Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kila ulipo unyayo wa Diamond, Zuchu anakanyaga

Ikiwa ni miaka mitatu tangu Zuchu kusainiwa WCB Wasafi, staa huyo wa Bongofleva anaendelea kupita njia za bosi wake, Diamond Platnumz kwa lengo la kuhakikisha muziki wake unakua na kufika mbali zaidi.

Zuchu ambaye ni msanii wa pili wa kike ndani ya WCB Wasafi baada ya Queen Darleen, amekuwa na mafanikio makubwa katika kipindi kifupi ukilinganisha na wasanii wote waliowahi kusainiwa katika lebo hiyo.

Ndiye msanii wa kwanza kutambulishwa na kuachia EP (I Am Zuchu) papo hapo, ameshashinda tuzo takriban 10 za ndani na kimataifa, amefanya kolabo na wasanii wakubwa na namba zake za mauzo katika majukwaa ya kidijitali zipo juu.

Hata hivyo, katika mafanikio hayo nyuma yake kuna uwepo wa Diamond, lakini kubwa zaidi ni kile kinachoonekana ni uwezo wa Zuchu kujiongeza yaani kupita njia zile alizopita Diamond hadi leo anatambulika kama miongoni mwa wasanii wakubwa Afrika.

Utakumbuka Diamond aliyetoka kimuziki mwaka 2009 ameshinda tuzo za kimataifa kama Channel O, MTV, Soundcity, Headies, Afrima, Afrimma, Kora, AEA, EAUSA, the HiPipo Music Awards n.k, ana lebo yake, WCB Wasafi na kadhalika.

Moja ya kolobo kali za Zuchu mwaka uliopita, Nani Remix akimshirikisha Innoss'B kutokea DR Congo katika video ya wimbo huo ameonekana mama yake mzazi Khadija Kopa.

Ikumbukwe Kopa ambaye ni Malkia wa muziki wa Taarab nchini Tanzania alianza kazi ya sanaa mwaka 1990 katika kikundi cha Culture Musical Club kilichopo Zanzibar.

Katika video hiyo Kopa amecheza kama mzazi ambaye anakwenda kumuozesha binti yake (Zuchu) katika famili ya kifalme, na mwishowe anavikwa taji la umalkia.

Kitendo cha Zuchu kufanya video na mama yake ni mwendelezo tu wa kile alichofanya Diamond mwaka 2015 ambapo mama yake mzazi, Sandra maarufu kama Mama Dangote alitokea kwenye video ya wimbo wake, Utanipenda?

Na katika video hiyo Mama Dangote alicheza uhusika wa maisha atakayoishi siku ambayo Diamond atakapofilisika kimuziki na kiuchumi, na aliyekuwa mpenzi wake na mzazi mwenziye, Zari The Bosslady alitokea pia.

Hakuna ubishi kuwa Zuchu anataka kufanikiwa kama Diamond au kurithishwa mafanikio hayo. Hiyo ni kwa sababu anaendelea kufanya kolabo na wasanii ambao Diamond tayari alishafanya nao awali.

Mfano ni Staa wa Nigeria, Adekunle Gold ambaye alishirikishwa na Diamond katika wimbo wake 'Sona' kutoka kwenye EP ya kwanza, First of All (FOA) iliyotoka Machi 2022 ikiwa na nyimbo 10.

Baadaye Zuchu akaja kumshirikisha Adekunle Gold katika wimbo wa Love uliotoka Septemba 2020 muda mfupi baada ya kufanya vizuri na mradi wake, 4:4:2 uliokuwa na nyimbo mbili, Fire na Jaro.

Zuchu haukuishia hapo. akahamia kwa Innoss'B ambaye ndiye amempa shavu katika wimbo Nani Remix. utakumbuka Innoss'B tayari alishafanya kazi na Diamond katika wimbo wa Yope Remix uliotoka Septemba 2019 na kufanya vizuri barani Afrika.

Kwa kifupi baada ya kuona Diamond kafanya remix na Innoss'B naye akafanya hivyo hivyo. Aanapita tu njia za Diamond kimtindo, kama haendi lakini ndio anaondoka hivyo na kuzidi kuvuna mashabiki wa kazi zake.

Utakumbuka Yope Remix ndio wimbo wa Diamond wenye mafanikio makubwa katika mtandao wa YouTube ambapo video yake imefikisha 'vews' zaidi ya milioni 223. Hii ndio video pekee ya muziki iliyotazamwa zaidi Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Katika mradi wake wa 4:4:2 uliotoka Julai 2022, Zuchu aliweka wimbo wa Fire ambao anadai alipanga kumshirikisha Diamond, lakini tayari alishamshirikisha katika nyimbo mbili awali ambazo ni Litawachoma na Cheche zilizotoka pamoja Novemba 2020.

Hata hivyo, tayari naye Diamond alishawahi kutoa wimbo unaoitwa 'Fire' Novemba 2017 akimshirikisha Tiwa Savage wa Nigeria ukiwa ni wimbo aliokuja kuujumuisha katika albamu yake ya tatu ya A Boy From Tandale (2018). Kwa kifupi Zuchu anapita hadi na majina ya ngoma za Diamond.

Zuchu aliamua kuupa mradi wake huo jina la 4:4:2 kutokana wimbo wake wa kwanza 'Fire' kuwa una herufu nne pia wa pili, 'Jaro' una herufi nne hivyo kutoka kwa pamoja zote mbili  kunakamilisha maana ya 4:4:2.

Ikumbukwe wakati Diamond akiwa ndiye msanii wa kiume wa Bongofleva anayeuza zaidi kwenye majukwaa ya kidijitali ya kutiririsha (streams) muziki, Zuchu ndiye msanii anayefanya hivyo upande wa wasanii wa kike.

Rekodi hiyo ya Zuchu ni ndani ya miaka mitatu tu tangu kutoka rasmi kimuziki baada ya mapambano ya muda mrefu bila mafanikio ikiwemo kushindwa kung'ara katika shindano la Karaoke Afrika, Tecno Tecno Own The Stage 2015 nchini Nigeria.