Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Urafiki wa miaka 13 wa Davido na Diamond

DAVIDO Pict

Muktasari:

  • Davido na Chioma waliwasili Dar es Salaam Jumanne, Novemba 10, 2026, na kupokelewa na Diamond Platnumz pamoja na Zuchu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Ujio wa mwanamuziki nyota wa Nigeria, David Adeleke, maarufu Davido, nchini Tanzania akiwa ameambatana na mkewe, Chioma Adeleke, umeibua shauku kubwa miongoni mwa mashabiki wa muziki, huku mapokezi aliyoyapata kutoka kwa Diamond Platnumz na Zuchu yakifufua kumbukumbu za urafiki na ushirikiano wa kimuziki ulioanza miaka 13 iliyopita.

Davido na Chioma waliwasili Dar es Salaam Jumanne, Novemba 10, 2026, na kupokelewa na Diamond Platnumz pamoja na Zuchu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Mapokezi hayo yalivuta hisia zaidi kutokana na magari ya kifahari yaliyotumika, ambapo Diamond alitumia gari lake aina ya Rolls-Royce kumpokea Davido, huku Zuchu akimkaribisha Chioma kwa kutumia Bentley yake.

DAVI 05

Hata hivyo, zaidi ya mapokezi hayo ya kifahari, jambo linalozua mjadala ni sababu ya Davido kurejea Tanzania, hasa ikizingatiwa kuwa ziara yake ya mwisho ilikuwa Februari mwaka huu alipofanya tamasha katika viwanja vya Lugalo Golf Club jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya taarifa zinazozunguka zimehusisha ujio wake na uwezekano wa kukamilisha mradi wa muziki na Diamond, lakini hadi sasa hakuna maelezo rasmi kutoka kwa wasanii hao yanayothibitisha sababu hiyo.

Swali linalobaki ni je, Davido amekuja kwa ziara ya kirafiki au kuna kazi nyingine kubwa ya muziki inayotarajiwa kuunganisha tena majina haya mawili?


DAVI 01

URAFIKI ULIOANZA MWAKA 2013

Historia ya ukaribu wa Diamond na Davido inaelezwa kuanzia mwaka 2013, wakati msanii huyo wa Nigeria alipokuja Tanzania kwa shughuli za muziki na kutambulishwa kwa Diamond kupitia Sallam SK.Kukutana huko kulifungua ukurasa mpya wa ushirikiano wao wa kimuziki, uliozaa wimbo My Number One Remix mwaka 2014.

Ushirikiano huo haukuwa kolabo ya kawaida tu, bali ulikuwa hatua muhimu katika safari ya Diamond ya kupanua muziki wake nje ya Afrika Mashariki, hususan katika soko la Afrika Magharibi ambako Davido alikuwa tayari akijenga jina kubwa.

Wimbo huo uliunganisha ladha ya Bongo Fleva na Afrobeats, huku video yake ikiongozwa na mtayarishaji wa video za muziki kutoka Nigeria, Clarence Peters.

Tovuti ya OkayAfrica, Januari 13, 2014, iliuelezea ushirikiano huo kama muunganiko wa muziki wa Afrika Mashariki na Magharibi, ikionyesha namna wasanii hao walivyoweza kuleta ladha mbili tofauti katika kazi moja.


DAVI 02

DAVIDO ALITUMIA KIASI GANI KUMFIKISHA DIAMOND KIMATAIFA?

Jambo jingine linaloonyesha uzito wa ushirikiano huo ni gharama zilizohusika katika kuufanikisha.

Meneja wa zamani wa Diamond Platnumz Sallam SK, aliwahi kueleza kuwa Diamond alitumia takribani dola 5,000 za Marekani kuwezesha kukutana na Davido, kabla ya gharama za mradi huo kuongezeka na kufikia zaidi ya dola 50,000.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, uwekezaji huo ulikuwa sehemu ya mkakati wa Diamond wa kuingia katika soko la muziki la Nigeria na kujenga jina lake katika kiwango cha Afrika.

Hatua hiyo ilionyesha kuwa mafanikio ya wasanii wa Afrika katika soko la kimataifa hayajengwi kwa kipaji pekee, bali pia kwa uwekezaji, mahusiano na mikakati ya kibiashara.


DAVI 03

TAMASHA LA MWAKA 2018 LILIONYESHA UKARIBU WAO

Urafiki wa wasanii hao uliendelea kuonekana hadharani mwaka 2018, wakati Davido alipofanya tamasha lake la 30 Billion Concert nchini Tanzania.

Katika tamasha hilo, Davido alimualika Diamond kupanda jukwaani na kutumbuiza pamoja wimbo wao wa My Number One Remix, jambo lililopokelewa kwa shangwe na mashabiki waliohudhuria.

Tukio hilo liliripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari vya burudani, vikiwemo TooXclusive, Juni 18, 2018.

Kwa upande mwingine, aliyekuwa meneja wa Diamond, Babu Tale, aliwahi kueleza kuwa Diamond hakulipwa fedha kwa kupanda jukwaani katika tamasha hilo, akisisitiza kuwa kitendo hicho kilitokana na urafiki wao.

Akielezea sababu ya Diamond kushiriki katika tukio hilo, Babu Tale alisema: “Ile ni love tunaita.”

Kauli hiyo inaweka wazi namna mahusiano yao yalivyokuwa na nafasi zaidi ya masuala ya kibiashara, huku yakijengwa pia katika msingi wa kuheshimiana na kusaidiana.

Tanzania imekuwa sehemu muhimu katika safari za Davido

Hivyo Davido amekuwa na historia ya kutembelea Tanzania kwa shughuli za muziki.

Hivyo, ujio huu wa sasa unakuwa wa pili kwa Davido kuripotiwa nchini ndani ya mwaka 2026.


DAVI 04

JE, KUNA UKURASA MPYA WA MUZIKI UNAANDALIWA?

Kurejea kwa Davido Tanzania miezi tisa baada ya tamasha lake la mwisho, huku akipokelewa na Diamond, kumeongeza matarajio ya mashabiki wanaotamani kuona wasanii hao wakifanya kazi nyingine ya pamoja.

Uwezekano wa mradi mpya unavutia zaidi kwa sababu ushirikiano wao wa kwanza ulisaidia kuunganisha masoko ya muziki ya Afrika Mashariki na Magharibi.

Hata hivyo, ni muhimu kutofautisha matarajio ya mashabiki na taarifa zilizothibitishwa. Mpaka sasa, hakuna tangazo rasmi lililotolewa na Diamond au Davido kuhusu kurekodi wimbo mpya, video au kukamilisha mradi maalumu katika safari hii.

Pamoja na kutokuwepo kwa uthibitisho huo, mapokezi ya Davido na Chioma yanaonyesha kuwa ukaribu kati ya familia hizo mbili bado unaonekana hata baada ya miaka mingi tangu ushirikiano wao wa kwanza.

Kwa sasa, mashabiki wanasubiri kuona iwapo kukutana kwa Diamond na Davido kutabaki kuwa ziara ya kirafiki au kutazaa ushirikiano mwingine ambao unaweza kuandika historia mpya katika muziki wa Afrika.

Jambo moja ni wazi,urafiki ulioanza mwaka 2013 uliwahi kuzaa wimbo uliovuka mipaka, na kila wanapokutana, matarajio ya mashabiki kuhusu muziki mpya huibuka tena.