May Day yamteka Makonda
Muktasari:
- Wimbo wa “May Day” ulikuwa miongoni mwa nyimbo zilizopokewa vizuri na mashabiki waliofurahia zaidi wakati ulipopigwa. Onyesho hilo lilionyesha kwa mara nyingine mvuto wa muziki wa Fally kwa mashabiki wa rika na makundi mbalimbali.
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, alikuwa miongoni mwa viongozi waliohudhuria shoo ya mwanamuziki nyota kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Fally Ipupa, iliyofanyika usiku wa kuamkia leo Novemba 29, 2026, katika viwanja vya Lugalo Golf Course, Kawe, Dar es Salaam.
Mwanaspoti lilimshuhudia Makonda akifurahia burudani iliyokuwa ikitolewa na Fally, akichezesha kichwa kufuatisha midundo ya nyimbo zake huku akipiga makofi kuonyesha namna alivyokuwa akiupokea muziki huo.
Hata hivyo, wimbo ulioonekana kumvutia zaidi ni “May Day” kwani ulipopigwa, Makonda alionekana kuufurahia kwa namna ya kipekee, akifuatisha midundo yake kwa kuchezesha kichwa na kupiga makofi.
Mbali na Makonda, viongozi wengine waliohudhuria shoo hiyo ni Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye, pamoja na Mbunge wa Viti Maalum na Mwenyekiti wa Bendi ya Twanga Pepeta, Asha Baraka.
Uwepo wa viongozi hao ulikuwa sehemu ya matukio yaliyojiri katika usiku huo ambao uliwakutanisha mashabiki wa muziki, watu maarufu na wadau mbalimbali wa burudani katika viwanja vya Lugalo.
Fally alitumia takribani saa tatu jukwaani bila kushuka, akiimba live na kutoa burudani kwa nyimbo mbalimbali zikiwamo “May Day”, “Elo Ko Oyo”, “Afsana”, “Bakanja” na “Associe”.
Wimbo wa “May Day” ulikuwa miongoni mwa nyimbo zilizopokewa vizuri na mashabiki waliofurahia zaidi wakati ulipopigwa. Onyesho hilo lilionyesha kwa mara nyingine mvuto wa muziki wa Fally kwa mashabiki wa rika na makundi mbalimbali.