Hongera Majay kwa kumsubiri Lulu akue
STAA wa Bongo Movie, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na CEO wa E Media, inayomiliki redio EFM na luninga ya ETV, Francis Ciza ‘Majay’, wameshatangaza ndoa. Mipango inaendelea ya wao kuelekea kukamilisha lengo la kuwa mume na mke.
Katika kuitafuta njia ya kuwazungumzia Lulu na Majay, naomba nimlete kwenye mjadala Aaliya Haughton ambaye ni mwanamuziki mwenye kipaji kikubwa, lakini hakuishi sana.
Aaliyah aliishi duniani kwa miaka 22 tu. Alifariki Agosti 25, 2001 akiwa bado maji ya moto sana. Ndoto zake zikazimika hapo. Hongera kwetu tuliopata bahati ya kuhudumiwa muziki wake kwa miaka saba.
Miaka 24 iliyopita, Aaliyah alitoa albamu yake ya kwanza yenye jina Age Ain’t Nothing but a Number. Iliingia sokoni Mei 24, 1994. Jina hilo la albamu lilitokana na wimbo uliopata umaarufu mkubwa; Age Ain’t Nothing but a Number (Umri sio chochote ni namba tu).
Wakati Aaliyah anatoa wimbo huo alikuwa na umri wa miaka 15 ambao, haukuwa ukimruhusu kujihusisha na mapenzi. Basi ndani ya Age Ain’t Nothing but a Number, Aaliyah anaimba hisia zake za kimapenzi akimwambia mwanaume anavyompenda na kumtaka awe huru naye. Anamtaka ajue kuwa umri sio chochote isipokuwa ni namba tu.
Stori ikawa hivi; Aaliyah alikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na galacha wa R&B, Robert Kelly, wewe mwite R Kelly. Wimbo Age Ain’t Nothing but a Number uliandikwa na R Kelly. Zaidi R Kelly ndiye aliyetengeneza nyimbo zote za albamu hiyo kwenye studio za Chicago Recording Company, Marekani.
Pamoja na R Kelly kusimama kama prodyuza wa nyimbo hizo, vilevile alishiriki nyimbo mbili ambazo pia zilibamba kwenye chati mbalimbali; Back & Forth na At Your Best (You Are Love). Kampuni zilizosimamia usambazaji na mauzo ya albamu hiyo ni Jive na Blackground Records.
Tuikaribie somo; prodyuza mkuu wa albamu hiyo alikuwa Barry Henkerson. Kwa kifupi Hankerson alikuwa meneja wa R Kelly. Henkerson ni mjomba wa Aaliyah. Sasa basi Aaliyah alipokuwa na umri wa miaka 12, Henkerson alimtambulisha kwa R Kelly ili washirikiane kumtoa kimuziki. Wakati huo R Kelly alikuwa na umri wa miaka 24.
R Kelly baada ya kukabidhiwa Aaliyah, akamfundisha na kumjenga kimuziki. Kwa bahati mbaya sana, R Kelly alimfundisha Aaliyah mpaka mapenzi. Uhusiano wao ukawa siri. Hata hivyo, mwaka 1995, ikabainika kuwa kumbe hata wimbo Age Ain’t Nothing but a Number, ulikuwa kuhalalisha mapenzi yao ya mtoto na ‘baba yake mdogo’.
MENGI YAKAFICHUKA
Ikavuja kuwa R Kelly na Aaliyah walifunga ndoa ya siri Agosti 30, 1994, yaani miezi mitatu baada ya albamu ya Age Ain’t Nothing but a Number kuingia sokoni. Cheti cha ndoa kikavuja kuonesha kuwa ndoa ilifungwa kisheria kwa mamlaka ya Jimbo la Illinois na jimbo dogo la Cook.
Wazazi wa Aaliyah wakaona imekuwa hatari, wakaingilia kati. Wakasimama kidete kuhakikisha ndoa ya Aaliyah na R Kelly inavunjwa. Mtoto wa kike hakuwa na pingamizi. Hata hivyo, mchakato wote ulifanywa kwa siri na daima Aaliyah na R Kelly walipohojiwa kuhusu ndoa yao walikanusha.
Cheti cha ndoa ya R Kelly na Aaliyah kilivuja. Kikaonesha kwamba mamlaka za Illinois na Cook zilidanganywa umri wa Aaliyah. Cheti kikaonesha kuwa Agosti 30, 1994, wakati ndoa inafungwa, Aaliyah alikuwa na umri wa miaka 18, kitu ambacho kilikuwa ni uongo mkubwa.
Simulizi ya Aaliyah inatoa somo kuwa ipo kiu kubwa ya watu kukimbilia mapenzi katika umri mdogo. Haijaanza leo, ipo tangu miaka mingi iliyopita. Kuna tamaa pia ya watu wenye umri mkubwa kutamani mapenzi na watoto wadogo. Hao ndiyo binadamu na tabia zenye kujirudia.
Mara nyingi binadamu hujawa haraka kabla ya muda utafikiri wanachokikimbilia watakuta kimeisha. Wakati wanayoyaharakia huyakuta na kuyaacha yakiwa yamepamba moto. Aaliyah alikuwa na miaka 15 alipofunga ndoa ya siri na R Kelly aliyekuwa na miaka 27.
