40 za watoto wa Diamond: Hizi ndo tofauti... ile ya Tiffah na ya Sandrah
Muktasari:
- Lakini Septemba 12, 2026, baada ya 40 ya mtoto wake na Zuchu, Sandrah Naseeb, kufanyika Saint Laurent Garden, Kawe jijini Dar es Salaam, mambo yalionekana kuwa na sura nyingine kabisa.
KUNA 40 za watoto ambazo ukizitaja tu, picha ya sherehe, mastaa, kamera na mbwembwe inajitokeza kichwani. Hii ni kwa sababu kwa miaka kadhaa Diamond Platnumz amekuwa akifanya siku 40 za watoto wake kuwa zaidi ya tukio la kifamilia.
Lakini Septemba 12, 2026, baada ya 40 ya mtoto wake na Zuchu, Sandrah Naseeb, kufanyika Saint Laurent Garden, Kawe jijini Dar es Salaam, mambo yalionekana kuwa na sura nyingine kabisa.
Kwa kifupi, Tiffah alitingisha, Nillan akaja na yake, Naseeb Junior akawa gumzo kwa kufichuliwa sura yake, lakini Sandrah safari hii mambo yakawa yametulia zaidi.
PRINCESS TIFFAH
Tukirudi nyuma, 40 ya kwanza iliyoweka mzani huu ilikuwa ya Princess Tiffah, mtoto wa Diamond na Zari Hassan iliyofanyika mwaka 2015.
Wakati huo Diamond na Zari walikuwa miongoni mwa couple zilizokuwa zikifuatiliwa zaidi kwenye burudani za Afrika Mashariki na ujio wa mtoto wao ulikuwa gumzo hata kabla hajazaliwa.
Tiffah alipofikisha siku 40, sura yake iliyokuwa imefichwa kwa muda ikawekwa hadharani. Sherehe hiyo ilifanyika nyumbani kwa Diamond, Madale jijini Dar es Salaam na baadaye kukawa na tukio kubwa Mlimani City. Vyombo vya habari viliripoti uwepo wa mastaa mbalimbali na maandalizi yake yakawa gumzo kubwa.
Lakini si hilo tu. Tiffah aliingia kwenye 40 akiwa tayari ana thamani ya kibiashara. Sura yake ilipotolewa, ilikwenda sambamba na matangazo ya dili za kibiashara, jambo lililoongeza zaidi presha na mvuto wa tukio hilo.
Ndiyo maana hata miaka miwili baadaye, wakati Diamond alipokuwa akijiandaa kwa 40 ya mtoto wake mwingine, Nillan, watu walikuwa tayari wanatega masikio kuona kama atarudia historia ya dada yake.
NILLAN
Ni mtoto wa Diamond na Zari, alitimiza siku 40 Januari 2017. Sherehe yake nayo ilikuwa na familia, marafiki na watu wa upande wa Diamond, lakini kwa kulinganisha na Tiffah, haikufikisha ile presha kubwa ya dada yake. Hata hivyo, bado ilikuwa sehemu ya zile 40 za Diamond zilizokuwa zikifuatiliwa sana na mashabiki.
NASEEB JUNIOR
Hapa Diamond na Tanasha Donna walikuja na kitu kilichofanya 40 hiyo kuwa gumzo kubwa, walimtoa mtoto wao ambaye sura yake ilikuwa imefichwa tangu kuzaliwa. Sherehe hiyo ilifanyika Madale mwaka 2019 na ilikuwa ya mwaliko maalumu, huku familia, watu wa WCB na majina kadhaa ya showbiz wakihudhuria.
Kwa hiyo, Naseeb Junior naye alikuwa na kitu chake. Watu hawakuwa wanaenda tu kusherehekea siku 40, bali walikuwa pia wanataka kumuona mtoto ambaye Diamond na Tanasha walikuwa wamemficha kwa muda.
SANDRAH
Mtoto huyu wa Diamond na Zuchu, aliyezaliwa Agosti 2, 2026, alifikisha siku 40 na familia ikaandaa hafla ya Septemba 12, 2026. Safari hii, tukio likafanyika Saint Laurent Garden, Kawe, na kwa macho ya mtu anayefuatilia historia ya 40 za watoto wa Diamond, tofauti zilianza kuonekana mapema.
Kwanza, haikuwa ile hali ya mastaa kujazana kama tulivyozoea kwenye baadhi ya 40 zilizopita. Majina makubwa yalikuwepo, walipiga picha na kuhudhuria, lakini idadi na mchanganyiko wa mastaa haukuwa ule wa zamani ambao ungeweza kufanya kila kona ya ukumbi kuwa gumzo.
Hata wale wadada maarufu wa mjini ambao mara nyingi huongeza ladha kwenye matukio makubwa ya Diamond, safari hii hawakuonekana kwa wingi ule ambao mtu angeweza kuutegemea. Na hapo ndipo neno 'imepoa' linapoingia.
Si kwamba hapakuwa na sherehe. Hapana. Ila kwa mtu anayelinganisha na Tiffah au hata Naseeb Junior, hii ya Sandrah ilikuwa na mwendo wa taratibu zaidi.
