Hatma ya P Diddy kujulikana leo
Muktasari:
- Kesi yake imekuwa gumzo kubwa duniani, ikihusisha tuhuma za ukahaba, usafirishaji wa watu na unyanyasaji wa kijinsia ambao umemuweka kwenye gereza la Metropolitan Detention Center (MDC) kwa mwaka sasa.
MACHO na masikio ya ulimwengu wa burudani yapo mjini Brooklyn, Marekani, ambako nyota wa muziki wa hip hop na mfanyabiashara mashuhuri Sean Combs ‘P Diddy’ anatarajiwa kusomewa hukumu yake.
Kesi yake imekuwa gumzo kubwa duniani, ikihusisha tuhuma za ukahaba, usafirishaji wa watu na unyanyasaji wa kijinsia ambao umemuweka kwenye gereza la Metropolitan Detention Center (MDC) kwa mwaka sasa.
Utakumbuka Diddy anakabiliwa na mashitaka ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono, njama za kihalifu, unyanyasaji wa kingono na usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ukahaba, lakini alikana mashitaka yote.
Wakati anakana mashitaka hayo, jopo la majaji lililokaa Julai 2025 lilimkuta na hatia kwenye makosa mawili ya kusafirisha mtu kwa madhumuni ya kushiriki ukahaba. Baadhi ya mashabiki wake walishangaa, huku wengine wakiona ni ushindi wa haki kwa waathirika.
Leo ndio hukumu yenyewe, na Mwanaspoti limekuchambulia kesi yake ilipoanzia na namna waendesha mashtaka wanavyosema, sambamba na upande wa mawakili wake wanaotetea asipewe adhabu kubwa baada ya kukaa gerezani kwa mwaka mmoja sasa.
HISTORIA YA KESI
P Diddy ni mmoja wa mastaa wakubwa zaidi katika historia ya muziki wa hip hop. Alijijengea jina kupitia lebo yake Bad Boy Records, akavuna utajiri kupitia biashara za mavazi, vinywaji na usambazaji wa muziki — miradi ambayo ilimfanya kutajwa kwenye tovuti mbalimbali kama miongoni mwa wasanii wenye utajiri mkubwa duniani.
Septemba 2024 alikamatwa na kushtakiwa na serikali ya Marekani kwa mashitaka kadhaa mazito yakiwamo mauaji ya pamoja ya kihalifu (racketeering conspiracy), usafirishaji wa kingono kwa nguvu na udanganyifu, pamoja na kusafirisha mtu kwa lengo la kushiriki ukahaba.
Baada ya kesi ya muda mrefu iliyojaa ushahidi wa video, ushuhuda wa waathirika na utetezi mkali kutoka kwa mawakili wake, majaji walimkuta na hatia kwenye makosa mawili ya kusafirisha mtu kwa ukahaba.
WAENDESHA MASHTAKA
Mashahidi wa upande wa mashtaka ni pamoja na Cassandra 'Cassie' Ventura, mpenzi wa zamani wa P Diddy na pia akiwa shahidi mkuu wa kesi. Ventura alieleza kuwa aliishi kwenye uhusiano wa zaidi ya miaka 10 uliokuwa na unyanyasaji wa kimwili na kisaikolojia, akilazimishwa kuhudhuria sherehe za ngono na hata kuburuzwa kupitia vitisho na fedha.
Wajumbe wa mahakama walionyeshwa pia video ya usalama ya mwaka 2016 ikimuonyesha P Diddy akimpiga Ventura kwenye korido ya hoteli. Mwanadada huyo alisema hadi sasa anaendelea kuathirika kisaikolojia na kuishi kwa hofu ya usalama wake na wa familia yake.
Hivyo waendesha mashtaka wa mahakama hiyo wametoa msimamo mkali kuwa msanii huyo anapaswa kupewa kifungo cha miaka 11 jela.
Katika barua waliyoandika kwa Jaji Arun Subramanian walisema:
“Hili sio kosa dogo, ni uhalifu uliofanywa kwa makusudi na kwa kutumia nguvu ya kifedha na kijamii. Mwathirika alidhuriwa na jamii inahitaji kuona mfano kwamba mtu yeyote, hata akiwa staa mkubwa, yuko chini ya sheria.”
Kwa mujibu wa sheria za Marekani, kosa la kusafirisha mtu kwa lengo la kushiriki ukahaba linaweza kubeba kifungo cha kati ya miaka 10 hadi 20, kutegemeana na mazingira.
MAWAKILI WA P DIDDY
Wakili mkuu wa msanii huyo, Marc Agnifilo, alisema adhabu iliyoainishwa na waendesha mashtaka si sahihi na anapaswa kuachiwa huru baada ya kukaa gerezani kwa takribani mwaka mmoja.
Mteja wetu si hatari kwa jamii, ameshapoteza kila kitu -- heshima, biashara, marafiki na hadhi yake ya kijamii. Hii peke yake ni adhabu kubwa kuliko kifungo cha ziada. Kumweka ndani zaidi hakutaleta maana, alisema Agnifilo.
MIA
Wakati ikisubiriwa hukumu hiyo, kuna mjadala umeibuka kuhusu msaidizi wa zamani wa P Diddy, maarufu kama Mia, kutoa ushahidi ingawa si miongoni mwa waathirika kwenye kesi ya staa huyo.
Waendesha mashtaka wanasisitiza kwamba ingawa Mia si mwathirika wa kosa lililothibitishwa kisheria, lakini ushuhuda wake leo unaweza kudhihirisha tabia ya ukatili na manyanyaso ya Diddy kazini.
Jaji Subramanian ana kibarua cha kuamua iwapo atampa nafasi Mia kuthibitisha madai yake au ataachana na suala hilo na kumaliza kesi hiyo.
ATHARI KWA MUZIKI WAKE
Ni wazi kama P Diddy atawekwa rumande muda mrefu, basi baadhi ya biashara zake na muziki wake utakuwa hatarini inaweza pia kuwa mwisho wa umaarufu na utajiri wake kwani hadi sasa baadhi ya kampuni zilizokuwa zikifanya kazi naye zimejiondoa kufuatia kesi hiyo.
Mchambuzi mmoja wa muziki aliandika kwenye ukurasa wa X: “Kama atahukumiwa miaka 11 au zaidi, hiuu ndiyo utakuwa mwisho wa hadithi ya Diddy katika muziki. Soko la muziki halitaki msanii mwenye doa kubwa.”
Yote kwa yote Ijumaa hii mahakama ya shirikisho mjini Brooklyn itakuwa hitimisho la habari ya msanii huyo. Hukumu hiyo itabainisha iwapo atakabiliana na zaidi ya muongo mmoja gerezani au atapata nafuu ya kutoka huru baada ya mwaka mmoja jela.
Kwa waathirika, hukumu hiyo itakuwa kipimo cha iwapo sauti zao zinathaminiwa. Kwa tasnia ya muziki, hukumu hiyo itafunga au kufungua ukurasa mpya juu ya uwajibikaji wa mastaa. Na kwa jamii pana, hukumu hii itabaki kama kumbukumbu ya jinsi sheria inavyoshughulikia kesi za mastaa wakubwa.