Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miaka 28 ya Mariah Carey kuvuna Sh5.8 bilioni kupitia wimbo ‘All I Want for Christmas is You’

Muktasari:

  • Ikiwa ni miaka 28 tangu kuachiwa kwake, mwimbaji wa Marekani, Mariah Carey anaendelea kuvuna mamilioni ya fedha kutokana na wimbo wake maarufu, ‘All I Want for Christmas is You’ ambao kila mwishoni mwa mwaka kuelekea Krismasi hujichukulia tena umaarufu duniani kote.

Ikiwa ni miaka 28 tangu kuachiwa kwake, mwimbaji wa Marekani, Mariah Carey anaendelea kuvuna mamilioni ya fedha kutokana na wimbo wake maarufu, ‘All I Want for Christmas is You’ ambao kila mwishoni mwa mwaka kuelekea Krismasi hujichukulia tena umaarufu duniani kote.

Wimbo huu ulirekodiwa Agosti 1994 huko New York na kuwekwa katika albamu yake ya nne na ya kwanza ya sikukuu, Merry Christmas (1994). Uliandikwa na kutayarishwa na Carey na Walter Afanasieff, ulitolewa kama wimbo wa kwanza katika albamu hiyo iliyotoka rasmi Oktoba 29, 1994.

Kwa mujibu wa ripoti ya Economist, kila mwaka humuingizia Carey fedha za mirabaha Dola2.5 milioni, wastani wa Sh5.8 bilioni, na tangu kutoka kwake umemuingizia Dola72 milioni, wastani wa Sh168.0 bilioni. Unashika nafasi ya 11 kati nyimbo zilizouza kwa muda wote, ukiwa umetanguliwa na ngoma, ‘My Heart Will Go On’ yake Celine Dion.

Billboard inautaja kuwa wimbo namba moja kwenye orodha yao ya nyimbo 100 bora za sikukuu kwa wakati wote. Mwaka jana uliingia kwenye chati za Billboard Holiday Hot 100 na kushika nafasi ya kwanza ukiwa umesikilizwa zaidi ya mara milioni 37.6 kwa Marekani pekee.

‘All I Want for Christmas is You’, ni wimbo wenye mapenzi ya hali ya juu, unachangamshwa na sauti za kengele na ulichochewa na sauti za kusisimua za Phil Spector, ambaye alitengeneza albamu maarufu ya Krismasi, ‘A Christmas Gift for You’ (1963).

“Mapenzi yanayoendelea kwa wimbo wangu hayaachi kunishangaza na kujaza moyo wangu na hisia nyingi za furaha, inanifurahisha sana kwamba wimbo huu umevuka enzi tofauti za tasnia ya muziki, nina bahati sana kuwa na mashabiki wengi duniani,” alisema Carey.

Kwa makadirio umeuza nakala zaidi ya milioni 16 duniani kote, na ni wimbo wa sikukuu wa msanii wa kike unaouza zaidi duniani.

Umefanyiwa video kadhaa, ile ya kwanza inaonyesha mtindo wa maisha wa Carey, mbwa wake na familia yake wakati wa msimu wa likizo, amevalia suti ya Santa akicheza kando ya mlima wenye theluji. Mume wake wa wakati huo, Tommy Mottola, alicheza kama Santa Claus, akimletea Carey zawadi na kuondoka.

Kufuatia mafanikio ya albamu yake, Music Box (1993), Carey na Lebo yake, Columbia Records na aliyekuwa mumewe, Tommy Mottola, Mkuu wa Columbia Sony Music Entertainment, walianza kupanga miradi mikubwa, ndipo likaja wazo la kufanya albamu ya Krismasi ila wakawa na wasiwasi kama itafanya vizuri.

Walter Afanasieff aliyeshiriki kuandika wimbo huo aliiambia Billboard kuwa hapo zamani, hakukuwa na wasanii wengi wenye albamu za Krismasi, hivyo wakaamua kuandika wimbo kwa dakika 15 hivi na Carey alikuwa na msimamo wa ajabu.

