Kazi na dawa Wanasoka wanavyokula bata na pisi kali
MSANII wa Bongo Flava, Darasa anasema ‘Maisha na Muziki’. Hamaanishi maisha ni muziki, bali anamaanisha baada ya mihangaiko ya maisha kuna burudani pia. Kuna bata. Wakati mwingine watu husema ‘Kazi na dawa.’
Ndio. Watu wanapotoka kwenye mihangaiko ya siku au mwisho wa wiki au mwezi, hupenda kufurahia pia maisha.
Ngoma hiyo iliyotesa hadi sasa ikifikisha miaka saba, inahamasisha bata. Baada ya kazi ngumu, kuna bata. Ndiyo maana hata wanasoka wana kipindi kikifika tu huwa wanatafuta pa kwenda, iwe ni mapumziko ya muda mrefu au hata ya siku chache. Wanapenda pia kufurahi. Kula bata.
Hivyo ndivyo maisha yalivyo. Wanatumia muda mwingi kazini kwao, kambini, uwanjani na safarini kucheza. Hawapati muda wa kupumzika, kukaa karibu na familia zao na wapenzi wao na watu wengine wa karuibu.
Hata hivyo, wanapokutana nao, kuna wanaokula bata kisirisiri na wengine bila kificho. Bata linaliwa kweli na wale wanaojificha wakati mwingine huumbuka.
Hawa hapa ni baadhi ya mastaa wa soka ambao walitrendi na wengine wanatrendi kwa sasa kwenye mitandao ya kijamii wakiwa na pisi kali za Bongo na hawa ni wale wanaotikisa na wanaotikisa kwenye kiwanda cha burudani, mitindo na sanaa.
AZIZ KI NA VANESSA
Hii bado ya moto kabisa. Ni juzi kati tu staa wa Yanga, Stephane Aziz Ki na mwanadada Vanessa Mmasa Kashera walitrendi kwa mahaba mazito waliokuwa wakionyeshana.
Ni hivi. Hawa mara kibao wameonekana wakitoka pamoja na kula bata kinoma na mapema mwezi huu walitrendi mitandao baada ya Aziz Ki kufanyiwa sapraizi na Vanessa kwenye siku yake ya kuzaliwa. Hapo ilikuwa fulu Maua na kukumbatiana na mabusu moto moto. Vanessa ni mwanamitindo sambamba na mwigizaji.
PACOME NA CAREEN SIMBA
Achana na ufundi wa kiungo wa Yanga, Pacome Zouzoua akiwa uwanjani. Huko kitaa pia anakula maisha kitaalamu zaidi.
Hivi karibuni mwamba huyu kutoka Ivory Coast alitrendi akiwa na mwigizaji na mwanamitindo, Careen Simba. Caaren ni miongoni mwa pisi kali ambazo kwa sasa zinafanya vyema kwenye tasnia ya sanaa na burudani. Caaren aliwahi kuwa mpenzi wa mwanamuziki Baraka The Prince na kupata mtoto mmoja wa kike.
NDIKUMANA NA UWOYA
Hii ni miongoni mwa kapo zilizotrendi sana kati ya miaka ya 2007-2009. Ni baada ya beki Mnyarwanda, Hamad Ndikumana aliyewahi kuichezea Stand United kuwa kwenye uhusiano na mwigizaji Irene Uwoya.
Penzi lao lilinoga hadi kufika kufunga ndoa na kupata mtoto mmoja wa kiume aitwaye Krish, hata hivyo walitengana baadae.Uwoya kwa sasa bado wa moto akiendelea kutikisa nchini, lakini Ndikumana aliaga dunia mwaka 2017 akiwa nchi kwao Rwanda.
CARLINHOS NA WEMA SEPETU
Anaitwa Carlos Stenio Fernandes Guimaraes do Carmo. Usisumbuke kutaja hilo jina hapo juu, tamka ‘Kalinyozi’. Huyo ni winga wa zamani wa Yanga kutoka Angola na aliyetikisa vyombo vya habari mwaka 2020 baada ya kuonekana akiwa na ‘Tanzania Sweetheart’ Wema Sepetu. Wabongo walilikuza sana jambo lile lakini ilikuwa ni picha na video za tangazo la moja ya bidhaa hapa nchini.
Wema kwa sasa anafanya maisha yake nchini huku Carlinhos akikipiga kwenye kikosi cha Petro Luanda ya kwao Angola.
BANDA NA ZABIBU KIBA
Huyu ni beki wa Taifa Stars na klabu ya Richards Bay FC na mahusiano yake na Zabibu Kiba ambaye ni dada wa Mfalme wa Bongo Fleva, Ali Kiba yaligonga sana vichwa vya habari na kutrendi kila kona. Banda na Zabibu walifika hatua ya kufunga Ndoa mwaka 2018, na walibahatika kupata mtoto mmoja wa kike. Hii ni miongoni mwa kapo zilizozungumzwa sana wakati wake.
NIYONZIMA NA MARRY BLIZZY
Staa wa zamani wa Yanga na Simba, Haruna Niyonzima naye aliwahi kutrendi kipindi yupo Bongo baada ya kuhusishwa kuwa kwenye mahusiano na Mwanadada anayefanya vizuri kwenye kiwanda cha Bongo Movies, Marry Blizzy.
Wawili hao walizungumzwa sana na inasemekana walikuwa kwenye penzi zito na wameponda bata la hapa na pale ndani ya jiji la Dar es Salaam. Kwa sasa Haruna yupo zake nchini Libya akiwa kwenye klabu ya Taawon Ajdab huku Marry akiendelea na kazi zake za sanaa na sasa anatamba kwenye tamthiliya ya Huba ambapo anatumia jina la Doris.