Hizi nyimbo ziliwarudisha mjini
Muktasari:
- Baadhi yao hupunguza kasi ya kutoa nyimbo kwa lengo la kuboresha ubora wa kazi zao, wengine hutanguliza familia, huku baadhi wakikabiliwa na changamoto za kiafya au za maisha binafsi zinazowalazimisha kukaa mbali na studio.
KATIKA muziki, kuna wasanii ambao wanaweza kukaa miezi kadhaa au hata miaka bila kutoa kazi mpya, lakini wanapoamua kurejea, wimbo mmoja tu unatosha kuibua gumzo kubwa na kuwakumbusha mashabiki sababu ya kuwapa nafasi katika muziki.
Baadhi yao hupunguza kasi ya kutoa nyimbo kwa lengo la kuboresha ubora wa kazi zao, wengine hutanguliza familia, huku baadhi wakikabiliwa na changamoto za kiafya au za maisha binafsi zinazowalazimisha kukaa mbali na studio.
Bongofleva ina mifano ya wasanii waliowahi kupitia vipindi hivyo, akiwamo Alikiba, Darassa, Chege, Mbosso na Aslay, ambao kila mmoja ana simulizi yake kuhusu ukimya na kurejea katika muziki.
ALIKIBA
Mfalme wa Bongofleva, Alikiba, ni miongoni mwa wasanii ambao hawana kawaida ya kukimbizana na utoaji wa nyimbo kila wakati. Hata hivyo, anapoachia kazi mpya, mara nyingi huibua gumzo katika soko la muziki.
Baada ya kuachia ‘Aje’ Juni 2016, Kiba alikaa takribani mwaka mmoja kabla ya kurejea Agosti 2017 kupitia wimbo ‘Seduce Me’. Video ya wimbo huo ilifikisha watazamaji milioni moja ndani ya takribani saa 38 tangu ilipowekwa kwenye YouTube. Lakini kwa nini Kiba hapendi kukimbizana na kutoa nyimbo kila wakati? Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Machi 2020, alieleza kuwa anathamini ubora wa kazi zake na hivyo huhitaji muda wa kutosha kuziandaa. Pia alisema alikuwa akitumia muda huo kuwajenga wasanii wa lebo ya Kings Music.
Mwaka 2026 ameongeza kasi ya kutoa kazi mpya akianza na ‘Finale’ aliyomshirikisha Bien iliyotoka Machi 25 na Mei 1 aliachia ‘Bhuju’ akimshirikisha Mbosso kabla ya kutoa ‘Utanionea’ aliyomshirikisha Harmonize, Juni 5.
Lakini, Septemba 4 aliachia ‘Hater’ kisha Septemba 25 akatoa ‘Jiji’ akiwa na S2kizzy. Oktoba 23 aliongeza wimbo mwingine uitwao ‘Natubu’. Kupitia kazi hizo ameendelea kuonyesha uwezo wake wa kushirikiana na wasanii wengine ndani na nje ya Tanzania.
DARASSA
Rapa Darassa naye ni mfano wa msanii ambaye ukimya wake uliwahi kuibua maswali mengi miongoni mwa mashabiki. Baada ya kutoa ‘Hasara Roho’ Mei 5, 2017, alikaa mwaka mmoja na miezi saba kabla ya kurejea Desemba 13, 2018 kupitia wimbo ‘Tofauti’.
Katika kipindi hicho, pia alipunguza matumizi ya mitandao ya kijamii, jambo lililoibua uvumi kuhusu maisha yake binafsi. Januari 2018, alizungumza na kukanusha taarifa zilizomhusisha na matumizi ya dawa za kulevya, akieleza kuwa alikuwa akiendelea na shughuli zake binafsi pamoja na miradi aliyokuwa akiifanyia kazi.
