Kuku, mbuzi wamteka Snare
Muktasari:
- Huku akiendelea na safari yake ya muziki, Snare anaonyesha kuwa maisha yake yana mengi zaidi ya yale ambayo mashabiki huyashuhudia jukwaani, huku ufugaji na kilimo vikiendelea kuwa miongoni mwa mambo yanayompa furaha nje ya sanaa.
UNAPOTAJA jina la msanii Uncle Snare, wengi huenda wakamfikiria kupitia muziki, studio na majukwaa ya burudani. Hata hivyo, nyuma ya maisha yake ya kisanii kuna mambo mengine anayoyapenda, yakiwemo ufugaji na kilimo.
Snare anasema amekuwa akivutiwa na shughuli hizo tangu akiwa mdogo, akitaja kuku, mbuzi, ng’ombe, kanga, bata na sungura kuwa miongoni mwa mifugo anayopenda. Mbali na ufugaji, pia anafurahia kulima mboga, zikiwemo nyanya na pilipili.
“Tangu nikiwa mdogo tunafuga mbuzi, kuku na ng’ombe. Kwa hiyo napenda maisha ya kuwa na mifugo, bustani na kulima mboga kama nyanya na pilipili. Hiyo ndiyo lifestyle ninayoipenda,” anasema Snare.
Kauli yake inaonyesha kuwa mapenzi yake kwa ufugaji na kilimo yamejengeka tangu utotoni, badala ya kuwa jambo aliloanza kulipenda baada ya kujipatia umaarufu kupitia muziki.
Kwa Snare, maisha ya msanii hayaishii kwenye kurekodi nyimbo na kutumbuiza jukwaani, kwani shughuli za ufugaji na kilimo pia ni sehemu ya mambo yanayompa furaha nje ya sanaa.
SOKO LINAVYOONGOZA MUZIKI WAKE
Licha ya kuvutiwa na mifugo na kilimo, muziki bado ni sehemu muhimu ya maisha yake. Snare anasema katika kutengeneza kazi zake, huzingatia mahitaji ya soko pamoja na mapenzi yake na uwezo alionao katika aina mbalimbali za muziki.
Anasema hapendi kujifungia kwenye mtindo mmoja, kwani mabadiliko ya mahitaji ya wasikilizaji yanaweza kumlazimu kufanya kazi zenye mitindo tofauti. Hata hivyo, anasisitiza kuwa hufuata pia kile anachokipenda na anachoweza kukifanya vizuri.
“Natengeneza muziki kutokana na jinsi ninavyoona soko linahitaji, lakini pia kile ninachokipenda na ninachokiweza zaidi. Itategemea na soko, lakini tunafanya muziki wa aina yoyote,” anasema.
Kwa mtazamo huo, Snare anaeleza umuhimu wa kusawazisha mahitaji ya soko na uwezo binafsi wa msanii katika kutengeneza kazi zinazoweza kuwafikia wasikilizaji.
Kwake, ubora wa wimbo hauamuliwi na aina ya midundo iliyotumika pekee, bali pia na ujumbe unaowasilishwa na namna unavyomfikia msikilizaji.
Huku akiendelea na safari yake ya muziki, Snare anaonyesha kuwa maisha yake yana mengi zaidi ya yale ambayo mashabiki huyashuhudia jukwaani, huku ufugaji na kilimo vikiendelea kuwa miongoni mwa mambo yanayompa furaha nje ya sanaa.