Masha Love amwaga ya moyoni kuhusu Mose Iyobo
Muktasari:
- Mose amejijengea jina katika tasnia ya burudani kupitia kazi yake ya kucheza dansi na Diamond Platnumz, huku pia akihusika na ufundishaji wa dansi. Kwa Masha, uwezo na mchango wa Mose haupaswi kupimwa kwa kumuona jukwaani akicheza pekee, bali kutambuliwa kama kazi yenye thamani na inayostahili heshima.
MSANII wa Bongo Movies na Video Vixen, Masha Love, amefunguka kuhusu mchumba wake, Mose Iyobo, akieleza namna anavyomthamini na kukerwa na baadhi ya watu wanaomchukulia kama dansa wa kawaida bila kutambua ukubwa wa mchango wake katika tasnia ya burudani.
Masha amesema amekuwa akifuatilia mijadala mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii na kubaini kuwa baadhi ya watu wanamzungumzia Mose kwa namna isiyomfurahisha. Anasema kinachomshangaza ni kuona watu wakimtazama akicheza muziki na kusahau kuwa dansi ni kazi inayohitaji kipaji, ubunifu na juhudi.
Akifafanua msimamo wake, Masha amesema anamwona Mose akiwa na nafasi kubwa zaidi katika tasnia hiyo, tofauti na baadhi ya watu wanaomdharau kwa sababu ya kazi yake ya kucheza muziki.
“Waache kumchukulia poa Moze wangu. Mimi namuona kama mkurugenzi fulani hivi, wao wakiona mtu anacheza muziki hawajui kama ni kazi, hawathamini na kuonyesha dharau tu mitandaoni,” amesema Masha.
Kauli hiyo inarejesha kumbukumbu za safari ya uhusiano wao, uliowekwa wazi Juni 2024 baada ya tetesi za kimapenzi kuhusishwa na wawili hao kusambaa mitandaoni. Wakati huo, Mose alikiri kuwa katika uhusiano na Masha, akieleza kuwa maneno ya watu waliokuwa wakimkosoa mwanamke huyo yasingebadili uamuzi wake wa kuwa naye.
Baada ya uhusiano huo kuwekwa wazi, Masha naye hakuficha hisia zake. Desemba 2024, akizungumza na Mwanaspoti, amesema anampenda Mose na alikuwa na imani na uhusiano wao, akieleza kuwa hakuona uwezekano wa wao kuachana.
Machi 2025, Masha alizungumzia mabadiliko ya mtazamo wake kuhusu mahusiano, akisema amekomaa kimawazo na hataki tena kuwa katika uhusiano usio na mwelekeo. Agosti mwaka huo, alifunguka kuhusu matarajio yake ya kufunga ndoa na Mose, akieleza kuwa walikuwa wameanza maandalizi madogo madogo.
Mose amejijengea jina katika tasnia ya burudani kupitia kazi yake ya kucheza dansi na Diamond Platnumz, huku pia akihusika na ufundishaji wa dansi. Kwa Masha, uwezo na mchango wa Mose haupaswi kupimwa kwa kumuona jukwaani akicheza pekee, bali kutambuliwa kama kazi yenye thamani na inayostahili heshima.