Jihan: Ndoto zinaweza kutimia ukiamini, kujituma
Mshindi wa Miss Grand International 2026, Jihan Dimack, amesema ushindi wake ni ushahidi kuwa ndoto zinaweza kutimia iwapo mtu ataamini katika uwezo wake, kufanya kazi kwa bidii na kuwa mvumilivu, akiwataka vijana kutokata tamaa wanapokutana na changamoto katika safari ya kufikia malengo yao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 19, 2026, Jihan amesema safari yake ya uanamitindo inaweza kuwa chanzo cha hamasa kwa vijana wanaotamani kufanikiwa katika maeneo mbalimbali ya maisha, akibainisha kuwa alianza kujihusisha na kazi hiyo akiwa na umri wa miaka 17.
Amesema familia ni sehemu muhimu ya maisha yake, akieleza kuwa anathamini familia yake, anapenda kufanya kazi kwa bidii na kuweka maslahi ya familia mbele.
Akitoa ujumbe kwa Watanzania na vijana wengine barani Afrika, Jihan amesisitiza umuhimu wa kuendelea kufuatilia ndoto bila kujali changamoto zinazoweza kujitokeza.
“Kila mtu anapaswa kuendelea kufuatilia ndoto zake, iwe katika michezo, sanaa, uanamitindo au eneo lolote analolipenda. Muhimu ni kuamini katika uwezo wako, kufanya kazi kwa bidii na kutokata tamaa unapokutana na changamoto,” amesema Jihan.
Ameongeza kuwa imani yake kwa Mungu inampa nguvu ya kuendelea kujituma, akiamini kuwa kila jambo lina wakati wake na milango ya mafanikio inaweza kufunguka kwa yule anayevumilia na kuendelea kufanya juhudi.
Katika hatua nyingine, mama wa Jihan, Shufaa Ismail, amepinga wanaotilia shaka uraia wa binti yake, akisisitiza kuwa alizaliwa na kukulia Mwanza kabla ya familia kuhamia Dar es Salaam.
Shufaa amesema Jihan ni mtoto wake wa pili kati ya watoto watano na alizaliwa katika Hospitali ya Mwananchi mkoani Mwanza.
“Jihan ni Mtanzania, amezaliwa Mwanza na ndiyo maana tangu walipoanza mashindano, aliandika kuwa anatoka Tanzania. Kwa hiyo, wanaozungumza hivyo wanafanya hivyo bila sababu, kwa sababu moja ya vigezo vya kushiriki ni kujulikana umetoka taifa gani,” amesema.
Amesema baadhi ya watu wanaotoa madai hayo kwenye mitandao ya kijamii wanapaswa kuacha kueneza taarifa zinazoweza kuleta mkanganyiko kuhusu utambulisho wa binti yake.
“Naona baadhi ya watu kwenye mitandao wakisema kwamba Jihan si Mtanzania. Sidhani kama wanafanya vyema, kwa sababu wanaompenda Jihan ni wengi. Hivyo, hao wachache wasiharibu kwa kuanzisha uzushi kuhusu Jihan,” amesema.
Shufaa, ambaye amesema ni Msukuma kutoka Mwanza, anaamini baadhi ya wanaotilia shaka uraia wa binti yake wanaweza kuwa wanachanganywa na rangi yake pamoja na uwezo wake wa kuzungumza Kiingereza.
“Mimi ni Msukuma kutoka Mwanza, na nimemzaa Jihan katika Hospitali ya Mwananchi huko Mwanza. Labda hiyo rangi na Kiingereza kingi ndicho kinachowachanganya baadhi ya Watanzania,” amesema.
Akizungumzia hisia zake baada ya Jihan kutangazwa mshindi wa Miss Grand International 2026, Shufaa amesema alifurahi kiasi cha kushindwa kuzuia machozi ya furaha. Ameeleza kuwa katika kipindi cha mashindano alikuwa akimtia moyo binti yake, hasa alipokuwa akionekana kukata tamaa.
“Niliufurahia ushindi wa Jihan sana, lakini nilishindwa kuvumilia, nililia kwa furaha. Nilikuwa nikimtia moyo sana katika kipindi ambacho alikata tamaa kuhusu mashindano,” amesema.
Shufaa amesema aliamini binti yake angefanya vizuri kutokana na bidii aliyoonyesha katika maandalizi, ikiwamo kuamka mapema na kushiriki shughuli mbalimbali za vyombo vya habari zilizohusiana na mashindano hayo.
Amesema Jihan alikuwa akiamka saa 12 asubuhi, sawa na saa sita mchana kwa mfumo wa saa za kimataifa, na kwenda kwenye shughuli hizo, jambo lililompa matumaini ya kufanya vizuri. Hata hivyo, alikiri kuwa na hofu kwa sababu binti yake alikuwa akiiwakilisha Afrika katika mashindano hayo.
“Jihan alikuwa anajituma sana. Alikuwa anaamka saa 12 asubuhi na kwenda kwenye shughuli za vyombo vya habari. Wengine hawakuwa wakifanya kama yeye, kwa hiyo hilo lilikuwa linanipa nguvu, ingawa nilikuwa na hofu kwa sababu alikuwa anatoka Afrika,” amesema.
Ameongeza kuwa kauli ya mwanzilishi wa Miss Grand International, Papa Nawat, kuhusu kufuatilia washiriki kupitia kamera wakati wote wa mashindano ilimpa moyo zaidi, akiamini kuwa juhudi za Jihan katika shughuli mbalimbali zingeweza kumsaidia kufikia lengo lake.
Shufaa amewashukuru Watanzania kwa kumuunga mkono binti yake hadi kutwaa taji hilo, ambalo fainali yake ilifanyika nchini Thailand.
Kwa upande wake, mwanzilishi wa Miss Grand International, Papa Nawat, amesema mashindano hayo hayabagui washiriki kwa misingi ya rangi, uraia, dini au uwezo wa kifedha, bali huzingatia ubora wa mshiriki na mchango anaoweza kuutoa kwa dunia.
Akizungumzia falsafa ya mashindano hayo, Nawat amesema lengo ni kuwapa nafasi wanawake wenye ndoto na uwezo wa kuzitimiza, bila kujali nchi wanazotoka au imani zao za kidini.
“Hatujali rangi ya ngozi, iwe nyeusi, ya kahawia au nyeupe. Pia hatuangalii pasipoti ya mtu, dini yake, iwe Muislamu, Mkristo, Mbudha au Mhindu, wala kiasi cha fedha alichonacho. Tunaangalia ubora wake na kile anachoweza kushiriki na dunia,” amesema Nawat.
Amesema anaamini kila mtu ana maisha yake ya kuishi na anapaswa kutumia fursa alizonazo kufanya mambo yenye maana, ikiwamo kuwasaidia wengine kutimiza malengo yao.
“Ninaamini naishi mara moja tu, sina maisha mengine ya kuja baadaye. Ndiyo maana ninataka kufanya mambo mbalimbali. Nina uwezo wa kujitunza na sasa nina fedha za kuwasaidia wengine, ndiyo maana ninaendelea kuwaunga mkono wasichana, hasa wale wanaotaka kutimiza ndoto zao,” amesema Nawat.