Iyobo ashindwa kuvumilia, afunguka ishu ya kulelewa
Muktasari:
- Iyobo ambaye amekuwa na lebo hiyo kwa muda mrefu amesema hajawahi kutoka kwenye lebo hiyo na hawezi kufanya hivyo kwani bosi wake huyo ni mtu poa kwake.
Dansa maarufu kutoka WCB, Mose Iyobo amesema bado anaendelea kufanya kazi na bosi wake Diamond Platnumz na WCB na yanayosemwa juu yake na lebo hiyo yapuuzwe, huku akifichua kazi hiyo ndo inampa hela na si kulelewa.
Iyobo ambaye amekuwa na lebo hiyo kwa muda mrefu amesema hajawahi kutoka kwenye lebo hiyo na hawezi kufanya hivyo kwani bosi wake huyo ni mtu poa kwake.
“Siwezi Kutoka WCB ng'oo, sasa naachaje kufanya kazi na Diamond wakati ni mtu poa sana na ni bosi mzuri kufanya naye kazi, kama hamjui tu Diamond ni mtu fulani ambaye yupo poa sana, hayo maneno hata mimi nimeyasikia lakini hayana ukweli wowote," amesema Iyobo.
Kuhusu kulelewa na Masha Love kama inavyovumishwa mitandaoni, amesema; "Nalelewaje wakati nafanya kazi kwa Diamond? Pia ni mwalimu nafundisha watu kudansi kitu ambacho napata pesa kupita wao, wananilipa na mimi nawapa ufundi na hata nikiwa na shida ya pesa nikimwambia Diamond ananisaidia kwa haraka sana," amesema.
Iyobo na Masha Love wapo katika mahaba mazito kwa muda mrefu, tangu dansa huyo alipotemana na mama mtoto wake, Aunty Ezekiel.
Na miezi michache iliyopita, Aunty Ezekiel baada ya kupishana na Iyobo kuhusu mtoto wao na wakawa wanatupiana maneno kupitia akaunti zao za Instagram, Aunty alitoa madai ya kuwa Iyobo analelewa na Masha Love na sasa amehamia nyumbani kwake kuishi pamoja kutokana na kuwa na hali ngumu ya pesa.