Mapenzi yanavyowatesa mastaa bongo kipindi hiki

Muktasari:
- Iko hivi. Karibu siku 10 sasa tangu kuanza kwa mfungo huo ambao waumini wa dini ya Kiislamu wote ulimwenguni wanajizuia kula na kunywa sambamba na kujiepusha na mambo machafu na kujibidiisha katika mambo mazuri na kufanya toba ikiwa ni utekelezaji wa nguzo ya nne ya imani ya dini hiyo.
KAMA ni kuteswa kwa mapenzi kwa baadhi ya wasanii wa Bongo, basi ni kipindi hiki cha mfungo wa mwezi wa Ramadhani ambao umekuwa shubiri kwao.
Iko hivi. Karibu siku 10 sasa tangu kuanza kwa mfungo huo ambao waumini wa dini ya Kiislamu wote ulimwenguni wanajizuia kula na kunywa sambamba na kujiepusha na mambo machafu na kujibidiisha katika mambo mazuri na kufanya toba ikiwa ni utekelezaji wa nguzo ya nne ya imani ya dini hiyo.
Kutokana na hali hiyo, wapo baadhi ya mastaa wa Bongo ambao ni waumini wa Kiislamu wamejikita pia kutekeleza mfungo huo, kiasi wale waliokuwa wakiishi kinyumba na wenzao, wamelazimika kutengana kwa muda ili kuepuka kuingia matatani katika utekelezaji wa ibada hiyo.
Mwanaspoti limefanya mahojiano na baadhi ya mastaa waliokuwa kwenye uhusiano bila ya kufunga ndoa, wamefunguka jinsi wanavyoweza kuishi katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani.

MARIOO
Nyota huyu wa Bongo fleva anasema: “Hili suala liko wazi na linaeleweka, na ukijua thamani ya mwezi huu huwezi kukumbatia dhambi ya aina yoyote. Mimi nalazimika kuwa mbali na mama mtoto wangu Paula hadi pale mwisho wa mwezi huu na nashukuru, Paula ni mwanamke mwelewa ndio maana nataka kutimiza jambo la ndoa mwaka huu mapema sana ili mwakani yasinikute kama haya ya mwezi huu , nampenda sana yule mwanamke.”

ZUCHU
Kupitia simu ya mama yake Khadija Kopa, msanii wa Bongofleva, Zuchu alizungumza machache na Mwanaspoti akisema: “Akaa mwenzangu kwenye hili mpenzi si lolote wala chochote mbele ya Rehema za Mwenyezi Mungu, na hiki kitu mpenzi wangu anakifahamu na nimemweleza katika kipindi hiki lazima tukae mbali mbali ndio.”€
MASHA LOVE
Mwanadada ambaye amejizolea umaarufu mkubwa Bongo kwa staili yake ya kuchezesha matiti anasema: “Kwa sasa nimerudi nyumbani, nimetengana na Mose Iyobo kwa muda hadi huu mwezi wa mfungo uishe, maana mimi na Mose tunaishi nyumba moja na watu wengi wanafahamu kuwa sisi ni wapenzi, sasa siwezi kuendelea kukaa naye na hali ya kuwa mimi nafunga.”
KALALA JUNIOR
Mwanamuziki wa muziki wa dansi anasema; “Mpenzi si kitu muhimu kama ibada ya mfungo wa mwezi Ramadhani, kwangu mfungo ni kitu kikubwa kuliko jambo lolote lile, nimekuwa nikifunga na kufanya ibada tangu nikiwa mdogo hadi sasa. Mpenzi na mambo mengine ya kijinga itabidi vingoje kwanza.”

ISHA MASHAUZI
“Kwangu mimi hii ni zaidi ya ibada, sheria za kuishi na mume ziko wazi nimeingia katika mfungo kwa kufuata taratibu na sheria zote kama Mwenyezi Mungu alivyosema, mpenzi itabidi angoje hadi Ramadhani ipite, na inshallah kabla mwaka haujaisha taratibu za ndoa zitakuja.”€

WHOZU
“Mimi sio Muislamu, lakini mpenzi wangu ni Muislamu, ndio maana nipo mbali naye ili nisimuharibie swaumu yake katika kipindi hiki ambacho ni muhimu kwake, na naheshimu sana dini yake”.
KUSAH
Mwimbaji wa Bongofleva anasema; “Pamoja na kuishi na Aunt Ezekiel nyumba moja, lakini huwa mwezi kama huu nakuwa mbali kwenye baadhi ya mambo ambayo hayatakiwi kufanywa, sababu mimi ni Muislamu na huwa nafunga ifikapo huu mwezi.”
SHILOLE
Mjasiriamali na msanii anasema; “Mimi ndio maana huwa napenda kuwa ndani ya ndoa sababu ya vitu kama hivi, huu mwezi ni mwezi kwanza mapenzi baadaye, mambo mengine yote ambayo nafanya au mtu anafanya akiwa na mpenzi wake inatakiwa ayaache, mimi kwa sasa nimeacha kila kitu na mpenzi wangu, kwani dini hainiruhusu.”