CHRISEAN ROCK: Staa maarufu anayezongwa na machungu mapenzini
Muktasari:
- Chrisean alizaliwa Machi 14, 2000. Kabla ya kuanza kuimba nyimbo za injili, alianza na muziki wa Hip Hop, lakini maisha yake ya kimahusiano pia yamekuwa yakivutia hisia za mashabiki wake.
KWA watumiaji wa mitandao ya kijamii, jina la mwanamuziki Chrisean Eugenia Malone, maarufu kama Chrisean Rock, raia wa Marekani, si geni kutokana na ushawishi mkubwa alionao kwa mashabiki, unaotokana na aina ya maisha anayoishi.
Chrisean alizaliwa Machi 14, 2000. Kabla ya kuanza kuimba nyimbo za injili, alianza na muziki wa Hip Hop, lakini maisha yake ya kimahusiano pia yamekuwa yakivutia hisia za mashabiki wake.
KAZI YA MUZIKI
Chrisean alianza safari yake ya muziki mwaka 2020 alipotoa wimbo wake wa kwanza ulioitwa Lonely, akimshirikisha rapper Blueface. Baadaye alitoa nyimbo nyingine, zikiwemo Vibe (2021) na Rainy Days (2022).
Mwaka 2023, alifanya kazi na rapper Lil Mabu kwenye wimbo Mr. Take Ya Bitch, ambao ulimsaidia kupata nafasi katika chati ya Billboard Hot 100. Mwaka 2025, alifanya mabadiliko ya kimuziki kwa kuingia kwenye muziki wa injili kupitia wimbo Yahweh.
MAHUSIANO
Moja ya mambo yaliyomfanya Chrisean kuwa gumzo ni uhusiano wake na rapper Blueface. Wawili hao walikuwa na uhusiano uliojaa migogoro, malumbano na matukio mbalimbali yaliyokuwa yakisambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Uhusiano wao ulivutia hisia za mashabiki kiasi cha kupewa kipindi chao cha televisheni kilichoitwa Blueface & Chrisean: Crazy in Love. Hata hivyo, uhusiano huo haukuwa na utulivu na baadaye walitengana, huku wakiendelea kuhusishwa na mijadala mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii.
Miongoni mwa matukio yaliyowahi kuwashangaza wengi ni lile lililotokea wakiwa pembezoni mwa bwawa la kuogelea, ambapo Blueface alionekana akimpiga teke Chrisean na kumsukuma. Tukio hilo lilikosolewa na mashabiki wao, ambao waliliona kuwa ishara mbaya ya mwanaume huyo kutokuwa na upendo wa kweli kwake.
Mwaka 2026, Chrisean alikiri kumsamehe Blueface kutokana na kujikita katika kuimba nyimbo za injili na kueleza kuwa bado anampenda. Hata hivyo, wawili hao hawajarudiana, ingawa mashabiki wao wanaamini huenda ni suala la muda tu kabla ya kurejeana, wakiona kuwa kuachana na kurudiana kumekuwa jambo la kawaida katika uhusiano wao.
UMAARUFU
Chrisean hakupata umaarufu kupitia muziki pekee. Mwaka 2020, alishiriki katika kipindi cha Blue Girls Club, kilichohusishwa na Blueface, jambo lililomfungulia milango ya kujulikana zaidi. Baadaye alijiunga na kipindi cha Baddies kupitia mtandao wa Zeus Network. Tabia yake ya kujieleza bila kuficha hisia, migogoro iliyokuwa ikitokea kwenye vipindi hivyo na matukio ya maisha yake ya kila siku vilimfanya kuwa gumzo miongoni mwa vijana wanaofuatilia burudani za Marekani.
Mfano wa matukio hayo ni lile la Julai 2023, wakati akiwa kwenye kipindi cha Crazy in Love, Chrisean alionekana akilia kwa uchungu mbele ya dada yake mkubwa, Tessa, kutokana na msongo wa mawazo aliokuwa akipitia wakati wa ujauzito wake.
Katika tukio hilo, alieleza kuchoshwa na maisha ya umaarufu pamoja na changamoto alizokuwa akipitia katika uhusiano wake na Blueface.
Akiwa analia, alisikika akisema kuwa hataki tena kuwa maarufu na kwamba alihitaji faraja kutoka kwa dada yake kutokana na hali ngumu aliyokuwa akiipitia. Tukio hilo liligusa hisia za watazamaji kwa sababu lilionyesha kuwa nyuma ya umaarufu wake kulikuwa na changamoto za kihisia ambazo hazikuonekana katika picha na video zake zilizokuwa zikisambaa mitandaoni.
MWONEKANO, TATTOO
Tofauti na mastaa wengi wanaojulikana kwa mitindo yao ya mavazi, Chrisean amekuwa akivutia macho pia kutokana na michoro mingi ya tattoo aliyonayo mwilini na usoni.
Moja ya vitu vilivyozua mjadala ni tattoo ya sura ya Blueface aliyowahi kuwa nayo usoni. Mwonekano huo umekuwa sehemu ya utambulisho wake na kumfanya awe rahisi kutambulika katika picha na video zinazozunguka mitandaoni.
MAISHA YA MAMA
Septemba 3, 2023, Chrisean alijifungua mtoto wa kiume aliyempa jina la Chrisean Jesus Malone Jr., ambaye alizaa na Blueface.
Kuzaliwa kwa mtoto huyo kuliongeza mijadala kuhusu maisha yake binafsi, hasa kutokana na uhusiano wake na baba wa mtoto. Hata hivyo, baada ya kupitia changamoto mbalimbali, Chrisean alianza kuzungumzia zaidi malezi ya mtoto wake na umuhimu wa kubadilisha mwelekeo wa maisha yake.
MUZIKI WA INJILI
Baada ya kupitia changamoto mbalimbali maishani, Chrisean alianza kuonyesha upande mwingine wa maisha yake kwa kujikita zaidi katika imani ya Kikristo.
Mwaka 2025, aliutambulisha kwa mara ya kwanza wimbo wake wa injili Yahweh katika Kanisa la Faith City Central, Maryland, Marekani, akiwa na waimbaji Tim Bowman Jr. na Arissa Divyne.Hatua hiyo ilivuta hisia za mashabiki kwa sababu wengi walikuwa wamemzoea kupitia muziki wa Hip Hop, vipindi vya burudani na migogoro ya maisha yake binafsi. Sasa amekuwa akionyesha nia ya kutumia muziki kueleza safari yake ya kiimani na mabadiliko anayoyapitia.