Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hili la mistari Mbosso anaishi 'dunia' yake

MBOSSO Pict


KWA miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mijadala kuhusu ni nani mwandishi bora wa nyimbo za Bongo Fleva, na mjadala huo umechukua nafasi kubwa miongoni mwa wadau wa sanaa, mashabiki na wachambuzi wa muziki.


Katika mjadala huo, jina la Mbosso limekuwa likitajwa mara kwa mara kama msanii mwenye uwezo mkubwa wa kuandika nyimbo zenye kugusa hisia za watu wengi. Lakini je, ni kweli Mbosso ndiye mwandishi bora kwa sasa, au ni umaarufu unaomfanya aonekane hivyo?


NI NANI?

Mbosso, ambaye jina kamili ni Yusuf Kilungi, ni msanii aliyepitia hatua mbalimbali za muziki kuanzia akiwa Yamoto Band, Wasafi, hadi kuwa msanii wa kujitegemea, akiwa pia amezindua lebo yake ya Khan Music.

Mbosso alianza kupata umaarufu akiwa na kundi la Yamoto lililokuwa na wasanii wengine watatu, Aslay, Enock Bella na Beka Flavour, kupitia wimbo wa Yamoto uliotoka mwaka 2013.

Miaka miwili baadaye, kundi hilo lilifanikiwa kuchukua tuzo yao ya kwanza ya muziki za TMA kama kundi bora la mwaka la Bongofleva, likiwaacha makundi mengine yaliyokuwa yanashi-ndania tuzo hiyo, kama Makomando, B.O.B, Weusi na NavyKenzo.

Mwaka 2017, kundi hilo likatawanyika na kila mmoja akawa anafanya yake. Hata hivyo, Mbosso akasainiwa katika lebo ya WCB Wasafi, aliko-achia nyimbo kama Watakubali (2017) na vibao vikali kama Mtaalamu, Tamba, Sonona, Alele na nyinginezo.

MBOS 06

UTUNZI

Safari yake imemjenga si tu kama mwimbaji mwenye sauti ya kipekee, bali pia kama mtunzi na mwandishi wa nyimbo mwenye mtazamo wa kitofauti katika muziki wa mapenzi.

Uandishi wake umejikita zaidi katika kuwasilisha hisia halisi za uhusiano, maumivu ya mapenzi, uvumilivu na matumaini, mada zinazogusa maisha ya watu wengi.

Kipimo kikubwa cha kupima ubora wa mwandishi bora ni muitikio wa kazi zake kwa jamii. Mbosso ni miongoni mwa wasanii waliopata usikilizaji mkubwa kwenye majukwaa ya kidijitali kama YouTube, Boomplay na Spotify.

MBOS 05

Nyimbo zake nyingi zimefikisha mamilioni ya streams, jambo linaloonyesha kuwa ujumbe na maneno yake yanafika na kukubalika kwa wasikilizaji wa rika na maeneo tofauti.

Mfano mzuri ni wimbo wa Darasa la Saba uliotoka siku chache zilizopita; ndani ya muda mchache tu uliingiza zaidi ya watazamaji milioni moja na sasa unaongoza kwa kusikilizwa Afrika Mashariki kupitia mtandao wa Audiomack.

Hii si bahati mbaya, bali ni matokeo ya uandishi unaoeleweka, unaohusisha hisia na unaoendana na uzoefu wa maisha ya watu wa kawaida.

MBOS 04

Kinachomtofautisha Mbosso na waandishi wengine ni urahisi wa lugha anayotumia. Hatumii maneno mazito au mafumbo yanayohitaji elimu ya juu kuyafasiri. Badala yake, anaandika kwa lugha nyepesi, ya moja kwa moja, lakini yenye uzito wa kihisia.

Mistari yake mara nyingi inajengwa juu ya simulizi linaloweza kumgusa mtu aliyewahi kupenda, kuumizwa au kutamani mapenzi ya dhati. Uandishi wa aina hii humfanya msikilizaji ajione kama sehemu ya wimbo.

