Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Isha Mashauzi; Miaka 20 katika Taarabu, Jahazi hadi Mashauzi Classic

MASHAUZI Pict

Muktasari:

  • Safari yake ilianza Jahazi Modern Taarab chini ya Mfalme Mzee Yussuf na alipata nafasi ya kujifunza muziki kwa vitendo, kupanda jukwaani na kutambulika zaidi.

MWANAMUZIKI wa Taarab, Isha Mashauzi mwaka huu anatimiza miaka 20 kwenye gemu, safari iliyomtoa kwenye hatua za mwanzo za muziki hadi kujenga jina lake na baadaye kuwa mmiliki wa Bendi ya Mashauzi Classic.

Safari yake ilianza Jahazi Modern Taarab chini ya Mfalme Mzee Yussuf na alipata nafasi ya kujifunza muziki kwa vitendo, kupanda jukwaani na kutambulika zaidi.

Baadaye, Isha aliamua kujenga njia yake na kuanzisha Mashauzi Classic, bendi iliyompa nafasi ya kuendelea kukuza jina lake na kutoa kazi zilizowafikia mashabiki wa taarab nchini.

Katika miaka hiyo, ameshuhudia mabadiliko makubwa kwenye muziki, kutoka mfumo wa zamani wa usambazaji wa kazi hadi zama za kidijitali, huku akiwa amebaki kwenye gemu na kuendelea kufanya muziki.

Katalogi yake inahusisha nyimbo mbalimbali zilizopata nafasi kwa mashabiki, zikiwamo Nani Kama Mama, Tugawane Ustaarabu, Viwavi Jeshi, Nimpe Nani, Vimba na Mke Mwenzio, miongoni mwa nyingine.

Sasa, baada ya miongo miwili kwenye sanaa, Isha anafungua ukurasa mwingine kwa kuandaa sherehe ya safari hiyo kwa tamasha maalumu la litakalofanyika Oktoba 24, 2026, Super Dome, Masaki, Dar es Salaam, likiwa na wasanii kutoka fani mbalimbali.

Akizungumza na Mwanaspoti, Isha anafunguka kuhusu mwanzo wake, maisha ya Jahazi, uamuzi wa kuanzisha Mashauzi Classic, kazi zilizomjenga, mabadiliko ya muziki na sababu ya kuamua kusherehekea miaka 20 kwa tamasha.


MASHA 01

MWANASPOTI: Isha, ukiangalia miaka 20 ya muziki, unaiona vipi safari yako tangu ulipoanzia hadi leo?

ISHA MASHAUZI: Naiona kama safari yenye mambo mengi. Nilianza nikiwa na mapenzi na muziki na nilitaka kujifunza. Miaka imepita na nimepitia hatua tofauti, nimejifunza mengi na nimekutana na watu ambao wamekuwa sehemu ya safari yangu.


MWANASPOTI: Mwanzo wako mkubwa ulikuwa Jahazi Modern Taarab. Uliingiaje kwenye kundi hilo?

ISHA MASHAUZI: Nilipata nafasi ya kuingia Jahazi na kufanya kazi chini ya Mzee Yussuf. Huo ulikuwa wakati muhimu kwangu kwa sababu nilipata nafasi ya kujifunza muziki kwa vitendo, kupanda jukwaani na kukutana na mashabiki wengi.


MWANASPOTI: Mzee Yussuf alikuwa na mchango gani kwenye hatua yako ya mwanzo?

ISHA MASHAUZI: Alikuwa sehemu muhimu sana. Nilipata nafasi ya kufanya kazi chini yake na kujifunza mambo mengi kuhusu muziki na jukwaa. Huwezi kusahau mtu aliyekupa nafasi wakati bado unaanza.


MASHA 02

MWANASPOTI: Kuna nini kikubwa ulichobeba kutoka Jahazi ambacho baadaye kilikusaidia ulipoanza safari yako mwenyewe?

ISHA MASHAUZI: Nilijifunza uvumilivu, nidhamu ya kazi, namna ya kukabiliana na mashabiki na kusimama jukwaani. Pia nilijifunza kwamba muziki unahitaji kujitoa na kufanya kazi kwa muda mrefu.


MWANASPOTI: Baadaye ukaanzisha Mashauzi Classic. Uamuzi huo ulitokana na nini?

ISHA MASHAUZI: Niliona ni wakati wa kujaribu kujenga kitu changu. Nilikuwa nimepata uzoefu na nilikuwa na mawazo yangu kuhusu muziki mbao nilitaka kuufanya. Mashauzi Classic ikawa sehemu ya safari hiyo.


MASHA 03

MWANASPOTI: Kuanzisha bendi yako mwenyewe kulikuwa na changamoto gani?

ISHA MASHAUZI: Zilikuwepo. Unatakiwa kuwajenga watu, mashabiki na kuhakikisha bendi ina mwelekeo. Lakini tuliamini katika kile tulichokuwa tunakifanya na tuliendelea kusonga mbele.