Baada ya kurejea, aliendelea kutoa kazi mbalimbali, zikiwemo ‘I Like It’ aliyomshirikisha Sho Madjozi mwaka 2020. Wimbo huo ulipata mapokezi mazuri, huku video yake ikifikisha zaidi ya watazamaji milioni 18 kwenye YouTube. Mwaka 2026 ameendelea kuachia kazi mpya. Aprili 24 alitoa ‘Beginning’ aliyomshirikisha Khaligraph Jones na ‘Music’. Juni 12 aliachia ‘Pakata’ akiwa na G-Nako, kisha Juni 19 akatoa ‘Broken’. Julai 24 alishirikiana na Harmonize katika wimbo ‘Love Design’, huku Septemba 24 akitoa ‘Ye’ akiwa na Khadija Kopa.
CHEGE
Chege Chigunda alijijengea jina kupitia kundi la TMK Wanaume Family na baadaye kufanya vizuri kupitia nyimbo kama ‘Waache Waoane’ aliyomshirikisha Diamond Platnumz, ‘Kelele za Chura’ na ‘Kipepeo’.
Desemba 2016, Chege alieleza kuwa yeye na Temba hawakuwa na mpango wa kutoa nyimbo mpya kwa kipindi hicho kutokana na mwenendo wa soko la muziki. Alisisitiza kuwa walikuwa wakifuatilia hali ya soko kabla ya kuamua kutoa kazi nyingine.
Baada ya kipindi hicho cha kupunguza utoaji wa kazi za kundi, Chege aliendelea na muziki wake binafsi. Januari 14, 2021 aliachia EP yenye nyimbo sita iliyoitwa ‘Burudani’, ikiwa ni mradi wake wa kwanza wa aina hiyo baada ya kuanza kujitegemea nje ya kundi. Agosti 14, 2024 alimshirikisha Alikiba katika wimbo ‘Kipofu’, huku mwaka 2026 akiachia wimbo ‘Ubaya’ aliyomshirikisha Mbosso. Wimbo huo ulitoka Septemba 11.
MBOSSO
Mbosso ni miongoni mwa wasanii walioanza ukurasa mpya wa muziki baada ya kuondoka katika lebo ya WCB Wasafi. Februari 2025, aliondoka rasmi katika lebo hiyo baada ya kuitumikia kwa takribani miaka saba na kuamua kuendelea na safari yake ya muziki kupitia Khan Music.
Baada ya kuondoka, alikaa takribani miezi minne kabla ya kutangaza kazi zake za kwanza akiwa msanii huru. Kipindi hicho kilizua maswali kwa mashabiki waliokuwa wakisubiri kuona hatua yake inayofuata nje ya WCB.
Juni 13, 2025, alirejea kwa kuachia EP yenye nyimbo saba iliyoitwa ‘Room Number 3’. Mradi huo ulikuwa na nyimbo kama ‘Pawa’, ‘Nusu Saa’, ‘Tena’, ‘Merijaah’, ‘Siko Single’, ‘Aviola’ na ‘Asumani’. Miongoni mwa nyimbo zilizovuta gumzo zaidi ni ‘Pawa’, iliyopata mapokezi mazuri na kuendelea kumjengea nafasi katika muziki akiwa nje ya lebo hiyo.
ASLAY
Aslay Isihaka ni msanii mwingine aliyewahi kukaa kipindi kirefu bila kutoa kazi mpya. Baada ya kuachia ‘Nashangaa’ ya Januari 15, 2021, aliendelea kutoa wimbo ‘Mama’, Septemba mwaka huo. Baadaye alikaa kimya kwa miezi kadhaa hadi Agosti 2022, alipotangaza kujiunga na lebo ya Rockstar Africa na kueleza kuwa kipindi alichokuwa kimya kilimfundisha mambo mengi.
Akizungumzia changamoto za maisha binafsi, Aslay aliwahi kueleza kuwa kipindi cha msongo wa mawazo baada ya kuachana na mama wa mtoto wake kiliathiri hali yake na muziki.