Mastaa wanavyonufaika Na watoto wao kibiashara
Muktasari:
- Wapo mastaa wanaonufaika kwa pamoja, kwa maana ya walio katika uhusiano iwe uchumba au ndoa na wengine wanatumika katika dili moja kutokana na ushawishi wao katika jamii.
MASTAA wengi duniai wanatengeneza pesa nyingi kutokana na kazi zao. Iwe ni sanaa, au michezo. Na zaidi ya pesa, majina yao yanakuwa makubwa na kufikia hatua ya kupewa dili za matangazo.
Wapo mastaa wanaonufaika kwa pamoja, kwa maana ya walio katika uhusiano iwe uchumba au ndoa na wengine wanatumika katika dili moja kutokana na ushawishi wao katika jamii.
Zaidi ya hapo, hata watoto wao wamekuwa wakiingia katika madili kutokana na umaarufu wa wazazi wao na wengine ni kuanzia pale tu wanapozaliwa wanaanza kupiga pesa.
Vyanzo vikuu vya madili hayo ni matangazo ya kibiashara kutoka kwa kampuni tofauti na ni kwa sababu ya umaarufu wa wazazi wao, kampuni zinaamini watoto hao watazifanya bidhaa zao kujitangaza zaidi.
Watoto kama Sandra, Rakeem, Naya, Latifa na Baby Ollie ni wa mastaa wakubwa nchini na sura zao tayari zimetambulika katika jamii huku kampuni mbalimbali zikiwapa dili ambazo kwa kiasi kikubwa zinawanufaisha wazazi wao.
Ni siku chache zimepita tangu Sandra, mtoto wa Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, na Zuhura Othman Soud ‘Zuchu’, kupata ubalozi wa moja ya kampuni hapa nchini. Hapa ndipo swali linapokuja; wazazi mastaa wananufaikaje watoto wao wanapoanza kupata dili?
JINA LA MTOTO, CHAPA YA FAMILIA
Kampuni inapomchagua mtoto wa staa kwenye kampeni, haivutii tu mtoto huyo, bali pia inapata nafasi ya kufikia hadhira inayomfuatilia mzazi wake. Kwa hiyo, mtoto anapoonekana kwenye tangazo, jina la familia linakuwa sehemu ya mvuto wa kampeni.
Hali hiyo inaweza kuwa na faida kwa mzazi, kwa sababu umaarufu wa mtoto unaweza kuongeza mwonekano wa familia nzima. Kwa mastaa wenye biashara zao, hali hiyo inaweza pia kusaidia kuendelea kujenga taswira ya familia yenye nguvu kwenye soko.
Kenaya William Lyimo, maarufu kama Naya, mtoto wa mastaa wakubwa nchini, Faustina Mfinanga, ‘Nandy’, na mume wake William Lyimo ‘Billnass’. Mtoto huyo alipata ubalozi wa mavazi ambao ulipunguza matumizi ya fedha, kwa sababu alikuwa akipatiwa nguo kama sehemu ya kazi yake katika kampuni ya nguo za watoto hapa nchini. Kutokana na majina ya wazazi wake, mtoto akawa anaingiza hela kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya umaarufu wake.
Pia wazazi ndio wasimamizi wa madili hayo, kuanzia mawasiliano na kampuni, ratiba za kazi, matumizi ya picha na video, pamoja na masuala mengine yanayohusu ushiriki wa mtoto kwenye kazi hiyo.
MITANDAO INAONGEZA THAMANI
Nguvu ya mitandao ya kijamii imeifanya hali hiyo kuwa kubwa zaidi.
Picha au video ya mtoto wa staa inaweza kupata uangalizi mkubwa kutokana na jina la wazazi wake. Kampuni inapoweka bidhaa yake kwenye maudhui yanayohusisha mtoto maarufu, inaweza kupata macho ya watu wengi ambao tayari wanafuatilia familia hiyo.
Hapo mzazi anaweza kunufaika kwa upande wa brand, kwa sababu jina lake linaendelea kuonekana na kuhusishwa na kampeni mbalimbali.
Kwa mastaa wanaofanya biashara nje ya muziki, hii inaweza kuwa nyongeza ya mwonekano wa familia yao katika soko la kibiashara.
Kama Rakeem amekuja na baraka kubwa kwa wazazi wake, alipata ubalozi wa kampuni nyingi huko Nigeria kwa sababu ya majina ya wazazi wake, Priscilla Ojo, ambaye ni mwanamitindo, na mumewe Juma Jux.
FAIDA KWA FAMILIA
Faida nyingine ni kuongezeka kwa thamani ya jina la familia na mtoto ambaye naye anaonekana, kampuni nyingine zinaweza kuvutiwa na hadhira hiyo hiyo. Hivyo, dili moja linaweza kusaidia kuongeza mwonekano wa familia kwenye mitandao na matukio ya kibiashara, ingawa hilo halimaanishi moja kwa moja kampuni nyingine itatoa mkataba.
Kwa mzazi, kinachoweza kuongezeka ni nguvu ya brand, huku mtoto naye akianza kujenga utambulisho wake.
SIYO FEDHA PEKEE
Watoto wanaweza pia kupata uzoefu wa mbele ya kamera, kujifunza namna ya kushiriki kwenye biashara na kuzoea mazingira ya kazi za matangazo kulingana na umri wao.
Latifa Nasib, mtoto Diamond na Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ alipata umaarufu na uzoefu tangu akiwa mtoto kama balozi wa bidhaa mbalimbali na sasa ana uzoefu hata wa kusimama mbele ya kamera.
Kwa wazazi mastaa, hii inaweza kuwa njia nyingine ya kuendeleza mwonekano wa familia bila kutegemea muziki au sanaa pekee.
Hata hivyo, umaarufu wa mtoto unahitaji usimamizi makini. Usalama, faragha, elimu na maslahi yake vinapaswa kubaki mbele kuliko thamani ya dili anazofanya.