MWANASPOTI: Katika safari ya Mashauzi Classic kuna nyimbo kama Nani Kama Mama, Tugawane Ustaarabu, Viwavi Jeshi, Nimpe Nani, Vimba na Mke Mwenzio. Unazikumbukaje kazi hizo na nafasi yake kwenye safari yako?

ISHA MASHAUZI: Kila wimbo una historia yake. Ni kazi ambazo ziliwafikia mashabiki na baadhi yao zimeendelea kukumbukwa hata baada ya miaka kupita. Hilo linanifurahisha kwa sababu linaonyesha ujumbe na kazi tulizofanya zilikuwa na nafasi kwenye maisha ya watu.


MASHA 04

MWANASPOTI: Miaka 20 imekuja sambamba na mabadiliko makubwa ya muziki. Taarab ya leo unaiona vipi ukilinganisha na ulipoanza?

ISHA MASHAUZI: Mambo yamebadilika sana. Teknolojia imebadilika, namna ya kusambaza muziki imebadilika na hata mashabiki wamebadilika. Zamani kulikuwa na njia tofauti za kusikiliza na kusambaza muziki, lakini leo mitandao ya kijamii imekuwa sehemu kubwa sana.


MWANASPOTI: Mabadiliko hayo yameathiri vipi kazi ya msanii?

ISHA MASHAUZI: Teknolojia inakupa nafasi ya kuwafikia watu wengi haraka, lakini ushindani nao umekuwa mkubwa. Msanii anatakiwa kufanya kazi zaidi na kujifunza mambo mapya.


MASHA 05

MWANASPOTI: Wewe pia umeonekana ukifanya mambo nje ya muziki, ikiwemo biashara na uigizaji. Hilo limekuja vipi?

ISHA MASHAUZI: Muziki bado ni sehemu kubwa ya maisha yangu, lakini msanii pia anatakiwa kuwa na shughuli nyingine. Nimekuwa nikifanya biashara na nimepata nafasi ya kujaribu uigizaji. Hayo ni maeneo ambayo yamenipa uzoefu mwingine.


MWANASPOTI: Kuna wakati mashabiki wamekuwa wakiona umetulia kwenye muziki na kudhani umeacha. Unasemaje?

ISHA MASHAUZI: Kuwa kimya kwa muda hakumaanishi umeacha muziki. Kuna wakati unaweza kuwa unaandaa kitu au una shughuli nyingine. Mimi bado muziki ni sehemu yangu.


MWANASPOTI: Umeendelea pia kushirikiana na wasanii wa kizazi kingine. Unaonaje mchanganyiko wa taarab na Bongo Flava?

ISHA MASHAUZI: Muziki hauna mipaka. Unaweza kuchanganya mitindo tofauti na ukapata kazi nzuri. Muhimu ni kuheshimu kila aina ya muziki na kuhakikisha unachofanya kina ubora.


MASHA 06

MWANASPOTI: Sasa baada ya miaka 20, umeamua kuisherehekea safari hii kwa tamasha. Kwa nini umechagua kufanya hivyo?

ISHA MASHAUZI: Nilitaka kusherehekea pamoja na mashabiki wangu. Hizi miaka siyo zangu peke yangu. Kuna watu wamekuwa wakinisikiliza, wakija kwenye maonyesho yangu na kunipa nguvu. Kwa hiyo nimeona tufanye sherehe pamoja.


MWANASPOTI: Unataka mashabiki wapate kitu gani kwenye usiku huo?

ISHA MASHAUZI: Nataka wawe na usiku wa kipekee. Kutakuwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali na nitakuwa pamoja nao kusherehekea safari hii.


MWANASPOTI: Umefanya miaka 20 ndani ya sanaa. Ungependa Isha wa miaka hiyo akumbukwe kwa kitu gani?

ISHA MASHAUZI: Ningependa akumbukwe kama mtu aliyependa muziki, aliyefanya kazi na ambaye hakuacha kujifunza. Miaka imepita lakini bado nina hamu ya kufanya kazi na kuwapa mashabiki muziki.


MWANASPOTI: Ukipata nafasi ya kuzungumza na Isha aliyeanza safari hii miaka 20 iliyopita, ungemwambia nini?

ISHA MASHAUZI: Ningemwambia asiogope changamoto. Kila safari ina matatizo yake, lakini ukiamini unachokifanya na ukawa mvumilivu, unaweza kufika mbali.


MWANASPOTI: Na kwa mashabiki waliokuwa na wewe tangu mwanzo hadi leo?

ISHA MASHAUZI: Nawashukuru sana. Wao ndio wamefanya safari hii iwe na maana. Wengine walinijua tangu Jahazi, wengine kupitia Mashauzi Classic na wengine wamekuja baadaye. Wote ni sehemu ya miaka yangu 20.