Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Johari alivyobadili upepo kwenye biashara, aitaja ndoa yake

JOHARI Pict

Muktasari:

  • Licha ya kuwa si mtu wa kuonekana sana kwenye matukio ya burudani kama ilivyokuwa zamani, Johari ameendelea kufanya kazi zake kimya kimya huku akisimamia miradi mbalimbali ya filamu na biashara zake binafsi.

Kwa zaidi ya miaka 20 kwenye tasnia ya filamu Tanzania, Blandina Chagula ‘Johari’ ameendelea kuwa miongoni mwa waigizaji waliodumu kwa muda mrefu huku akibadilika kutoka kuwa mwigizaji wa kawaida hadi mtayarishaji, mfanyabiashara na mmoja wa wanawake wenye ushawishi mkubwa kwenye sekta ya filamu nchini.

Licha ya kuwa si mtu wa kuonekana sana kwenye matukio ya burudani kama ilivyokuwa zamani, Johari ameendelea kufanya kazi zake kimya kimya huku akisimamia miradi mbalimbali ya filamu na biashara zake binafsi.

Katika mahojiano haya ya Dakika 5 Na..., amefunguka kuhusu hali ya tasnia ya filamu kwa sasa, safari yake ya mafanikio, biashara, ndoa na mipango yake ya baadaye.


Mwanaspoti: Kwa sasa wengi wanakufahamu kama mtayarishaji na mfanyabiashara. Mabadiliko hayo yamekuwaje kwako?

Johari: Ni hatua ya ukuaji. Nilianza kama mwigizaji lakini kadri muda ulivyokwenda niliona umuhimu wa kujifunza upande wa uzalishaji na biashara. Leo ninafurahia kuona ninachangia tasnia siyo tu kwa kuigiza bali pia kwa kutengeneza fursa kwa wengine.

JOHA 05

Mwanaspoti: Unaionaje tasnia ya filamu Tanzania kwa sasa?

Johari: Kuna mabadiliko makubwa. Teknolojia imebadilika na namna ya kusambaza kazi pia imebadilika. Changamoto bado zipo, pia fursa zimeongezeka. Kazi yetu ni kuhakikisha tunatengeneza maudhui bora yatakayoweza kushindana ndani na nje ya Tanzania.


Mwanaspoti: Wapo wanaosema tasnia ya filamu imepoteza mvuto wake ukilinganisha na zamani. Wewe unasemaje?

Johari: Si kwamba imepoteza mvuto, bali mazingira yamebadilika. Zamani watu walikuwa wanategemea sana DVD na televisheni. Sasa kuna majukwaa ya kidijitali. Tunapaswa kubadilika na wakati na kutumia fursa zilizopo.


Mwanaspoti: Ni kitu gani kimekusaidia kudumu kwa muda mrefu kwenye tasnia?

Johari: Nidhamu, kujitambua na kuheshimu kazi. Pia nimekuwa nikijifunza kila siku. Ukijiona unajua kila kitu ndiyo mwanzo wa kurudi nyuma.

JOHA 01

Mwanaspoti: Mbali na filamu, biashara zina nafasi gani kwenye maisha yako?

Johari: Biashara ni sehemu muhimu ya maisha yangu. Sanaa inaweza kuwa na misimu yake, hivyo ni muhimu kuwa na vyanzo vingine vya mapato. Nimekuwa nikiamini msanii anatakiwa kuwa na kitu chake nje ya sanaa.


Mwanaspoti: Unawashauri nini wasanii wa kizazi hiki kuhusu biashara?

Johari: Wasisubiri umaarufu pekee uwalishe maisha yote. Watumie majina yao vizuri kujenga biashara na uwekezaji wa muda mrefu. Umaarufu unaweza kupungua, lakini biashara nzuri inaweza kudumu kwa miaka mingi.

JOHA 04

Mwanaspoti: Kwa miaka yote hii umekuwa mtu wa kuweka maisha yako binafsi mbali na macho ya umma. Kwa nini?

Johari: Kuna amani kubwa sana unapokuwa na mipaka kati ya maisha ya kazi na maisha binafsi. Mashabiki wanahitaji kuona kazi zangu, lakini si lazima wajue kila kitu kinachoendelea kwenye maisha yangu.


Mwanaspoti: Mashabiki wengi bado wanakuuliza kuhusu ndoa. Wewe mwenyewe una mtazamo gani kuhusu suala hilo?

Johari: Ndoa ni jambo zuri na kila mwanamke anatamani kuwa na familia yenye furaha. Mimi naamini kila jambo lina wakati wake. Muhimu ni kupata mtu anayekuheshimu, anayekuelewa na ambaye mnaweza kujenga maisha yenye amani.


Mwanaspoti: Mwanamume wa aina gani anaweza kukuvutia?

Johari: Awe mtu anayejitambua, anayefanya kazi zake kwa bidii na anayeheshimu wanawake. Mimi naamini maelewano, heshima na upendo wa kweli vina thamani kubwa kuliko vitu vingine vingi.

JOHA 02

Mwanaspoti: Wasanii wengi wa kike sasa wanaingia kwenye uzalishaji wa filamu na biashara. Unalionaje hilo?

Johari: Nafurahi sana kuona wanawake wanachukua nafasi kubwa zaidi kwenye tasnia. Kadri wanawake wanavyoongezeka kwenye maamuzi na umiliki wa miradi, ndivyo tasnia inavyokuwa imara zaidi.


Mwanaspoti: Kuna mradi gani mpya ambao mashabiki wanapaswa kuutarajia kutoka kwako?

Johari: Kuna mambo kadhaa yanaendelea nyuma ya pazia. Bado siwezi kusema mengi kwa sasa, lakini mashabiki wakae tayari kwa kazi mpya ambazo zitakuwa na ubora mkubwa.

JOHA 03

Mwanaspoti: Ujumbe wako wa mwisho kwa mashabiki?

Johari: Nawashukuru kwa upendo wao wa miaka yote. Wao ndiyo sababu tumekuwa hapa kwa muda mrefu.

Waendelee kuunga mkono kazi za Kitanzania kwa sababu maendeleo ya tasnia yanahitaji mchango wa kila mmoja wetu.