Wimbo wa Nusu Saa kutoka kwenye albamu yake ya Room Number 3 ni wimbo unaoelezea simulizi yenye hisia; anasimulia jinsi kumpata mwenzi wake kulivyomletea amani na matumaini baada ya maisha ya kutelekezwa na kuvunjika moyo.

MBOS 03

Kiitikio kinasisitiza kuwa hata ‘Nusu Saa’ haitoshi anapokuwa na yule anayempenda ishara ya ukaribu wa kihisia na mapenzi ya dhati aliyonayo. Kwa mistari ya kishairi, midundo laini na uwasilishaji wa kutoka moyoni, wimbo huo unaelezea kwa uzuri furaha ya mapenzi anayohisi kama kamba ya uhai baada ya giza.

Ingawa inajadiliwa kwamba Mbosso ndiye mwandishi bora, tasnia ya muziki Tanzania ina waandishi wengi wenye uwezo mkubwa. Wasanii kama Marioo, Jay Melody, Harmonize, Darassa, Vanillah na wengineo pia wamekuwa wakionyesha ubora mkubwa katika kuandika nyimbo zenye ujumbe, hadithi na mbinu tofauti za kisanaa.

Tofauti kubwa ni kwamba Mbosso amejikita zaidi katika hisia za mapenzi, wakati wengine wanagusa pia masuala ya kijamii, mafanikio, changamoto za maisha na mitazamo ya kizazi kipya.

MBOS 02

Kiitaalamu, ubora wa mwandishi haupimwi tu kwa idadi ya nyimbo zinazopendwa, bali pia kwa ubunifu, ujumbe na uwezo wa kuandika mada tofauti. Mbosso anaonekana kuwa imara zaidi katika eneo la mapenzi, lakini bado kuna mjadala iwapo anaweza kupanua zaidi wigo wa uandishi wake na kuendelea kubaki trending.

Hata hivyo, sio kosa kwa msanii kuwa na eneo analolitawala vizuri, mradi afanye kwa ubora wa hali ya juu, jambo ambalo Mbosso amefanikiwa.

Ni muhimu pia kutambua kuwa muziki ni sanaa inayotegemea ladha ya msikilizaji. Kwa mashabiki wa nyimbo za hisia na mapenzi, Mbosso anaonekana bila shaka kuwa mwandishi bora zaidi kwa sasa.

Mbosso ni shabiki mkubwa wa muziki wa Bollywood, India; ndio maana hujiita “Muhindi wa Kusini” na muziki wa nchi hiyo asilimia kubwa unaogusa hisia zaidi kuliko kucheza.

MBOS 01

Kwenye listi ya nchi zinazoongoza kwa kuuza muziki duniani, India ipo nafasi ya 17, ishara kwamba muziki wa hisia unauza zaidi. Ndiyo maana hata Mbosso anafanya vizuri zaidi eneo hilo kutokana na kuwafikia mashabiki wengi.

Hata kwenye ngoma zake, amekuwa na utaratibu wa kuchanganya na lugha ya Kihindi; mfano, kwenye wimbo wa Darasa la Saba, kuna maneno kama Tere Liye, Tere Sanam. Kiitikio chake ametoa kwenye wimbo wa Tere Liye ulioimbwa na wakongwe wa India, Lata Mangeshkar na Roop Kumar Rathod.

Kwa ujumla, kwa kuangalia takwimu za usikilizaji, mvuto wa kazi zake, lugha anayotumia na namna anavyogusa hisia za wasikilizaji, Mbosso ni mmoja wa waandishi bora wa Bongo Fleva kwa sasa Tanzania.

Msanii huyo amefanikiwa kujijengea utambulisho wa kipekee kama mtunzi wa nyimbo za mapenzi zenye nguvu ya kihisia na mvuto wa kibiashara. Mbosso si tu mwimbaji mzuri, bali pia ni mwandishi mwenye ushawishi mkubwa katika muziki wa kizazi cha sasa. Ubora wake upo wazi, takwimu zinambeba na kazi zake zinaishi katika mioyo ya mashabiki.