Sehemu kubwa ya mwanzo wa shughuli ilienda kwenye upande wa dini na mila. Madufu yakapigwa, Qur’an ikasomwa, huku wageni wakiendelea na taratibu za hafla. Badala ya muziki na dansi kuanza mapema, burudani ya nguvu ikasubiri hadi usiku kusogea.
Lakini safari hii kulikuwa na picha nyingine iliyojitokeza na ambayo si rahisi kuipuuza.
Sanura Kassim, maarufu Mama Dangote, ambaye ni mama wa Diamond, hakuwa tu mgeni wa kawaida. Kwa muda wa hafla, alionekana kutuzwa, kuheshimiwa na kuhudumiwa kwa namna ya pekee, huku upande wa Zuchu ukiwa mstari wa mbele katika hilo.
Hapa ndipo Khadija Kopa, mama mzazi wa Zuchu, naye alipoingia kwenye picha. Badala ya kuonekana kama mama wa upande mwingine tu wa familia, yeye na Zuchu walionekana kumzunguka Mama Dangote kwa upendo na heshima, jambo lililokuwa miongoni mwa picha zilizotawala usiku huo. kwa kifupi, Mama Dangote alipewa nafasi kubwa sana katika sherehe hiyo.
Hii ni tofauti ambayo inaweza kuonekana ukilinganisha na zile 40 za nyuma. Kwenye matukio hayo, macho ya wengi yalikuwa zaidi kwa Diamond na wanawake ambao amezaa nao watoto, akiwemo Zari na Tanasha, huku kila mmoja akiwa na nafasi yake katika sherehe ya mtoto wake.
Safari hii, kwa sababu mtoto ni wa Diamond na Zuchu, picha ya familia imekuwa pana zaidi. Mama wa mtoto, Zuchu, pamoja na mama yake mzazi, Khadija Kopa, wameonekana kumpa Mama Dangote heshima kubwa, jambo lililoongeza picha ya familia mbili kukutana kufurahia.
Kwa hiyo, ukikaa ukitazama tukio hili kwa jicho la udaku, unaweza kusema hii 40 haikuwa tu ya Sandrah, kwa namna fulani ilikuwa pia usiku ambao Mama Dangote alipewa maua yake.
Muda mwingi ukaonekana kuelekezwa kwenye kuhakikisha Mama Dangote anakuwa sehemu ya tukio kwa namna ya kipekee. Hili likawa moja ya mambo yaliyoifanya 40 hii kuwa na ladha tofauti na zile zilizopita, ambazo zilikuwa zikibeba zaidi presha ya Diamond, mama wa mtoto husika na mastaa waliokuwa wamejazana.
BURUDANI ILICHELEWA
Ilipokaribia saa sita usiku, ndipo baadhi ya wasanii wakaanza kupewa nafasi ya kutumbuiza. Na hapa ndipo 40 ya Sandrah ilipochukua ladha ambayo labda wengi hawakuitegemea.
Badala ya Bongo Fleva na mastaa wa kizazi kipya kutawala jukwaa muda wote, taarabu na muziki wa moja kwa moja vikapewa nafasi kubwa.
Bendi ya Jahazi Modern, Mzee Yussuf na mkewe wakaingia kazini, huku Kassim Mganga naye akitoa burudani. Baadaye Hassan Ally akapanda na kuimba kibao Kata, huku wageni wakianza kujiachia zaidi kadiri usiku ulivyozidi kwenda.
Kulikuwa pia na vinywaji vya aina mbalimbali, vya kawaida na vile vya mchanganyiko, ambavyo vilianza kuonekana zaidi kadiri muda ulivyokwenda.
Kama ilivyo kwa 40 za watoto wa Diamond zilizopita, Sandrah naye hakutoka mikono mitupu kwenye upande wa kibiashara. Mtoto huyo ametajwa kuhusishwa na dili za ubalozi, jambo ambalo limeongeza gumzo kuhusu namna watoto wa Diamond wanavyoanza kuingia kwenye biashara mapema.
Tofauti kubwa ni kwamba kwa Tiffah, suala la dili za kibiashara lilikuwa moja ya vitu vilivyolipua zaidi habari za 40 yake. Sandrah naye sasa anaingia kwenye mstari huo wa watoto wa Diamond ambao hata kabla hawajaanza kuelewa umaarufu, tayari jina lao linaanza kuwa na thamani kibiashara. Lakini kwenye suala la shangwe, hapa ndipo tofauti ilipo.
Tiffah alikuwa kama tukio la kihistoria. Nillan akaja huku watu wakisubiri kuona kama ataweza kurudia presha ya dada yake. Naseeb Junior akaja na fumbo la sura yake iliyokuwa imefichwa. Sandra yeye amekuja wakati ambao familia ya Diamond tayari imezoea matukio kama haya. Hii inaweza kutoa majibu huenda ndiyo sababu usiku wake ukawa wa utulivu zaidi kuliko kishindo.
Kwa hiyo, ukiweka hizi 40 nne mezani, Tiffah, Nillan, Naseeb Junior na Sandrah kila mmoja ana stori yake. Lakini kwa upande wa mbwembwe, mastaa, muziki na presha ya tukio, Tiffah bado anaonekana kuweka kiwango ambacho zile zilizofuata zimekuwa zikilinganishwa nacho.