Khadija Kopa afichua siri za Zuchu
Muktasari:
- Kopa ambaye ni mkongwe wa muziki nchini akitamba katika Taarab, amesema mwanaye huyo ambaye ni mke wa Diamond Platnumz alipokuwa mdogo, ndoto yake ilikuwa kuwa mwanasheria, lakini yeye kama mama na mwanamuziki ambaye Zuchu anamchukulia kama 'role model' wake, alitamani kumuona binti yake akifuata njia zake.
MAMA wa msanii wa Bongo Fleva, Zuchu, Khadija Kopa amefichua mwanaye anaimba kutokana na kipaji alicho nacho pamoja na kurithi kutoka kwake, lakini alikuwa na ndoto nyingine tofauti na sanaa.
Kopa ambaye ni mkongwe wa muziki nchini akitamba katika Taarab, amesema mwanaye huyo ambaye ni mke wa Diamond Platnumz alipokuwa mdogo, ndoto yake ilikuwa kuwa mwanasheria, lakini yeye kama mama na mwanamuziki ambaye Zuchu anamchukulia kama 'role model' wake, alitamani kumuona binti yake akifuata njia zake.
Amesema pamoja na ndoto hiyo, alitamani afanye muziki na baada ya kutoka masomoni, alimpeleka kwa Babu Tale ili aanze safari ya muziki. Hata hivyo, alimshauri Zuchu aendelee kwanza na masomo kwa sababu wakati huo bado alikuwa mdogo.
"Ndoto ya mwanangu ilikuwa kuwa mwanasheria lakini nilitamani awe msanii kama mimi na imekuwa hivyo. Nilimpeleka kwa Babu Tale ili aanze lakini alimshauri amalize kwanza masomo," amesema Kopa na kuongeza; Zuchu ana kipaji cha kuandika nyimbo na baadhi ya wasanii wamewahi kunufaika na uwezo huo akiwamo Shaa ambaye aliandikiwa wimbo na mwanaye.