi uamuzi wa mwisho.

Katika makosa hayo yaliyomponza Diddy, limo la kusafirisha wapenzi wake wawili wa zamani na kuwalazimisha kushiriki ngono na wanaume waliolipwa kwenye sherehe zilizoitwa 'freak offs'.

Diddy alikamatwa Septemba 16, 2024 katika Hoteli ya Park Hyatt, Manhattan, New York na kupelekwa moja kwa moja katika gereza la Metropolitan. Kesi yake ilianza kusikilizwa Mei 5,2025 huku watu mbalimbali wakitoa ushahidi akiwemo mpenzi wake wa muda mrefu Cassie Ventura, Jane, Mia, Kid Cudi, Bongolani, mama mzazi wa Cassie na wengineo.

Utakumbuka serikali ilitaka Combs ahukumiwe kifungo cha kati ya miezi 51 hadi 63 jela, lakini kwa upande wa utetezi ulipendekeza kifungo kifupi cha kati ya miezi 21 hadi 27.

P 04

KILICHOTOKEA MAHAKAMANI

Kwenye siku ya hukumu, ripoti zilitofautiana kuhusu hisia za P Diddy. Baadhi zilieleza mmiliki huyo wa lebo ya Bad Boy hakujutia baada ya kuhukumiwa, huku zingine zikieleza alipatwa na mshtuko.

BBC ilieleza msanii huyo alikaa kimya na bila hisia, macho yake yakielekezwa chini wakati jaji akisoma hukumu.

Gazeti la The Guardian la Uingereza kupitia michoro ya waandishi wa habari (sketches) ilimwonyesha akiwa ameshika uso kwa mikono, ishara kwamba alipatwa na mshtuko na huzuni.

Ripoti nyingine zilifafanua baada ya hukumu aliigeukia familia yake na kuanza kulia, akiongea kwa majuto makubwa.

“Mama nimekosea kama mwanao, samahani. Ulinilea kwa malezi bora lakini nimekuangusha.”

Aidha, alimwomba radhi aliyewahi kuwa mpenzi wake Cassie Ventura pamoja na waathirika wengine wa kashfa hizo akisema “Matendo yangu yalikuwa ya aibu, ya kusikitisha na ya kishenzi. Ninachukua jukumu lote kikamilifu na sitajitetea.”

P 01

WATOTO WAKE

Ndani ya mahakama hiyo, watoto wa Diddy walihudhuria na kati ya saba, sita walitoa ushuhuda wakimwomba jaji ampe baba yao fursa ya pili ya kurekebisha makosa yake.

Baada ya hukumu, mmoja wa watoto wake alinukuliwa akisema: “Tumepoteza baba yetu kwa muda, lakini tunajua ataweza kubadilika. Tunamwombea.”

P 03

HADI 2029

Kwa mujibu wa sheria za Marekani, kifungo cha miezi 50 kinamaanisha Diddy atatumikia takribani miaka minne na miezi miwili. Hata hivyo, amekuwa gerezani tangu Julai 2024, hivyo tayari ametumikia zaidi ya miezi tisa.

Kwa misingi hiyo, anatarajiwa kuachiliwa mapema mwaka 2029. Kwa kuwa makosa yake hayahesabiki kama ya vurugu (non-violent offenses), anaweza kuomba msamaha wa masharti baada ya kutumikia miezi tisa ya kifungo.

Kama angepatikana na hatia ya mashtaka ya sex trafficking na racketeering, angeweza kufungwa kifungo cha maisha kutokana na ukubwa wa makosa hayo.

P 02

MANENO YA JAJI

Jaji Subramanian aliyesimamia kesi hiyo, alisema mahakama imefanya kazi yake na hadhi na utajiri wa nyota huyo havikuwa kikwazo cha kupunguzia hukumu hiyo.

“Historia ya matendo mema haiwezi kufuta rekodi ya kesi hii. Uliwadhulumu wanawake hawa, ushahidi ni mkubwa. Dawa za kulevya zinaweza kuwa ziliathiri tabia zako, lakini mahakama lazima izingatie historia yako yote.”

“Mahakama haina uhakika ukiachiliwa hutarudia makosa haya tena. Hili ni fundisho kwa wengine. Kila aliyefanya kosa, uchunguzi ukimkuta na hatia, atapata anachostahili, haijalishi ni mtu wa hadhi gani.”

Kwa maneno hayo, Jaji Subramanian alisisitiza kifungo cha miezi 50 na faini ya Dola 500,000 ilikuwa adhabu inayostahili kwa msanii huyo aliyezoea maisha ya kifahari na utajiri.

MAWAKILI WA DIDDY

Licha ya hukumu hiyo, mawakili wa P Diddy hawakukubaliana na adhabu hiyo, wakiona msanii huyo alionewa na wako kwenye mchakato wa kukata rufaa.

Marc Agnifilo, mmoja wa mawakili, alisema wana sababu thabiti za kukata rufaa kwa kuwa jaji alitumia mara kadhaa neno kulazimisha au shinikizo la kisaikolojia wakati jopo la wazee wa mahakama lilimkuta hana hatia katika kipengele hicho.

Wakili mwingine, Brian Steele, alisema “Hukumu hii inatuma ujumbe mbaya. Combs amehukumiwa kwa matendo ambayo jopo la wazee wa mahakama halikumkuta nayo na hiyo ni kinyume na misingi ya haki za Marekani.”

Hata hivyo, pamoja na malalamiko ya mawakili wa mkongwe huyo, upande wa waendesha mashtaka ulisisitiza hukumu hiyo ilikuwa ndogo ikilinganishwa na uzito wa kesi, kwa sababu walikuwa wakiomba kifungo cha miaka 11.

ATHARI MUZIKI WA HIPHOP

Hukumu ya P Diddy ni pigo siyo tu kwake binafsi, bali tasnia ya muziki wa hip hop duniani. Diddy ambaye ni mwanzilishi wa Bad Boy Records amekuwa na ushawishi mkubwa katika muziki na biashara ya burudani, lakini sasa anakabiliwa na kipindi kigumu kwenye maisha yake.

Kwa kipindi kirefu, alitazamwa kama mmoja wa wafanyabiashara wakubwa wa muziki na mtayarishaji mashuhuri, aliyewahi kushinda tuzo nyingi ikiwemo Grammy Awards mara tatu, mwaka 2022 alipokea tuzo ya Lifetime Achievement Award kwenye tuzo za BET Awards kama heshima kwa mchango wake mkubwa katika muziki na utamaduni, pamoja na zingine nyingi.

Lakini sasa jina lake limeingia doa kubwa kwenye muziki huo baada ya kukutwa na hatia hizo, ambazo si picha nzuri kwa jamii inayomzunguka.

Hukumu ya miezi 50 kwa P Diddy imezua mjadala mkubwa upande mmoja wanaona kuwa amepewa adhabu ndogo kwa makosa yaliyothibitishwa, na upande mwingine wanaamini kuwa ni fursa ya pili kwake kubadilika.

Wakati huo huo, taswira yake katika macho ya jamii na mashabiki imepata doa kubwa ambalo huenda lisifutike hata baada ya kifungo chake kumalizika.

Swali linalobaki je, Diddy ataweza kurudi tena kwenye chati za muziki na kurejesha heshima yake au historia hiyo itamfunga kabisa?