Jux anakula tu matunda ya WCB Wasafi!
Muktasari:
- Jux, mwanachama wa zamani wa kundi la Wakacha, ni miongoni mwa wasanii wachache wa Bongofleva waliopata nafasi ya kufanya kazi nyingi na WCB Wasafi.
Kwa mara nyingine tena Jux amefanya kazi na mwanamuziki aliyewahi kuwa chini ya WCB Wasafi, awamu hii ikiwa ni zamu ya Mbosso, mwanachama wa zamani wa kundi la Yamoto.
Jux, mwanachama wa zamani wa kundi la Wakacha, ni miongoni mwa wasanii wachache wa Bongofleva waliopata nafasi ya kufanya kazi nyingi na WCB Wasafi.
Tayari amefanya kazi na Diamond Platnumz na Zuchu, vilevile Rayvanny na Mbosso ambao kwa nyakati tofauti kila mmoja aliagana na rekodi lebo hiyo.
Je, ni lini na kwa namna gani Jux alifanya kazi na wasanii hao?, makala haya yanaenda kuangazia hilo kwa kufuatana na mtiririko wa muda wa kazi husika ilipotoka.
1. Diamond & Jux
Tayari Diamond, mshindi wa MTV EMAs mara tatu, amesikika katika nyimbo tatu za Jux - Sugua (2019), Enjoy (2023) na Ololufe Mi (2024), zote zikitayarishwa na S2kizzy kutokea studio za Pluto Republic.
Naye Jux amesikika katika wimbo wa Diamond, Joy (2026) ambao pia umepita katika mikono ya S2kizzy ambaye alifahamika na wengi baada ya kutengeneza wimbo wa Country Wizzy, Aah Wapi (2016).
Oktoba 2024, video wimbo 'Enjoy' iliyotayarishwa na Director Fole X na kuachiwa Oktoba 7, 2023, iliweka rekodi ya kutazamwa mara milioni 100 YouTube ikiwa ni video ya kwanza nchini kufanya hivyo ndani ya muda mfupi.
Vilevile ilikuwa ni video ya kwanza kwake kufikia namba hizo ila ndani ya Bongofleva ilikuwa ni ya nane huku Jux, mwanzilishi wa chapa ya African Boy, akiwa msanii wa nne kwa ujumla kufanya hivyo.
2. Zuchu & Jux
Katika albamu ya pili ya Jux, King of Hearts (2019) iliyotoka ikiwa na nyimbo 16, moja kati ya hizo uitwao 'Nidhibiti' alimshirikisha Zuchu, mshindi mara saba wa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kwa msimu miwili pekee.
Kufuatia kolabo hiyo, Jux akawa msanii wa kwanza wa Bongofleva kutokea nje ya WCB Wasafi ambaye alifanikiwa kumshirikisha Zuchu katika wimbo wake.
Kabla ya hapo, Zuchu alikuwa akishirikiana zaidi na wasanii wa lebo yake ya WCB na wachache wa kimataifa, na hata yeye hashirikishi kabisa wasanii wa Bongofleva nje ya WCB Wasafi katika nyimbo zake.
Licha ya wimbo huo (Nidhibiti) kufanya vizuri kwa kiasi chake, wanamuziki hao walishindwa kuachia video yake, kitu ambacho kimejirudia sana kwa wasanii wengine wa nje ya WCB Wasafi waliokuja kufanya kazi na Zuchu baadaye.
3. Rayvanny & Jux
Katika albamu ya kwanza ya Rayvanny, Sound From Africa (2021) iliyotoka akiwa bado yupo WCB Wasafi, Jux alisikika katika wimbo namba 16 uitwao 'Lala' ukiwa umetayarishwa na S2kizzy.
Lala ni miongoni mwa nyimbo zilizoibeba albamu hiyo ukifanya vizuri hasa mtandaoni (digital streaming), ambapo hadi sasa video yake imeshatazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 16.4.
Wawili hao waliutumia kutuma ujumbe kwa wapenzi wao ambao walikuwa wameachana nao, Jux akizungumza na Vanessa Mdee, huku Rayvanny akisema Fahyma.
Hata hivyo, baadaye Rayvanny alikuja kurudiana na Fahyma, mwanamitindo ambaye ametokea katika video za nyimbo zake zaidi ya sita akiwa ndiye mrembo pekee mwenye rekodi hiyo kwa msanii huyo.
4. Mbosso & Jux
Mwaka mmoja baada ya Mbosso kuondoka WCB Wasafi, ndipo amekuja kusikika katika wimbo wake Jux, Kipepeo (2026) unaofanya vizuri kwa sasa.
Jux amefanya kazi Mbosso kipindi hiki ambacho msanii huyo anapiga sana kolabo kubwa ambapo hapo awali alifanya kazi na Harmonize na Alikiba, mwanzilishi wa Kings Music.
Mbali na uzuri wa wimbo huo (Kipepeo), pia video yake isimamiwa kwa ustadi mkubwa na Director Fole X akifanyika Zanzibar na Dar es Salaam.
Kupitia wimbo wa Kipepeo, Jux na Mbosso wanasherehekea uzuri wa Mwafrika, utamaduni wa Kiafrika, na nguvu ya upendo usio na mipaka. Hii ni kazi nyingine ya Jux ambayo S2kizzy amehusika na kuitendea haki.