Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Harmonize, Rayvanny walivyovunja ‘ukuta WCB’ kuungana na Alikiba

WCB Pict

Muktasari:

  • Hata hivyo, upepo ulibadilika mara tu baada ya Harmonize na Rayvanny kufanya uamuzi wa kujitegemea na kuondoka WCB Wasafi. Ukaribu wao mpya na Alikiba pamoja na kuachia ngoma za pamoja umesababisha mijadala, huku baadhi ya mashabiki wakidai ni mkakati wa kuungana dhidi ya Diamond. Lakini ukweli wa picha hilo unakwenda mbali zaidi ya fikra hizo.

Katika ulimwengu wa Bongo Fleva, siasa za kimuziki na tofauti za makambi zimekuwa zikichukua nafasi kubwa katika kuamua nani anashirikiana na nani. Kwa miaka mingi, baadhi ya mashabiki na wadau wa muziki walijenga taswira kwamba msanii anayefanya kazi chini ya lebo ya WCB Wasafi inayomilikiwa na Diamond Platnumz, hawezi au hapaswi kuwa na ukaribu na Mfalme wa King’s Music, Alikiba.

Hata hivyo, upepo ulibadilika mara tu baada ya Harmonize na Rayvanny kufanya uamuzi wa kujitegemea na kuondoka WCB Wasafi. Ukaribu wao mpya na Alikiba pamoja na kuachia ngoma za pamoja umesababisha mijadala, huku baadhi ya mashabiki wakidai ni mkakati wa kuungana dhidi ya Diamond. Lakini ukweli wa picha hilo unakwenda mbali zaidi ya fikra hizo.

WC 03

Kutoka uhasama wa lebo hadi urafiki mitaani, studio

Wakiwa ndani ya lebo ya WCB, wala Harmonize wala Rayvanny hakuwahi kuonekana karibu na Alikiba. Nyakati hizo zilitawaliwa na utani, majisifu, na mara kadhaa vijembe vya kimuziki vilivyoakisi ushindani wa pande hizo mbili.

Lengo kuu la Lebo zote mbili lilikuwa kulinda utawala na umaarufu wao. Kutokana na mazingira hayo, wazo la Rayvanny au Harmonize kuingia studio na Alikiba lilichukuliwa kama jambo lisilowezekana.

Hatua ya wasanii hao kujitoa WCB haikutenganisha tu mikataba yao ya kazi, bali pia ilivunja mipaka ya kihisia iliyowatenganisha na wasanii wengine, ikiwemo Alikiba. Mashabiki wameanza kuwashuhudia wakikutana kwenye matukio mbalimbali ya kijamii, kwenye mahojiano, na hata kubadilishana mawazo kwa furaha, jambo lililoshitua wengi.

WC 02

Muziki unavyoongea, ‘Utanionea’ na ‘Naoa’

Ukaribu huu haukuishia tu kwenye picha za mitandaoni au salamu za mara kwa mara; uliingia hadi kwenye chumba cha kurekodia nyimbo

Harmonize na Alikiba “Utanionea”,  ushirikiano huu ulikuwa moja ya matukio makubwa zaidi ya kimuziki. Ulileta mshtuko chanya kwa mashabiki waliokuwa wamezoea kuwaona kama ‘pande mbili tofauti ‘.

Ngoma hii ilidhihirisha jinsi ushindani unavyoweza kubadilishwa kuwa mshikamano wenye tija.

Rayvanny na Alikiba “Naoa”  Rayvanny naye alifuata nyayo hizo kwa kuachia kibao hiki kitamu na Alikiba. Hatua hii ilipongezwa sana kama ishara ya kukua kwa ukomavu wa kimuziki na kuvunja miiko ya zamani iliyojengwa na ushabiki wa Lebo.

WC 05

Wenyewe wamezungumza

Mijadala inapoendelea uraiani, Mwanaspoti limewatafuta na kuweka wazi mtazamo wao kuhusu uhusiano huo mpya.

Rayvanny kuhusu Alikiba: “Alikiba ni kaka yangu na ni mwanamuziki mkubwa ambaye nimemkuta kwenye hii tasnia. Kipindi cha nyuma mambo yalikuwa tofauti kwa sababu ya mazingira na ushindani wa kibiashara, lakini muziki ni upendo. Kufanya naye kazi ni heshima na ni kuonyesha kwamba Bongo Fleva ipo moja.”

WC 01

Harmonize kuhusu Alikiba anasema: “Mimi sina tatizo na mtu yeyote kwenye hii sanaa. Alikiba ni Legend na mtu ambaye namheshimu sana kwa mchango wake. Kuonekana naye au kufanya naye kazi siyo kwa ajili ya kupambana na mtu mwingine, bali ni kuonyesha mfano kwa mashabiki kwamba Bongo Fleva inahitaji mshikamano ili ifike mbali zaidi.”

Hata hivyo, Alikiba aliwahi kuwazungumzia hivi Rayvanny na Harmonize kuhusu ukaribu wao: “Sijawahi kuwa na chuki na msanii yeyote. Wote ni wadogo zangu na ni wasanii wakali sana wenye talent yao. Zamani kulikuwa na mambo ya kitoto na ushabiki wa mashabiki, lakini sasa hivi wamekuwa na wanajituma kwa ajili ya muziki wao. Milango yangu ipo wazi muda wote kufanya kazi na mtu yeyote anayeheshimu kazi.”

WC 04

Tafsiri ya mashabiki na uhalisia wa sanaa

Licha ya ushahidi kuwa ukaribu huu unalenga kukuza muziki na kujenga ukomavu, sehemu ya jamii na mashabiki wa Bongo Fleva bado inatafsiri ushirikiano huu kama muungano wa “adui wa adui yangu ni rafiki yangu.”

Ukweli ni kwamba, Rayvanny na Harmonize wametoka kwenye mfumo uliowalea na kuingia kwenye soko huru linalohitaji mahusiano mapana ili kubaki kileleni. Ukaribu wao na Alikiba si mkakati wa vita, bali ni hatua ya busara ya kibiashara na kiutamaduni inayothibitisha kuwa muziki ni chombo cha kuunganisha watu na sio kuwatenganisha.