Katika mahojiano mengine na Business Insider mwaka 2013, Afanasieff alibainisha kuwa anashangazwa jinsi wimbo huo ulivyokuwa na mafanikio makubwa ya kibiashara.

“Sio wimbo wa kidini,” anasema Profesa msaidizi wa muziki kutoka Chuo Kikuu cha Northeastern, Andrew Mall katika mahojiano na Time.

“Anazungumza juu ya Krismasi, lakini hakuna imani ya kidini. Hakika ni wimbo wa mapenzi, yeyote anaweza kukariri maneno hayo, hivyo mtu yeyote anaweza kujiweka katika hali hiyo ya kuhitaji mtu wa kumpenda kwenye likizo. Ni wimbo wa mapenzi wa kiulimwengu na sio wimbo wa kidini wa Krismasi,” alisema Mall.

Carey akihojiwa na Good Morning America mwaka 2015 alisema upendo wake kwa Krismasi pamoja na talanta yake ya uimbaji ndivyo vimezaa matunda hayo.

“Mimi ni mtu wa sherehe sana na napenda likizo, nimeimba nyimbo za Krismasi tangu nilipokuwa msichana mdogo,” alisema Carey.

Tayari Carey ameandika kitabu chake, ‘The Christmas Princess’ kama sehemu ya kufurahia mafanikio ya wimbo huo, ni hadithi ya sikukuu isiyoweza kusahaulika iliyosimuliwa na Mariah Carey mwenyewe pamoja na Michaela Angela Davis.

Katika hadithi hiyo inayoangazia likizo ya familia, Carey amemtambulisha ‘Little Mariah’, binti mdogo ambaye hana mengi na hataki mengi, lakini kuna jambo moja tu analotamani; msimu wa likizo wenye amani na furaha.

“Ni kitabu kifupi, lakini kina maana zaidi,” alisema Carey wakati akizungumza na USA Today.

Alisema kuishi katika nyumba yake wakati wa Krismasi, unapaswa kujua kuna sheria ameziweka ambazo yeyote anapaswa kuzizingatia.

“Sijali ni nani hata watoto, ikiwa nina wageni au chochote, hakuna mtu anayeruhusiwa kucheza au kutazama kitu chochote isipokuwa kitu kinachohusiana na Krismasi. Nikiamka usiku na kuingia sebuleni na kukuta muziki hauchezwi na taa hazijawashwa, siwezi kumudu hali hiyo,” alisema Carey.

Hata hivyo, hivi karibuni Mariah Carey ameshtakiwa kwa madai ya ukiukaji wa hakimiliki inayohusiana na wimbo huo na Andy Stone, mtu ambaye aliandika wimbo mwingine wa Krismasi wenye jina sawa na hilo.

Stone, ambaye anatumia jina Vince Vance katika muziki, anadai kuwa wimbo wa Carey unatokana na kazi yake iliyoandikwa na kurekodiwa mwaka 1989.

Wakili wake aliwataarifu washtakiwa Desemba 2021, lakini hawakuweza kufikia makubaliano yoyote kuhusu kuendelea kuuza wimbo wa Carey wa mwaka 1994.

Mwandishi mwenza na Carey katika wimbo huo, Walter Afanasieff naye ametajwa katika kesi hiyo pamoja na Sony Music Entertainment, kampuni tanzu ya Sony Corporation of America.

Lakini Desemba 2020 Carey akiongea na The Times, alisema wazo la kutunga wimbo huo lilianza baada ya kukaa katika piano na kuicheza mara kadhaa, lakini hawezi kuweka wazi wimbo huo ulifikaje kwake.

“Nilikuwa nimekaa tu, nikipata wimbo huu, katika nyumba yenye giza na mti wa Krismasi, siwezi kukuambia jinsi wimbo huo ulivyokuja kwangu. Kwa kweli naiona kama zawadi,” alisema Carey.

Desemba 2021 All I Want for Christmas is You, uliandika rekodi ya kuwa wimbo wa kwanza na wa pekee wa sikukuu kuchukua tuzo ya Almasi zinazotolewa na RIAA baada ya kufikia mauzo ya nakala zaidi ya milioni 10 nchini Marekani.