AALIYAH KAMA LULU
Maisha ya muziki yalimfanya Aaliyah aanze kujimilikisha kwa mwanaume akiwa binti mdogo. Alimzoea R Kelly akiwa na miaka 12 kama mwalimu wake wa muziki, mwandishi wa nyimbo zake na prodyuza wake. Miaka mitatu iliyofuata ikadhihirika walifunga ndoa ya siri.
Lulu akiwa mtoto kabisa, alidhihirisha kipaji chake cha sanaa za maigizo. Kazi yake ikamfanya azoeane na wanaume aliofanya nao kazi. Mtoto wa kike akawa na ushirikiano wa kikazi na wanaume. Tena wanaume wakubwa aliostahili kuwaita baba, wajomba na babu.
Mazingira ya kikazi yalimfanya aone ya wakubwa aliyaweza katika utoto wake. Sawa na Aaliyah, baada ya kudanganyana na R Kelly aliona ukubwa na umri ni namba tu.
Alijiona alikuwa na uwezo wa kubeba majukumu ya ndoa. Kwa hivyo alidanganya mpaka umri ili kuhalalisha mpango wake.
Ni sawa na Lulu, mwaka mmoja kabla halijamfika balaa la kifo cha aliyekuwa ‘Godfather’ wa Bongo Movie, Steven Kanumba, alifanya sherehe ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa, akautangazia umma kwamba tayari alikuwa amefikisha umri wa miaka 18.
Lulu alifanya hivyo ili apate uhuru ambao hakuustahili katika umri wake. Alitaka akiingia klabu aruhusiwe na asiulizwe. Angeonekana na mwanaume aachwe kama alivyokuwa maana alishajitangaza ni mkubwa. Wakati huo kulikuwa na lawama kwa waendeshaji wa klabu za usiku kumruhusu Lulu kuingia kisha kupigwa picha akiwa amelewa, wakati alikuwa mtoto.
Baada ya Kanumba kufikwa na mauti katika mazingira ya ugomvi na Lulu, alipofikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji ndipo ikagundulika kuwa alijibusti miaka alipojitangaza kuwa na miaka 18. Kumbe Aprili 7, 2012, Kanumba alipofariki dunia, Lulu alikuwa na umri wa miaka 16.
HAPA KWA MAJAY SASA
Tangu kale, kumekuwa na mila za watu kuposa watoto wadogo kisha wanawasubiri wakue ndipo wafunge nao ndoa.
Tanzania kuna makabila yenye desturi za aina hiyo. Wengine wanazifanyia ‘booking’ mpaka mimba, akizaliwa mtoto wa kike anakua wake. Akikua anaambiwa alishalipwa mahari kisha anaolewa.
Nidhamu ya kumsubiri mtoto akue ndipo amiliki ilimshinda R Kelly kwa Aaliyah, alimuoa kwa siri ikabumbuluka. Hawakuiweza wengine kadhaa kwa Lulu ndani ya mviringo wa Bongo Movie. Kwa ushahidi wa wazi kabisa, Kanumba hakuimudu mpaka yaliyotokea yalipotokea. Mahakama ikaambiwa kumbe Lulu na Kanumba waliitana mke na mume.
Hivi sasa imeshatangazwa na mipango inaendelea ya Lulu kufunga ndoa na Majay, ambaye pamoja na umiliki wake wa Redio EFM na luninga ya ETV, vilevile ni DJ mwenye jina kubwa Bongo. Hivyo basi, yajayo yatakuwa ya furaha kwa Lulu na Majay kwa maana watakuwa mke na mume.
Mipango yao ikiwa inaendelea, naona ni uungwana kumpongeza Majay kwanza kwa kufanikiwa kuvuka na Lulu kwenye nyakati ngumu na sasa anakwenda kuwa mume wake. Hata hivyo, muhimu zaidi ni kumpongeza Majay, kwani aliweza kumsubiri Lulu akue.
Inawezekana Majay alimtamani Lulu tangu zama hizo, lakini aliheshimu utoto wake na kumwacha akue kwanza. Ni sawa na kusema Majay hakutaka kuangua maembe yasiyoiva. Hakuwa kama wanaume ‘walafi’ waliombebesha Lulu majukumu ya mapenzi katika umri wa utoto.
Wakati Majay akipokea pongezi, upande wa pili wale wanaume waliombebesha Lulu majukumu kabla ya umri wake wanajionea kuwa ni raha sana ‘kudili’ na mtu aliyevuka daraja la utoto. Kama mwaka 2012 Lulu alikuwa na miaka 16, kwa hiyo leo ana miaka 22. Majay hafanyi siri, wala Lulu haongopi ili aolewe. Maandalizi halali yanafanyika.
Dua kwao wafikie lengo. Wale walafi wajifunze kusubiri watoto wakue kama kweli wanawapenda. Wakiwawahi kabla hawajakua, hawatakuwa na uhuru kwenye mapenzi yao. Tena wataitwa wabakaji. Na wakinaswa ni jela. Ukisubiri utakula kihalali kwa nafasi.
Heko Majay kwa subira. Naamini wewe si miongoni mwa wale waliomchangamkia Lulu alipokuwa mtoto.